The House of Favourite Newspapers

TFF Yamzuia Boban Kucheza Yanga

WAKATI wapenzi na mashabiki wa Yanga wakiwa na shauku kubwa ya kutaka kumuona uwanjani mchezaji wao mpya, Haruna Moshi ‘Boban’, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), linadaiwa kumzuia mchezaji huyo kuitumikia timu hiyo.

 

Boban alijiunga na Yanga hivi karibuni katika dirisha dogo la usajili akitokea African Lyon ambayo pia aliungana nayo mwanzoni mwa msimu huu akitokea Friends Rangers inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Meneja wa Boban, Herry Mzozo, alisema TFF imemzuia Boban kuitumikia Yanga kutokana na maagizo yake iliyoyatoa hivi karibuni kwa timu zote za ligi kuu kuto­watumia wachezaji wa ndani waliosajiliwa katika dirisha dogo la usajili mpaka hapo Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji itakapokutana na kupitia usajili huo.

 

Alisema kama isingekuwa hivyo, basi Boban angeanza kuitumikia Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting wa Jumapili iliyopita ambao timu hiyo iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 lakini hakuweza kuonekana uwanjani kutokana na maagizo hayo ya TFF.

 

“Hiyo ndiyo sababu kubwa hasa ambayo imemfanya Boban mpaka sasa ashindwe kuitumikia Yanga japokuwa tayari al­ishajiunga nayo kwa ajili ya mazoezi.

“Hata hivyo, ngoja tuendelee kuisubiri kamati hiyo mpaka hapo itakapokutana na kutoa maamuzi,” alisema Mzozo.

Stori: Sweetbert Lukonge

Comments are closed.