The House of Favourite Newspapers

Tanzania Kuwa Mwenyeji Mkutano  wa Kimataifa Kujadili Changamoto za Usonji na Utindio wa Ubongo

0
Mkurugenzi wa taasisi ya Victorious Centre of Excellence Bi Sarah Laiser (katikati) akizungumza na waandishi wa Habari kuhusiani na ujio wa Mkutano wa Kimataifa unaolenga kujadili changamoto zinazohusiana na usonji na utindio wa ubongo utakaofanyika tarehe 2 hadi 3 Disemba mwaka huu katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC), Dar es Salaam. Mkutano huo muhimu umeandaliwa kwa ushirikiano baina ya taasisi ya Victorious Centre of Excellence na Autism Connect. Wengine ni pamoja na Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa taasisi ya Autism Connect Bi Dolly Thakkar (Kushoto) na  Mtaalamu wa Masuala ya Afya Dk Issack Maro (Kulia)

Tanzania inatazamiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimatifa unaolenga kujadili changamoto zinazohusiana na usonji na utindio wa ubongo utakaofanyika tarehe 2 hadi 3 Disemba mwaka huu katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Centre (JNICC), Dar es Salaam.

Mkutano huo muhimu umeandaliwa kwa ushirikiano baina ya taasisi ya Victorious Centre of Excellence na Autism Connect. Victorious Centre of Excellence ni kituo kinachotoa huduma mbalimbali za tiba ya urekebishaji (rehabilitation therapies) na shughuli za ziada kwa watoto wenye hali ya usonji nchini Tanzania kwa lengo la kuwajumuisha katika jamii kupitia juhudi makini za kujenga uelewa wa kijamii. Autism Connect ni taasisi ya kimataifa iliyojikita kwenye kueneza ufahamu, kutoa elimu na kuwezesha utunzaji wa kina kwa watu wenye changamoto za usonji kwa nchi mbalimbali duniani.

Juhudi hizo za pamoja zimefanikisha ujio wa mkutano huo wa siku mbili, ambao utakuwa na lengo la kuongeza ufahamu kuhusu usonji na kutoa jukwaa kwa wataalamu kutoka duniani kote kubadilishana uzoefu na kujadili maendeleo ya hivi karibuni kuhusiana na changamoto hiyo. Mgeni rasmi kwenye Mkutano huo anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Ummy Alli Mwalimu (Mb), Waziri wa Afya, ambaye ataongeza umuhimu zaidi katika mkutano huo.

Akizungumza na wadau wa habari jijini Dar es Salaam, mapema siku ya Alhamisi, Mkurugenzi wa taasisi ya Victorious Centre of Excellence ambae pia ni Mwenyekiti wa Mkutano huo, Bi Sarah Laiser alieleza kufurahishwa kwake na mkutano huo akisema, “Tunafuraha kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huu muhimu, kwani unatoa fursa maalum kwa wataalamu wa matibabu kuungana na wenzao kutoka maeneo mbalimbali duniani wanaoshughulika na changamoto ya usonji’’

Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa taasisi ya Autism Connect Bi Dolly Thakkar (Katikati) akizungumza na waandishi wa Habari kuhusiani na ujio wa Mkutano wa Kimataifa unaolenga kujadili changamoto zinazohusiana na usonji na utindio wa ubongo utakaofanyika tarehe 2 hadi 3 Disemba mwaka huu

Alisema, zaidi mkutano huo unalenga kuwezesha kubadilishana mawazo na matokeo ya kimatibabu kati ya wazazi na wataalamu, na hatimaye kupelekea huduma bora kwa watu binafsi walio na changamoto hiyo.

Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo kutokana na changamoto za kipekee ambazo bara la Afrika inakabiliana nazo katika kukabiliana na usonji, kwa mujibu wa waandaaji hao.

“Kuongezeka kwa watu wenye changamoto ya usonji ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa. Kituo cha Kudhibiti Magonjwa (CDC) nchini Marekani kinaripoti takwimu za kustaajabisha. Katika kila mtoto mmoja  kati ya watoto 36 nchini Marekani amegundulika kuwa na changamoto ya usonji. Tafiti hiyo ilifafanua kwamba kati ya watoto 37 wa kiume mmoja wao huwa na changamoto ya Usonji. ‘’

“Zaidi, tafiti hiyo ilibaini kati ya watoto 157 wa kike mmoja wao hubainika na changamoto ya usonji. Hii inaonesha watoto wa kiume hupatwa na tatizo hili mara nne zaidi ya watoto wa kike. Kwa hapa Tanzania, takwimu zetu wenyewe zinaonyesha ongezeko kubwa la tatizo hili katika miongo miwili iliyopita, huu ni  wito wa kuchukua hatua, wito wa kujibu kwa huruma, uelewa, na kwa hatua madhubuti.’’ Alibainisha.

Alisema, watoto walioathiriwa na usonji hukumbana na changamoto katika mawasiliano, kushindwa kutamka maneno vizuri, hukabiliwa na ugumu katika kupokea mafunzo ya kielimu na mara nyingi huonyesha tabia za ukorofi kupindukia.

Kwa mujibu wa Bi Sarah Laiser, changamoto zitokanazo na hali ya usonji kwa kiasi kikubwa zinachangiwa na ukosefu wa ufahamu na imani za kiasili zinazoambatana na hali hii barani Afrika. “Kwa kuzingatia changamoto hizi, mkutano huu unatoa matumaini kwa watoto wetu. Na hii ndio sababu tunasisitiza kwamba mkutano huu sio tu kama tukio lingine lolote bali ni kichocheo cha mabadiliko, kinachoangazia njia kuelekea siku zijazo ambao ni angavu kwa watu kwenye changamoto ya usonji,’’ Alisema Bi Sarah Laiser.

Zaidi, akizungumzia Mkutano huo Bi Dolly Thakkar, Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa taasisi ya Autism Connect, alisema mkutano huo utawaleta pamoja wataalamu kutoka Tanzania, Kenya, na Uganda, pamoja na wajumbe kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Kwa mujibu Bi Thakkar tukio hilo la kipekee ni fursa nzuri kwa wataalamu kuangazia kazi zao, kubadilishana ujuzi, na kuwasiliana na wenzao ambao wanaendeleza maendeleo katika utafiti na utunzaji wa taarifa kuhusu usonji.

“Hivyo, wazazi wa watoto wenye mahitaji maalum kutoka nchi mbalimbali duniani watapata fursa ya kujifunza kuhusu hatua muhimu iliyofikiwa katika nchi zao na kimataifa kuhusiana na changamoto hii. Maendeleo mapya na ya hivi punde zaidi ya utafiti yanayotokea ulimwenguni kote, pamoja na matibabu mapya ya usonji, yatajadiliwa. Mkutano huu utatoa jukwaa la kipekee la kisayansi na majadiliano ya kimatibabu, na walengwa wa mwisho wakiwa ni watoto kwenye tatizo la usonji.’’ Alibainisha.

Bi. Thakkar aliongeza kuwa mkutano huo pia utashirikisha wazungumzaji mashuhuri kutoka nchi mbalimbali  duniania zikiwemo Tanzania, Uingereza, Zimbabwe, Kenya, India, Marekani,  Afrika Kusini, Belgium, Italy na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

“Jambo zuri ni kwamba, Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Alli Mwalimu (Mb), atapamba mkutano huo kwa uwepo wake. Mahudhurio yake yanaashiria wazi dhamira na msaada wa Serikali katika kuboresha maisha ya watu wenye usonji nchini.’’ Alibainisha

Leave A Reply