The House of Favourite Newspapers

Tanzia: Mchungaji Mtikila afariki kwa ajali Chalinze

0

Mch.Christopher Mtikila.

Mwanasiasa mashuhuri nchini na Mwenyekiti wa Chama Cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amefariki dunia na watu wengine watatu kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea katika Kijiji cha Msolwa kilichopo Chalinze mkoani Pwani alfajiri ya leo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Jafari Mohamed, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa “Taarifa za mwanzo” zinasema Mtikila amefariki majira ya saa 11:45 alfajiri ya leo katika kijiji cha Msolwa, Chalinze.

Mwili wa marehemu Mtikila baada ya ajali hiyo.

Amesema gari alilokuwa amepanda Mtikila lilikuwa linatoka mkoani Morogoro kwenda Dar es Salaam, ndani ya gari hilo kulikuwa na watu wanne ambapo wengine watatu wamejeruhiwa vibaya na kupelekwa katika Hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha, Pwani kwa matibabu.

Wasifu wa Mchungaji Mtikila

Mtikila alizaliwa mkoani Iringa mwaka 1950. Pamoja na shughuli za siasa, Mchungaji Mtikila ni mwanzilishi na mkuu wa Kanisa la Kipentekoste la Full Salvation Church.

Enzi za uhai wake Mchungaji Mtikila alikuwa akijihusisha pia na harakati za haki za binadamu kupitia kitengo cha haki za binadamu cha kanisa hilo kiitwacho Liberty Desk.

mtikila

Gari alimokuwa Mtikila wakati wa ajali.

Maisha yake katika siasa

Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Mchungaji Mtikila alijipatia umaarufu mkubwa katika siasa za Tanzania kutokana na uwezo wake mkubwa wa kujenga hoja, upinzani wake dhidi ya muundo wa muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, madai yake kuhusu uhujumu wa uchumi uliokuwa unafanywa na wahindi (ambao aliwaita Magabacholi), na kesi mbalimbali za kikatiba alizokuwa akifungua katika mahakama za Tanzania.

Kwa muda mrefu chama chake cha DP hakikuweza kupata usajili wa kudumu kutokana na kukataa kwake kuitambua Zanzibar.

Alikuwa akisisitiza kuwa chama chake ni cha Tanganyika na siyo Tanzania. Hata hivyo Mtikila alibadili msimamo wake katika miaka ya karibuni kwa kukubali kutafuta wanachama kutoka Zanzibar (kama sheria ya uchaguzi inayotaka) na hivyo chama chake kuweza kupata usajili wa kudumu.

Mtikila alikuwa ni kati ya wagombea 10 wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005. Katika uchaguzi huo alipata asilimia 0.27 ya kura zote.

Kesi na kifungo

Kesi za kikatiba ambazo amewahi kufungua ni pamoja kesi ya kutaka wagombea binafsi kuruhusiwa katika uchaguzi Tanzania, wananchi wa Tanzania Bara kuruhusiwa kwenda Zanzibar bila pasipoti, na vyama vya siasa kuruhusiwa kufanya mikutano bila kuomba kibali kutoka kwa mkuu wa wilaya na polisi.

Mtikila alifungwa kwa mwaka mmoja mwaka 1999 baada ya kupatikana na hatia ya kutoa maneno ya kashfa dhidi ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, marehemu Horace Kolimba.

Mwaka 2004 alihukumiwa kifungo kilichosimamishwa cha miezi sita kwa kutoa maneno ya kashfa dhidi ya mkuu wa polisi wa wilaya ya Ilala.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. AMEN

Leave A Reply