The House of Favourite Newspapers

The Angel Of Darkness -27

0

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna. Arianna anaokotwa na vikosi vya uokoaji na kurejeshwa Tanzania ambako awali anakabidhiwa kwa mdogo wa marehemu baba yake, Hans ambaye anapewa jukumu la kusimamia mirathi na kumlea mtoto huyo.

Brianna anaokotwa na mwanamke mwendawazimu, Mashango na kwenda kuanza naye maisha kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare. Japokuwa mwanamke huyo alikuwa amechanganyikiwa akili, lakini anamlea vizuri mtoto huyo na kadiri muda unavyozidi kusonga mbele, ndivyo anavyozidi kuwa mkubwa huku mwanamke huyo naye akipona maradhi ya akili yaliyokuwa yanamsumbua.

Siku zinazidi kusonga mbele na kwa bahati mbaya zaidi, Mashango, mwanamke aliyekuwa akimlea Brianna kwa mapenzi makubwa, anagongwa na gari na kupoteza maisha, jambo linalomuathiri sana Brianna. Baadaye anajitokeza msamaria mwema, Wailima Njoroge ambaye anaamua kumchukua mtoto huyo na kuishi naye pamoja na familia yake.

Upande wa Arianna, maisha yanaanza kumuendea kombo ambapo Hans anatumia vibaya mali alizoachiwa Arianna na baadaye anatorokea kusikojulikana na familia yake. Arianna anaendelea kukua lakini kwa sababu ya kukosa uangalizi wa karibu, anajikuta akiingia kwenye vitendo viovu, ikiwemo matumizi ya madawa ya kulevya.

Baada ya Arianna kuuza nyumba anakwenda Arusha akiwa na teja mwenzake, Diego. Wanapofika huko, kwa bahati mbaya wanakamatwa na polisi hivyo kujikuta wakimaliza fedha zote mahakamani kwenye kutoa hongo. Baadaye, wakiwa kwenye maisha ya msoto, Arianna anakutana na mzee tajiri ambaye anatokea kumpenda. Kwa ushauri wa Diego, wanakubaliana kumfanya mzee huyo kuwa kitega uchumi chao.

Je, nini kitafuatia?

SONGA NAYO…

Arianna na Diego walikuwa na hali mbaya ya kiuchumi, walikosa fedha za kununulia madaya ya kulevya hivyo kitendo cha Arianna kupendwa na mzee huyo kiliwapa uhakika kwamba kila kitu kingekwenda sawa.

“Sawa. Nimekuelewa, nipo tayari kuwa nawe kwa sababu hata mimi nakupenda,” alisema Arianna.

“Na kama nitataka ukaishi nami nyumbani kwangu?”

“Nyumbani kwako?”

“Ndiyo!”

“Na mkeo je?”

“Sina mke, alifariki dunia kwa ajali ya gari nchini Marekani miaka mingi iliyopita,” alisema mzee huyo, Arianna hakuwa na tatizo, akakubaliana na mzee huyo kwenda kuishi naye ila kwa sharti moja, kwamba naye Diego alitakiwa kuishi naye awe mfanyakazi wa ndani, kwa hilo, wala halikuwa tatizo, mzee Msuya akakubaliana naye pasipo kujua kama watu hao walikuwa na mipango yao vichwani.

“Kwa hiyo mtakuwa tayari lini?”

“Nitakutaarifu lakini nafikiri ndani ya wiki hiihii,” alisema Arianna huku aking’ata kucha, aibu za kikekike zikiwa zimetawala kwenye uso wake. Baada ya kumaliza mazungumzo hayo nyeti, Arianna alimuita Diego ambaye alikuwa amekaa pembeni kabisa, akiendelea kunywa juisi taratibu.

Isingekuwa rahisi kuhisi kwamba Diego na Arianna walikuwa na uhusiano wa kimapenzi wala isingekuwa rahisi kwa mtu yeyote asiyewafahamu kuhisi kwamba wawili hao walikuwa wametopea kwenye matumizi ya madawa ya kulevya kwa jinsi walivyojitahidi kutengeneza mwonekano wao kwa siku hiyo.

Diego alienda kujumuika na Arianna na tajiri Engbelt Msuya, wakaendelea kupata vinywaji na vyakula mpaka kila mmoja aliporidhika.

“Nataka leoleo niwapeleke nyumbani kwangu mkapafahamu,” alisema Msuya, Arianna na Diego wakatazamana usoni kwa sekunde kadhaa kisha Arianna akamgeukia Msuya na kumwambia kwamba wapo tayari, akaachia tabasamu pana na kumuita mhudumu aliyekuwa akiwahudumia kwa vyakula na vinywaji. Akamlipa fedha zake kisha wote wakainuka na kuelekea kwenye gari la mfanyabiashara huyo wa madini ya Tanzanite.

Wakaingia na muda mfupi baadaye, safari ya kuelekea Njiro, nyumbani kwa mfanyabiashara huyo ikaanza, huku Arianna akiwa amekaa kwenye siti ya mbele, pembeni ya dereva na Diego akiwa amekaa kwenye siti ya nyuma ya gari hilo la kifahari.

Safari iliendelea na dakika kadhaa baadaye, gari hilo lilisimama mbele ya geti kubwa la kisasa, ambalo liliunganishwa na uzio uliokuwa na nyaya zilizokuwa zinapitisha umeme.

Baada ya kupiga honi mara moja tu, mlango ulifunguliwa na askari wawili waliokuwa wamevalia sare maalum, kila mmoja akiwa na bunduki begani, gari likaingizwa ndani na kupelekwa mpaka kwenye maegesho maalum ndani ya jumba hilo la kifahari, Msuya akawa wa kwanza kuteremka na kumfungulia Arianna mlango kisha akamfungulia na Diego.

Wawili hao walishindwa kuficha mshtuko walioupata baada ya kufika kwenye hekalu hilo la mfanyabiashara huyo mkubwa. Usingeweza kudhani kwamba Msuya ndiye aliyekuwa anaishi kwenye jumba hilo ambalo lilikuwa likifanana na ikulu au hekalu la mfalme.

Diego na Arianna waliendelea kushangaa huku na kule, wakiwa ni kama hawaamini macho yao. Wafanyakazi wawili wa kike, waliokuwa wamevalia sare nadhifu, walikuja kumpokea Msuya na kumsalimu kwa adabu, wakawakaribisha wageni na kuwaongoza mpaka kwenye sebule kubwa iliyokuwa imesheheni vitu vingi vya thamani.

“Karibuni sana, hapa ndiyo kwangu, jisikieni kuwa nyumbani,” alisema Msuya na kuwapa maagizo wafanyakazi wake kuwahudumia wageni wake vinywaji, yeye akapanda ngazi na kuelekea chumbani kwake, ghorofani.

“Duuh! Hapa tumelamba dume mwanangu, ukishikwa shikamana,” Diego alisema kwa sauti ya chini huku akigeuka huku na kule akiendelea kushangaa jumba hilo la kifahari. Arianna aliachia tabasamu pana, akamkonyeza Diego kwamba anatakiwa kutulia.

Muda mfupi baadaye, Msuya alishuka ghorofani akiwa ameshabadilisha nguo alizokuwa amevaa awali, safari hii akawa amevaa pajama na fulana, akaungana na wawili hao ambao licha ya kwamba muda mfupi uliopita walitoka kula na kunywa mpaka wakasaza, kila mmoja alikuwa na glasi ya juisi mkononi wakiendelea kufaidi.

Waliendelea kupiga stori za hapa na pale mpaka kigiza cha jioni kilipoanza kuingia ambapo Msuya aliwapa dereva wa kuwarudisha nyumbani kwao. Kabla hawajaondoka, aliwakabidhi kila mmoja bahasha yake, ya Arianna ikionesha kutuna kuliko ya Diego.

Wakamshukuru sana na kuondoka na dereva aliyewapeleka mpaka jirani na mahali walipokuwa wanaishi. Akawashusha na kugeuza gari kurudi Njiro, Arianna na Diego wakapitia mtaa wa pili kununua kete nyingi za madawa ya kulevya kisha wakaenda kujifungia ndani ya chumba chao, kila mmoja akionesha kuwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake.

Siku hiyo kazi ilikuwa moja tu, kujidunga madawa ya kulevya na kufanya ngono mpaka usiku wa manane, wakalala kila mmoja akiwa hoi. Kesho yake walichelewa sana kuamka, mpaka saa tano za asubuhi, bado walikuwa kitandani. Mlio wa simu ya Diego ndiyo uliowazindua kutoka usingizini.

“Anapiga! Arianna, tajiri Msuya anapiga simu,” Diego alisema huku akimtingisha Arianna ambaye bado alikuwa usingizini, harakaharaka akaamka baada ya kusikia kwamba Msuya ndiyo alikuwa anapiga.

“Haloo!”

“Haloo baby! Bado umelala?”

“Najisikia homa mpenzi.”

“Ooh! Pole sana mke wangu mtarajiwa, nini zaidi.”

“Ni malaria lakini nimeshaenda kupata matibabu.”

“Pole sana, vipi umeshaenda kununua simu kama tulivyokubaliana?”

“Hapana, nimeshindwa kwenda kwa sababu ya afya yangu lakini usijali nitamtuma Diego.”

“Kama bado hujaenda basi usiende, nimeshakutafutia simu nzuri, nitakuletea jioni wakati natoka kazini,” alisema Msuya, kauli iliyomfurahisha sana Arianna, wakaendelea kuzungumza mambo kadhaa kisha akakata simu. Baada ya kumaliza kuzungumza na Msuya, Arianna alimgeukia Diego na kumueleza kwamba tayari ameshanunuliwa simu, wakafurahi na kugongesheana mikono.

“Sasa hiyo jioni akija na kukukuta huumwi utamwambia nini?”

“Nitajifanyisha kwamba naumwa, mambo yote niachie mimi,” alisema Arianna, wakagongesheana tena mikono kwa furaha.

“Ila tuache masihara Arianna, unajua mwenzio najisikia wivu sana.”

“Wivu wa nini?”

“Naona kama mwisho wa siku unaweza kuacha kunipenda mimi ukakolea kwa Msuya maana anakujali sana na ananizidi kwa kila kitu,” alisema Diego huku akionesha kumaanisha kile alichokisema, Arianna akacheka sana na kumtoa wasiwasi kwamba hata iweje kamwe hawezi kuachana naye.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

Leave A Reply