The House of Favourite Newspapers

TCRA, mna cha kufanya na picha hizi

0

TCRA (1)KWENU Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), habari za kazi? Vipi mnaendeleaje na mapambano ya shughuli za kila siku?

Binafsi sijambo. Namshukuru Mungu naendelea kupambana katika eneo langu. Kuwapa habari Watanzania, kuwaelimisha na kuwaburudisha kupitia kalamu yangu.

Ndugu zangu TCRA, nimewakumbuka leo kwa barua. Nina jambo nataka kuwaeleza kwani nisipofanya hivyo nitakuwa siitendei haki kalamu yangu na nchi yangu.

Kwanza niwapongeze maana najua jukumu mlilonalo ni kubwa. Mnajitahidi kufanya kila linalowezekana kuhakikisha mnadhibiti mawasiliano ya Watanzania wasiopungua milioni 45, kupitia mawasiliano mbalimbali.

Ndugu zangu, natambua kwamba jukumu lenu ni zito. Kusimamia maadili ya Kitanzania katika vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na mitandao ya mawasiliano.

Ni kazi kubwa. Ni dhamana ambayo kwa kila Mtanzania anayejali utaifa, lazima atawaunga mkono. Nawapongeza katika hilo.

Pamoja na pongezi hizo, lakini kuna kitu cha kufanya katika suala zima la mitandao ya kijamii. Mitandao kama Facebook, Instagram na mingineyo. Kuna kila sababu ya kufanya tathmini upya ili kuona namna ambavyo mnaweza kudhibiti maadili ya Kitanzania.

Ndugu zangu, siku hizi mitandao inatumika vibaya. Inatumika kuchafua watu, inatumika kuharibu tabia za watoto wetu. Mtu ana uwezo wa kupiga picha au kusambaza picha isiyokuwa na maadili kwa watu mbalimbali pasipo kujulikana na mtu yeyote.

Hivi ni kweli tunashindwa kudhibiti kwa kutumia teknolojia tuliyonayo? Kwamba mtu akiweka kitu ambacho kinakiuka maadili ashindwe kufanya hivyo?

Na kama pia tumeshindwa kudhibiti katika teknolojia, kwani tunashindwa nini kuzuia kabisa baadhi ya mitandao ya kijamii ambayo tunaiona inachangia kwa kiasi kikubwa kusambaza picha zisizokuwa na maadili.

Mifano ipo mingi tu, kuna nchi ambazo wananchi wake hawatumii baadhi ya mitandao ya kijamii kwa sababu wameona haina faida kwao. Kama tunaona Instagram ina changia kwa kiasi kikubwa maadili kuporomoka, kwa nini tusizuie?

Licha ya kuwa mitandao hii ya kijamii ina faida zake kama tutaitumia vizuri lakini kuna kila sababu kuangalia faida na hasara. Tukiona hasara inakuwa kubwa kuliko faida, ni bora kuachana nayo.

Bahati mbaya sana kwa kushindwa kwenu kudhibiti, watu wamekuwa wakisambaza taarifa zisizokuwa na ukweli. wanatunga uongo, unapita bila kuchujwa na matokeo yake Mtanzania wa kawaida anapotoshwa.

Ndugu zangu, nyinyi mna mamlaka ya kusimamia mawasiliano. Shirikianeni na mamlaka nyingine za kiserikali na kweli matokeo tuyaone. Lazima tufike mahali mtu akiwa na akaunti kwenye mtandao fulani, akiweka kitu kibaya, atambuliwe kirahisi.

Sheria ya makosa ya mtandao haiwezi kufanya kazi bila nyinyi kusimamia mawasiliano ya mitandao husika.

Simamieni na muishauri serikali kutekeleza na kuhakikisha maadili ya Mtanzania yanabaki kuwa yaleyale yanayoheshimika.

Kukaa kwenu kimya na kushindwa kudhibiti hali hiyo kunaliharibu taifa letu hususan vijana ambao huziangalia picha hizo bila kujali athari zake.

Niwatakie mafanikio mema, mimi yangu ni hayo tu.

Mimi ni ndugu yenu;

Leave A Reply