The House of Favourite Newspapers

The angel of darkness -47

1

Watoto wawili mapacha, Arianna na Brianna wanazaliwa katika familia ya Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa. Kwa bahati mbaya wakati wakiwa bado wadogo, familia yao inakuwa miongoni mwa watu wanaokumbwa na shambulio baya la kigaidi linalotokea kwenye kituo kikubwa cha biashara nchini Kenya, Kikuyu Mall.

Wazazi wao wote wawili wanapoteza maisha katika tukio hilo na huo unakuwa mwanzo wa mapacha hao kutengana. Arianna anarudishwa jijini Dar es Salaam wakati Brianna anakulia kwenye mtaa wa watu maskini wa Mathare jijini Nairobi.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kumuoa lakini Arianna anakula njama na Diego na tayari wamefanikiwa kumuibia mfanyabiashara huyo mamilioni ya fedha na kutengeneza mazingira ionekane kama wamevamiwa na majambazi.

Arianna ametorokea nchini Kenya, ambako anamsubiri Diego ili watoroke pamoja kama walivyokubaliana lakini ghafla anajikuta akiangukia mikononi mwa polisi wa Kenya.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Ndege kubwa iliyokuwa na maandishi ubavuni yaliyosomeka American Airways, ilikuwa ikipasua mawingu kwa kasi kubwa kuelekea jijini Nairobi, Kenya ikitokea katika Uwanja wa Ndege wa JFK jijini New York, Marekani.

Miongoni mwa abiria wengi waliokuwa ndani ya ndege hiyo, alikuwepo pia Msuya ambaye licha ya ukweli kwamba ndege ilikuwa ikisafiri kwa kasi kubwa, alikuwa anaona kama haiendi kabisa. Alitamani kufumba na kufumbua ajikute tayari ameshawasili jijini Dar es Salaam, jambo ambalo halikuwezekana.
Mawazo mengi yaliendelea kupita ndani ya kichwa chake, kila alipokuwa akimfikiria mkewe na kuvuta taswira jinsi watekaji walivyokuwa wakimtesa na ujauzito wake, machozi ya uchungu yalikuwa yakimtoka.

“Lazima niwashikishe adabu wote waliohusika,” alisema Msuya na kujipigapiga kifuani, jambo lililofanya abiria wenzake waliokuwa wamekaa siti moja wabaki wakimshangaa. Safari iliendelea na baada ya saa nyingi angani, hatimaye sauti laini ya mhudumu wa ndege ilisikika ikiwataarifu abiria wote kufunga mikanda wakati ndege ikijiandaa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jommo Kenyatta jijini Nairobi, Kenya.

Msuya na abiria wenzake walitii maagizo hayo na kufunga mikanda, ndege ikaanza kuinama upande wa mbele kuonesha kwamba ilikuwa ikijiandaa kutua, ikawa inazidi kushuka na muda mfupi baadaye, magurudumu yake ya nyuma yaligusa ardhi na kufuatiwa na ya mbele, ikakimbia kwa kasi uwanjani hapo na dakika kadhaa baadaye, ilikuwa imesimama jirani na jengo kubwa la uwanja huo wa ndege.

Japokuwa Msuya hakuwa amekaa jirani na mlango, ngazi ziliposogezwa na mlango kufunguliwa tu, alikuwa wa kwanza kuteremka, harakaharaka akashuka kwenye ngazi mpaka chini. Akili yake ilikuwa ikienda mbio mno, alitamani muda huohuo apate ndege ya kuunganisha mpaka jijini Arusha.

Baada ya kukamilisha taratibu za uwanjani hapo, Msuya alienda kwenye jengo maalum la kusubiria abiria kwa sababu ndege ya kuelekea jijini Arusha ilikuwa iondoke saa moja baadaye. Muda wote alikuwa akizunguka huku na kule uwanjani hapo, alitamani kama uwepo usafiri mwingine wa haraka zaidi unaoweza kumfikisha jijini Arusha.

Muda ulizidi kuyoyoma na hatimaye ule wakati ambao Msuya alikuwa akiusubiri kwa hamu uliwadia, sauti ya mhudumu wa uwanjani hapo ilisikika ikiwataarifu abiria waliokuwa wakitarajia kusafiri na ndege ya Kenya Airways kuanza kujiandaa kwa ajili ya kuelekea kwenye ndege, tayari kwa safari ya kuelekea jijini Arusha.

Harakaharaka Msuya akachukua mkoba wake mdogo na kuelekea tena sehemu ya ukaguzi, dakika chache baadaye tayari alikuwa ndani ya ndege. Abiria wengine wakaendelea kupanda na hatimaye safari ya kuelekea jijini Arusha ilianza.

Ndege ilipowasili Arusha tu, Msuya aliteremka na abiria wengine na bila kupoteza muda aliongoza moja kwa moja mpaka kituo kikuu cha polisi kwa ajili ya kupata maelezo ya kilichotokea.

Kwa kuwa alikuwa akifahamika sana, alipofika tu kituoni hapo, alipelekwa moja kwa moja kwenye ofisi ya mkuu wa kituo ambaye naye alimuita mkuu wa upelelezi na kuanza kuzungumza na Msuya juu ya kilichotokea.
***
A
rianna aliendelea kushikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Lianai, Jimbo la Taveta nchini Kenya, akihusishwa na tuhuma mbaya za ugaidi baada ya kukamatwa akiwa na bastola, kinyume na sheria lakini pia akiwa hana nyaraka zozote zinazoonesha kwamba ameingia nchini humo kihalali.

Wimbi la matukio ya ujambazi na ugaidi uliokuwa unafanywa na raia wa Somalia nchini humo, wakishinikiza Serikali ya Kenya iyaondoe majeshi yake katika ardhi yao, iliwafanya polisi wawe makini mno na kazi yao. Kila aliyetiliwa shaka ilikuwa ni lazima akamatwe na kuwekwa nyuma ya nondo wakati uchunguzi ukiendelea.

Ni katika mkumbo huo, Arianna naye alipojikuta akinaswa kiulaini na kuwekwa nyuma ya nondo katika kituo hicho, akichanganywa na rais wengine wengi wa Somalia ambao nao walikuwa wakihusishwa na ugaidi.

Kwa kuwa muda ulikuwa umeenda, baada ya kukamatwa, Arianna aliingizwa lupango kwa ajili ya kusubiri suala lake kufuatiliwa kwa kina siku iliyokuwa inafuatia, akalala selo moja na wanawake wengine wengi wa Kisomali huku wanaume wao wakishikiliwa kwenye selo nyingine ndani ya jengo hilohilo.
***
Saa nane za usiku, milio ya risasi na mabomu ya kutupwa kwa mkono ilizizima kwenye Mji wa Lianai na kusababisha hofu kubwa miongoni mwa raia wa kawaida. Hofu hiyo haikuishia kwa raia tu, hata askari waliokuwa doria nao walipatwa na kiwewe kutokana na uzito wa silaha zilizokuwa zinatumika.

Kundi kubwa la watu waliokuwa wamevalia mavazi kama Wasomali, wakiwa wameziba nyuso zao na kuongea lugha inayofanana na Kiarabu, walisambaa kwenye mji huo kila mmoja akiwa na bunduki nzito mkononi. Kila walipokuwa wanapita walikuwa wakisababisha uharibifu mkubwa, ikiwemo kuchoma moto nyumba za serikali.

Purukushani hizo ziliishia kwenye Kituo cha Polisi cha Lianai ambapo watu hao, wakiwa wamejihami kwa silaha nzitonzito, walivamia kituo hicho na kuanza kurushiana risasi na askari ambao baadaye walizidiwa nguvu.

Baada ya kuwazidi nguvu polisi na kuwaweka chini ya ulinzi huku wengine wengi wakipigwa risasi, walianza kazi ya kuwachambua watu waliokuwa selo.
“Jina lako?”
“Khaleel al Jabir!”

“Kaa huku.”
“Jina lako nani?”
“Geofrey Otieno.”
“Rudi kule ndani.”

“Na wewe jina lako nani?”
“Fakhir Khan.”
“Kaa huku,” mwanaume mmoja aliyekuwa akizungumza Kiswahili chenye lafudhi ya Kisomali, mkononi akiwa ameshika bunduki nzito, alikuwa na kazi ya kuwachambua mahabusu waliokuwa nyuma ya nondo. Kazi ya kuwachambua iliendelea kwa muda mrefu huku wakitumia vigezo walivyokuwa wanavijua wenyewe.

Baada ya kumaliza upande wa wanaume, wale ambao hawakuwa na vigezo walifungiwa tena mlango wa selo kwa nje na kuhamia upande wa wanawake ambako nako waliendelea kumhoji mmoja baada ya mwingine, wengine wakatolewa na wengine wakaachwa ndani ya selo na kufungiwa mlango kwa nje.

Baada ya kumaliza kazi hiyo ya kuwachambua, wengine walianza kazi ya kumwagia mafuta ya petroli kuzunguka kituo chote kisha wakapanda kwenye magari ambayo yalikuwa tayari yameandaliwa nje ya kituo hicho, wakaondoka kwa kasi kubwa. Walipofika umbali wa mita kadhaa, walikilipua kituo hicho na kusababisha moto mkubwa ulioambatana na moshi mzito
mweusi angani.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

 

1 Comment
  1. Prince'kabagala says

    ubaya ulioufanya ni mkubwa ariana. ona yanayokupata sasa.

Leave A Reply