The House of Favourite Newspapers

TCDC Yasisitiza Elimu, Mpango wa Uzazi kwa Wanawake

Meneja Utetezi wa Mradi wa Utetezi na Huduma za Uzazi wa Mpango wa shirika la Tanzania Communications and Development Center (TCDC), James Mlali (kulia) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juu ya hali ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango nchini.  Kushoto ni Meneja Ufuatiliaji na Tathmini wa TCDC,  Nazir Yusuph.

 

SHIRIKA lisilo la kiserikali linalojihusisha na utetezi wa afya ya mama na uelimishaji la Tanzania Communications And Development Center (TCDC) limesema bado elimu ya uzazi wa mpango inahitajika ili kufikia malengo ya wanawake kujikomboa kiuchumi.

 

Meneja Ufuatiliaji na Tathmini wa TCDC,  Nazir Yusuph,  alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Siku ya Kimataifa ya Uzazi Salama inayoadhimisha Septemba 26 kila mwaka.

 

Alisema baadhi ya wanawake ambao hawafuati njia za uzazi wa mpango, wanasababisha kushindwa kushiriki katika shughuli za kujenga uchumi wa taifa.

 

‘Uzazi usiozingatia kanuni za kitaalamu nchini, unasababisha wanawake wengi kushindwa kupewa nafasi za juu za uongozi  na wengine kushindwa kuendelea na masomo,  hivyo kuishia kujiajiri katika biashara ndogondogo,” alisema.

 

Aliongeza kwamba wanawake wengi wapo katika sekta isiyo rasmi kwa sababu mbalimbali, lakini mojawapo ni kutokana na kutokuwa na utaratibu wa kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango.

 

Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), wanawake walio na elimu ya juu ni asilimia 30 na walioshika nafasi za juu ni asilimia 15 pekee.

 

Naye, Meneja Utetezi wa Mradi wa Utetezi na Huduma za Uzazi wa Mpango, James Mlali,  alisema maadhimisho ya siku hiyo ya kimataifa yanalenga kutafakari kama taifa linashiriki kikamilifu katika matumizi ya uzazi wa mpango.

 

Alisisitiza kwamba bado elimu inahitajika zaidi kutolewa kwa jamii juu ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango ili kuondoa dhana potofu zilizojengeka katika jamii kwamba njia hizo zina madhara

Comments are closed.