The House of Favourite Newspapers

TANZIA: Waziri wa Kikwete Afariki Dunia

ALIYEWAHI kuwa Waziri wa Uchukuzi katika Serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete, na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Simu Mawasiliano Tanzania (TTCL), Omari Rashid Nundu (71) amefariki dunia wakati akiwa njiani akipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya matibabu.

 

Taarifa iliyotolewa leo mchana na Kitengo cha Mawasiliano cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imeeleza kuwa, Nundu alifikishwa hospitalini hapo kwa gari binafsi la kubeba wagonjwa.

 

Februari 27, 2017, Rais Dkt. John Magufuli alimteua Omary Nundu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la TTCL.  Nundu aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tanga kuanzia mwaka 2010 hadi 2015

******

Taarifa iliyotolewa leo mchana Jumatano Septemba 11, 2019 na Kitengo cha Mawasiliano cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dar es Salaam kimesema, “Waziri wa zamani Omary Nundu alifikishwa leo MNH, akitokea nyumbani kwa gari binafsi la wagonjwa akiwa tayari ameshafariki.”

“Hivyo waliomleta waliamua wakahifadhi mwili wake katika hospitali ya rufaa ya Jeshi Lugalo,” imeeleza taarifa hiyo.

Dk Nundu enzi za uhai wake aliwahi kuwa mbunge wa Tanga na Waziri wa Uchukuzi katika Serikali ya awamu ya nne ya Tanzania.

Juni 12, 2019, Rais wa Tanzania, John Magufuli alimteua Dk Nundu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Airtel Tanzania ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Bharti Airtel International.

Katika makubaliano hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Airtel Tanzania pamoja na ofisa mkuu wa ufundi wanapaswa kuteuliwa na Serikali.

Historia Ya Marehemu, Omary Nundu

Omari Rashid Nundu, alizaliwa Tanga, Tanzania mwaka 1948 na huko ndiko alikopata elimu yake ya shule kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Glasgow, Scotland mwaka 1971 kusomea uhandisi na sayansi ya vyombo vya anga (Aeronautical Engineering); na baadaye kuendelea na shahada za juu na utafiti vyuo vikuu vya Cranfield, England na Concordia, Canada.

Omari amebahatika kufanya kazi kwenye taasisi mbalimbali duniani katika kuitendea haki taaluma hiyo aliyoisomea na anayoipenda. Kwa nyakati mbalimbali alikuwa mhandisi na mkurugenzi kwenye mashirika ya ndege, alikuwa mshauri na mhadhiri kwenye vyuo vya kimataifa, na pia alikuwa mkuu wa vitengo vya usafiri wa anga katika jumuia za kimataifa.

Kabla ya kurejea Tanzania na kuwa mbunge wa Tanga na pia Waziri wa Uchukuzi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikuwa Rais wa jopo la kimataifa la magwiji wa taaluma ya Usafiri wa Anga Duniani (Air Navigation Commission) kwa miaka miwili mfululizo

Ingawa ni mhandisi na mwana sayansi aliyebobea, Omari anapenda kuongea lugha mbalimbali lakini ana mapenzi ya dhati kwa lugha ya Kiswahili ambayo ndiyo iliyomkuza. Hivyo basi kuwa yeye ni malenga wa mashairi halishangazi. Utenzi uliomo mwenye kitabu hiki unajaribu kusimulia maisha na mwenendo wa Dunia kwa kadri alivyoyashuhudia mhandisi huyu hadi mwaka 2015.

Comments are closed.