The House of Favourite Newspapers

Tanzania, Marekani Kushirikiana Kiutalii

0

Tanzania na Jimbo la Dallas la nchini Marekani zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika nyanja za utalii, michezo, uwekezaji pamoja na kubadilishana uzoefu katika masuala ya uhifadhi wa maliasili pamoja na uendelezaji Utalii.

Makubaliano hayo yamefikiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro (Mb) pamoja na viongozi mbalimbali katika Jimbo la Dallas wakati walipofanya vikao vilivyokuwa na lengo la kujifunza namna wanavyoendesha shughuli za utalii pamoja kukuza ushirikiano baina ya pande zote mbili.

“Tumezungumzia masuala ya kuimarisha uhusiano wetu baina ya Tanzania na Jimbo la Dallas pamoja na kuangalia namna tunavyoweza kuliteka soko la watalii katika Jimbo hilo, tumejadili mikakati ya kuanza na watalii ambao ni wanafunzi wa vyuo vikuu katika jimbo hilo lengo likiwa ni kupata soko la uhakika la watalii wengi zaidi katika siku za usoni,” Amesema Waziri Ndumbaro.

Akizungumza na Mkurugenzi wa Idara ya Utalii wa Jimbo la Dallas Liliana Rivera, Dkt. Ndumbaro amesema moja ya shabaha kubwa ni kuhakikisha kunaanzishwa ndege ya moja kwa moja ya kutoka Tanzania hadi Dallas ambapo amesema itaweza kusaidia Watanzania ambao ni watalii kwenda Dallas na Watalii kutoka Dallas kutembelea Tanzania.

Katika ziara hiyo pia, Waziri Ndumbaro amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Mchezo wa Gofu nchini Marekani, Bruce Davidson ambapo Dkt. Ndumbaro ametumia fursa hiyo kuinadi Tanzania kuwa ipo tayari kuwa Mwenyeji wa mashindano makubwa ya mchezo wa gofu duniani.

Leave A Reply