The House of Favourite Newspapers

TATIZO LA KUKOSA HEDHI (AMENORRHEA) – 2

KARIBUNI tena katika safu yetu ya Afya. Kama mtakumbuka wiki iliyopita tulianza somo letu hili la tatizo la kukosa hedhi ambalo kitaalamu tunaita Amenorrhea.  Sasa tumalizie somo letu ambalo naamini litakusaidia sana wewe mwanamke unayesoma ukurasa huu.

 

JE, NI VIPIMO GANI VINATAKIWA KUFANYIKA ILI KUCHUNGUZA TATIZO HILI?

-Kupima damu kwa ajili ya kuchunguza kiwango cha homoni za FSH, LH, TSH na Prolactin ambazo uzalishwaji wake unachochewa na tezi ya pituitary, na pia kupima kiwango cha homoni ya Oestrogen inayozalishwa na matai ya mwanamke (ovaries).

-Kipimo cha Ultra-sound ya nyonga kwa ajili ya kuchunguza uwepo wa matatizo katika njia ya uzazi na pia kuchunguza hali ya mayai ya mwanamke.

-CT Scan au MRI ya kichwa kwa ajili ya kuchunguza uwepo wa matatizo kwenye tezi ya pituitary au hypothalamus.

 

-Vipimo vya kufahamu ufanyaji kazi wa tezi ya thyroid

-Kupima damu ili kufahamu kiwango cha homoni ya prolactin katika damu

-Kuchunguza uterus kwa kutumia aina ya X-Ray inayoitwa Hysterosalpingogram na kipimo kingine kiitwacho Hysteroscopy ambacho huchunguza chumba cha uterus.

MATIBABU YA KUKOSA HEDHI

Matibabu ya kukosa hedhi yanaweza kufanyika nyumbani bila kuhitaji dawa, ingawa pia, kutegemeana na chanzo cha tatizo, yanaweza kuhitaji dawa na hata upasuaji wakati mwingine.

 

MATIBABU YASIYOHITAJI DAWA

Baadhi ya wanawake wanaopata tatizo la kukosa hedhi kwa sababu ya kujinyima kula (wanaofanya dieting) na hivyo kupata upungufu wa virutubisho mwilini, wanashauriwa kula lishe bora. Baadhi ya wanawake wanaopata tatizo hili la kukosa hedhi kwa sababu ya kuongezeka uzito kupitiliza, wanashauriwa kuwa makini katika aina ya vyakula wanavyokula ili kuwa na uzito unaotakiwa.

 

Wanawake wanaokosa hedhi kwa sababu ya kufanya mazoezi ya mwili kupita kiasi wanashauriwa kujiwekea kiasi katika ufanyaji wao wa mazoezi. Iwapo kukosa hedhi kumesababishwa na msongo wa mawazo, ni jambo jema kutafuta njia za kushughulikia matatizo hayo na kuyatatua ili kuondoa msongo wa mawazo Inashauriwa kutokuvuta sigara na kuacha kunywa pombe.

 

MATIBABU YANAYOHITAJI DAWA

Matibabu ya kukosa hedhi hutegemea chanzo cha tatizo. Matibabu huelekezwa katika kutibu chanzo, na iwapo chanzo cha tatizo ni matatizo ya kimaumbile, upasuaji unaweza kufanyika.

Kwa wanawake wenye matatizo ya kuwa na kiwango kingi cha prolactin, daktari anaweza kushauri matumizi ya dawa aina ya bromocriptine au pergolide. Kwa wanawake wenye upungufu wa homoni ya Oestrogen au wale wenye matatizo katika ovary zao, dawa zenye kurejesha homoni hiyo zaweza pia kutumika.

 

Wakati mwingine dawa za uzazi wa mpango zaweza kutumika kurejesha mzunguko wa hedhi na pia kusaidia kuongeza kiwango cha homoni ya oestrogen mwilini.

UPASUAJI

Upasuaji unaweza kufanywa iwapo kuna:

-Uvimbe katika ubongo unaoathiri tezi ya pituitary na hypothalamus

-Matatizo katika njia ya uzazi ya mwanamke

Je kukosa hedhi kunaweza kusababisha mwanamke asipate mtoto?

 

Ikumbukwe kuwa, kukosa hedhi si ugonjwa bali ni dalili ya kuwepo tatizo hivyo basi iwapo tatizo hilo lina uhusiano na kutunga mimba na kupata mtoto, uwezekano wa kupata mtoto utakuwa mdogo ikiwa tatizo hilo halitashughulikiwa.

Matatizo kwenye tezi za pituitary, hypothalamus pamoja na ovary ambayo yana uhusiano mkubwa na kukosa hedhi, husababisha pia tatizo la ugumba. Iwapo matatizo hayo yatashughulikiwa ipasavyo, uwezekano wa kupata kupata hedhi na hatimaye kupata mimba huwa mkubwa.

MWISHO

Comments are closed.