The House of Favourite Newspapers

The Angel Of Darkness  – 58

0

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake. Mfanyabiashara huyo anamuoa Arianna na kumchukua na Diego pia kwenda kuishi naye kwenye jumba lake la kifahari bila kujua kwamba wawili hao walikuwa wapenzi.

Siku chache baada ya ndoa, Arianna anagundua kwamba amenasa ujauzito wa Diego, baadaye wanapanga njama za kutoroka. Arianna anakuwa wa kwanza kuvuka mpaka na kuelekea Kenya lakini akiwa huko, anakutana na janga jingine na kunasa ndani ya kituo cha polisi kinachoungua baada ya kuvamiwa na magaidi wa Kisomali.

Anaponea kwenye tundu la sindano na kufanikiwa kutorokea kwenye Mji wa Bisil, anakopanda basi la kuelekea jijini Nairobi lakini kilometa chache mbele wanasimamishwa na polisi.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Jina lako nani?” askari mmoja mwenye mwili mkubwa, mweusi kama mkaa, alimuuliza Arianna kwa sauti iliyoonesha kutokuwa na hata chembe ya masihara.

“Lupita Wainaina.”

“Watokea wapi?”

“Natoka kwa township ya Bisil,” Arianna alimdanganya askari huyo huku akijitahidi kuiga lafudhi ya Kikenya ili isiwe rahisi kushtukiwa kwamba ni Mtanzania kwani kama ingetokea hivyo, angeulizwa hati yake ya kusafiria na huo ndiyo ungekuwa mwanzo wa kutambulika na kukamatwa.

“Jina lako lafanana na Lupita Nyong’o anayeitangaza Kenya kwa kimataifa, ni jina zurii kama wewe!” alisema askari huyo huku akiachia tabasamu pana. Kwa Arianna huo ulikuwa ushindi mkubwa kwani alijua askari huyo hawezi tena kuendelea kumhoji kwa sababu tayari alishaingiza suala la masihara.

Alichokifikiria ndicho kilichotokea, askari huyo aliachana na Arianna na kuendelea kuwahoji abiria wengine. Baada ya kazi hiyo iliyochukua karibu dakika ishirini, abiria waliruhusiwa kuingia ndani ya basi. Ni mpaka Arianna alipokaa kwenye siti yake na basi kuruhusiwa kuondoka ndipo akili yake ilipotulia.

Akashusha pumzi ndefu na kuinua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu wake kwani hakuamini kama atatoka salama kwenye kizuizi hicho. Basi la kisasa la Taveta Safari liliendelea kuchanja mbuga kwa kasi kubwa kuelekea jijini Nairobi.

Abiria wote walikuwa kimya ndani ya gari, wengi wakiwa wamesinzia kwenye siti zao kutokana na uchovu wa safari hiyo ndefu. Arianna alikuwa ametulia kwenye siti yake, huku mawazo yake yakionekana kwenda mbali sana. Kila alipokuwa akifikiria hatima ya maisha yake, alikuwa haelewi nini kitakachofuata.

Janga lililomkumba kwenye Mji wa Lianai lilimfanya akose kabisa amani ndani ya moyo wake, alijua chochote kinaweza kumtokea wakati wowote, akaona njia nyepesi ya kuwa salama ni kuepusha mbawa zake. Hakutaka tena kuendelea kumsubiria Diego, alichoamua ni kusonga mbele na kama ni kumtafuta, atafanya hivyo akishakuwa na uhakika wa usalama wake.

Basi lilizidi kuchanja mbuga na hatimaye liliwasili jijini Nairobi baada ya safari ndefu iliyochukua saa kadhaa. Japokuwa muda ulikuwa umeenda sana, Arianna hakutaka kulaza damu.

Alijua kwa vyovyote lazima upelelezi wa chini kwa chini ulikuwa ukiendelea jijini Nairobi, hasa kwenye mahoteli makubwa, jambo ambalo alihisi linaweza kumuingiza matatani endapo ataamua kutafuta hoteli yenye hadhi ya juu.

Alichofanya baada ya kuteremka kwenye basi baada ya kufika kwenye Stendi Kuu ya Mabasi jijini Nairobi, ilikuwa ni kupanda daladala ambazo zinafahamika zaidi kwa jina la matatu nchini humo na kumueleza kondakta kwamba anaelekea Kariobangi na kumuomba msaada wa kumshusha wakifika kwa sababu hakuwa akipajua.

Alichagua kwenda Kariobangi kwani aliwahi kusikia kwamba mtaa huo una mchanganyiko wa watu maskini na matajiri kiasi kwamba, si rahisi kwa mamlaka za usalama kufika kwa urahisi, hasa Kariobangi Kaskazini iliyokuwa inakaliwa na watu maskini.

Baada ya kukatiza mitaa ya Nairobi huku akishangaa huku na kule kwa sababu ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kufika kwenye jiji hilo, akili zake zote zikiwa ni kwenye begi alilobeba lililokuwa na fedha nyingi na madini ya Tanzanite, hatimaye aliwasili Kariobangi.

Akateremka kwenye matatu na kukodi Bajaj huku akimuelekeza dereva kumpeleka kwenye nyumba yoyote ya kulala wageni ya bei nafuu. Japokuwa alikuwa amebeba utajiri mkubwa, hakutaka mtu yeyote amshtukie. Dakika chache baadaye, alikuwa tayari ameshawasili kwenye nyumba ya kulala wageni iitwayo Kimathi Lodge iliyokuwa mita kadhaa kutoka kwenye kituo cha matatu.

Akamlipa dereva huyo wa Bajaj na kuingia ndani ya nyumba hiyo ya kulala wageni, akalipia chumba kwa usiku mmoja na kuingia kwenye chumba alichoelekezwa, angalau akawa na uhakika kwamba hakuna mtu anayeweza kugundua kwamba yupo mahali hapo kwa wakati huo.

Alipanga alfajiri na mapema awahi kuamka na kurudi kwenye stendi kuu ya mabasi kwa ajili ya safari ndefu ya kuelekea Mandera, mji uliokuwa kwenye mpaka wa Kenya na Somalia. Malengo yake yalikuwa ni kwenda kuweka makazi yake kwenye mji huo akiamini haiwezi kuwa rahisi kwa mtu yeyote kutoka Tanzania kufika huko. Aliamini pia kwamba haitakuwa rahisi kwa polisi wa Kenya kumkamata.

***

Taarifa kwamba Arianna alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakishikiliwa kwenye Kituo cha Polisi cha Lianai usiku kilipovamiwa na magaidi kutoka Somalia, zilimchanganya mno Msuya. Kwa jinsi alivyokuwa anampenda mkewe, hakutaka kupoteza muda.

Harakaharaka aliwasiliana na rafiki yake mkubwa, Mtei Jackton aliyekuwa akimiliki kampuni ya kusafirisha watalii ya Maasai Empire na kumuomba amkodishie helikopta yake kwa ajili ya kuwahi eneo la tukio. Kutokana na uhusiano mzuri uliokuwepo kati yao, alikubali na muda mfupi baadaye, tayari helikopta ilikuwa imeshaandaliwa tayari kwa safari.

Safari ya kuelekea Lianai, Kenya ikaanza huku pia askari kutoka Tanzania wakivuka mpaka kuelekea eneo la tukio kwani ukiachilia mbali Arianna, walikuwepo pia Watanzania wengine kadhaa ndani ya kituo hicho wakati kikishambuliwa na magaidi.

Baada ya kusafiri kwa muda angani, hatimaye helikopta iliyokuwa imembeba Msuya iliwasili Lianai, ikatua kwenye uwanja wa shule ya msingi uliokuwa jirani ambapo Diego alienda kumpokea Msuya na kumueleza hali halisi ilivyokuwa. Wakaongozana pamoja mpaka eneo la tukio ambapo askari wengi wa Kenya walikuwa wakiendelea na kazi.

Kwa kuwa tayari jeshi la polisi nchini Tanzania lilishawasiliana na wenzao wa Kenya, Msuya alipowasili tu eneo hilo, alipelekwa sehemu maalum na kuanza kuhojiwa, huku naye pia akitaka kupewa maelekezo ya nini hasa kilichotokea.

Baadaye polisi wa Tanzania nao waliwasili eneo la tukio ambapo taratibu zote za kijeshi zilifanywa na wakaanza kushirikiana na wenzao wa Kenya kufuatilia kwa makini kilichotokea. Baada ya kuelezwa kilichotokea, Msuya alishindwa kujizuia, akawa analia kama mtoto mdogo kwani aliamini huo ndiyo mwisho wa mkewe.

Mabaki ya miili yote ya watu walionasa kwenye kituo hicho na kuteketea kwa moto, ilitolewa na kupelekwa hospitalini ambapo kazi ya kupima vinasaba (DNA) ili kuwatambua ilianza. Muda wote Msuya alikuwa akilia huku Diego akitumia muda mwingi kumbembeleza.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply