The House of Favourite Newspapers

TANZIA: Mtendaji Mkuu wa Safaricom Afariki Dunia

TANZIA: Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya mawasiliano nchini Kenya (Safaricom), Bob Collymore,  amefariki dunia leo asubuhi, Julai 1, 2019.

 

Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Safaricom, Nicholas Nganga,  imesema Collymore alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya saratani kwa muda mrefu.

 

“Oktoba 2017 alienda Uingereza kwa matibabu na akarejea Julai 2018 kuendelea na majukumu yake huku akihudhuria hospitali kila ilipobidi. Mara ya mwisho alikuwa anatibiwa katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan hapa Nairobi kabla hali yake haijawa mbaya zaidi,” amesema Nganga.

 

Raia huyo wa Uingereza ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya taasisi ya saratani nchini Kenya, ameacha mke, Wambui Kamiru, na watoto wanne.

 

Kifo cha Collymore (61), kimetokea mwezi mmoja kabla hajastaafu kwani alipanga kuachia wadhifa huo Agosti mwaka huu.

 

Katika kipindi cha uongozi wake katika kampuni hiyo kubwa ya mawasiliano Afrika Mashariki, Safaricom imeweza kuisogeza mbele huduma ya M-Pesa iliyozinduliwa mwaka 2007, hivyo kuleta mageuzi katika sekta ya fedha Afrika.

Comments are closed.