The House of Favourite Newspapers

TATIZO LA WATOTO KUKOJOA KITANDANI LINATIBIKA

TATIZO la kukojoa kitandani kwa jina la kisayansi linaitwa enuresis ambapo mtoto aliye katika umri ambao uwezo wa kuzuia mkojo unatarajiwa; anakua bado anaendelea kukojoa kitandani au kwenye nguo.  

 

Tatizo la kukojoa kitandani lipo la aina mbili, wakati wa usiku (nocturnal enuresis) na lile la kujikojolea wakati wa mchana (diurnal enuresis). Tunaweza kusema enuresis ni tatizo la kushindwa kuzuia mkojo wakati wa mchana au usiku katika umri wa miaka mitano au zaidi. Idara ya magonjwa ya akili hospitalini ndiyo inayohusika kutoa matibabu ya tatizo hilo ambalo lipo katika kundi la magonjwa ya akili.

 

Kukojoa kitandani ni tatizo la kiakili, kawaida tatizo huanza kujitokeza wakati wa ukuaji wa mtoto, lakini kwa kuwa wengi hawajui, huchukulia kama ni hali ya kawaida na kwamba litaisha kadiri mtoto anavyoendelea kukua. Ingawa wapo ambao huacha kukojoa kitandani bila kwenda hospitali, wengine kwa kukosa matibabu hali hiyo huendelea nayo hadi wanapofikia umri wa ujana au kuoa au kuolewa.

 

Watoto wengi wanaacha kukojoa kitandani usiku katika umri wa miaka mitatu. Asilimia tano hadi 15 ya watoto wa miaka mitano wanaoendelia kijikojolea kitandani wengi wao ni wavulana ambayo ni asilimia saba kuliko wasichana ambayo ni asilimia tatu.

 

Katika miaka 15 wanaoendelea kujikojoa kitandani ni asilimia mbili hadi tatu tu, na asilimia moja tu katika miaka 18. Mkojo unapohifadhiwa katika kibofu cha mkojo, kibofu kinatanuka kama puto. Katika sehemu fulani neva za kutanua kuta za kibofu cha mkojo zinapeleka ishara ya kuzuia mkojo katika akili.

 

Hii hutokea katika sehemu ya ubongo inayohusika na matendo yasiyo ya hiari. Kama ubongo wa mtoto haujapaya ishara hii, au ukishindwa kujua maana ya hiyo ishara, hatua ya makusudi ya kuzuia mkojo haitafanyika.

 

Hii mara nyingi husababishwa na kuchelewa kwa ukuaji wa kibiologia wa utenda kazi wa kuzuia mkojo. Ukuaji wa kijinsia unaweza kusababishwa na kushindwa kwa akili kutambua ishara kutoka kwenye kibofu cha mkojo; ujazo mdogo wa kibofu cha mkojo; au usingizi nzito.

Zipo sababu nyingi zinazochochea mtoto kupata matatizo ya akili na kujikojolea kitandani, ikiwamo mjamzito kukaa na uchungu kwa muda mrefu. Pia mtoto hupata tatizo iwapo mama akikaa na uchungu muda mrefu wakati wa kujifungua, hali hiyo husababisha athari kwenye ubongo wa mtoto, kwani hukosa oksijeni ya kutosha.

 

Yapo pia baadhi ya magonjwa ambayo mama akiugua katika kipindi cha ujauzito huweza kumsababishia mtoto athari katika ubongo wake hivyo kumfanya akojoe kitandani, ndiyo maana wataalamu wa afya husisitiza mama afike kliniki kipindi chote cha ujauzito. Ni muhimu kutambua kwamba watoto hawajikojolei kwa makusudi na kawaida huona aibu, kwa sababu hiyo wazazi wasiwadhalilishe kwa kuwaaibisha au kuwaadhibu.

 

Mara nyingi tatizo la kujikojolea limegawanyika katika sahemu mbili, ya kwanza ni pale mtoto anaposhindwa kukuza uwezo wa kuzuiya mkojo tangu utoto wake, ya pili ni pale mtoto anaweza kujizuia kujikojolea kwa miezi sita au zaidi, halafu anaanza kujikojolea tena.

 

Tafiti kutoka somo la vinasaba inaonyesha kwamba ikiwa wazazi wote walikuwa wanakojoa kitandani wakiwa watoto, asalimia 77 ya watoto watakaowazaa watajikojolea zaidi ya miaka mitano na ikiwa mzazi mmoja alikua na tatizo hili, asalimia 44 ya watoto watajikojolea zaidi ya miaka mitano. Kwa upande mwingine, tatizo la kukojoa linalokuja baadaye huweza kuwa limesababiswa na matatizo ya hisia au ya kisaikolojia na msongo wa mawazo(stress).

 

Mara nyingi hii hutokea pale anapozaliwa mdogo wake, ugomvi wa wazazi, msongo anaoupata mtoto anapoanza shule au kutengana wazazi. Asilimia ndogo sana ya watoto wenye tatizo hili husababishwa na magonjwa au maambukizi katika sehemu ya kibofu au uwezo wa figo.

MATIBABU NA USHAURI

Adhabu kali, kumpiga, au kumchapa mtoto mwenye tatizo hili humuongezea tatizo na kufanya tatizo lizidi au kuchelewa kuisha. Ni muhimu zana kutomuadhibu kumtisha au kumsema vibaya mtoto mwenye tatizo hili. Kufanya hivyo sio tu kama kutazidisha tatizo bali pia humfanya kuwa katika hatari ya kupata matatizo mengine ya kisaikolojia.

 

MSAADA ASIJIKOJOLEE

Yafuatayo husaidia kumfanya mtoto kuacha kukojoa. Mpunguzie unywaji wa maji na ulaji wa vyakula vya majimaji kama vile uji saa tatu kabla ya kulala, kumpongeza siku ambazo hajajikojolea au kukojoa kitandani.

 

MASAJI

Masaji pia inatibu tatizo la kukojoa kitandani na kwa matokeo mazuri zaidi tumia mafuta ya zeituni (olive oil). Yapashe moto kidogo mafuta hayo ili yawe ya uvuguvugu kwa mbali na upake ya kutosha sehemu ya chini ya tumbo la mtoto na ufanye masaji eneo hilo polepole kwa dakika kadhaa. Fanya zoezi hili kila siku mpaka umeridhika na mtokeo yake. Mtoto akiendelea kujikojolea mara kwa mara ushauri ni kwamba mpeleke hospitalini kwa uchunguzi na tiba.

Comments are closed.