The House of Favourite Newspapers

The Angels of darkness (Malaika wa Giza)-56

0

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake. Mfanyabiashara huyo anamuoa Arianna na kumchukua na Diego pia kwenda kuishi naye kwenye jumba lake la kifahari bila kujua kwamba wawili hao walikuwa wapenzi.

Siku chache baada ya ndoa, Arianna anagundua kwamba amenasa ujauzito wa Diego, baadaye wanapanga njama za kutoroka. Arianna anakuwa wa kwanza kuvuka mpaka na kuelekea Kenya lakini akiwa huko, anakutana na janga jingine na kunasa ndani ya kituo cha polisi kinachoungua baada ya kuvamiwa na magaidi wa Kisomali. Anaponea kwenye tundu la sindano.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Baada ya kusumbuana sana na mlinzi, ilibidi Arianna atumie akili za ziada. Kama wahenga walivyosema penye uzia penyeza rupia, Arianna alimuahidi mlinzi huyo kumpa fedha endapo atamruhusu kuingia ili akachukue vitu vyake, baada ya kusitasita sana hatimaye alimfungulia mlango, akaenda moja kwa moja mpaka kwenye chumba chake.

Kwa bahati nzuri, wakati anapita mapokezi, mhudumu aliyekuwa hapo alikuwa amepitiwa na usingizi kwani vinginevyo angemzuia kama ilivyokuwa kwa mlinzi kwa sababu alikuwa amebadilika sana kimwonekano na kuwa wa ajabu.

Nguo zake zilikuwa zimeungua sehemu mbalimbali, ngozi yake ilikuwa imebadilika rangi kwa sababu ya moshi huku nywele zake nazo zikiwa zimeungua katika harakati za kuvunja mlango.

Alipoingia chumbani kwake, jambo la kwanza alipitiliza mpaka bafuni, akavua nguo zake ambazo sasa zilikuwa hazitamaniki na kufungulia ‘bomba la mvua’, maji yakawa yanamwagika kwa wingi. Alitumia muda mrefu kuusafisha mwili wake ambao sehemu nyingine ulikuwa umetoka malengelenge kwa sababu ya moto.

Aliporidhika, alitoka na kwenda mahali alipokuwa amehifadhi begi lake, kwa bahati nzuri kila kitu chake kilikuwa kama alivyokiacha, akainua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu wake. Harakaharaka akavaa nguo nyingine zilizokuwa kwenye begi lake na kuchukua vitu vyake vyote.

Hakuwa na muda wa kupoteza tena kwa sababu alijua tukio lililofanywa na magaidi waliovamia kituo cha polisi, lazima litasababisha serikali yote ya Kenya kuelekeza nguvu zake kwenye mji huo kuhakikisha wahusika wote wanasakwa na kukamatwa, jambo ambalo lingeweza kumuingiza kwenye matatizo kwa mara nyingine.

B

aada ya kumaliza kujiandaa, alitoka mpaka getini ambapo mlinzi alimfungulia tena mlango, safari hii akawa anamshangaa kwani alikuwa amebadilika na kuonesha kweli alikuwa na hadhi ya kukaa kwenye hoteli ile.

“Vile umebadilika sijakujua, kumbe uko manzi bomba joo!” alisema mlinzi huyo kwa Kiswahili chenye lafudhi ya Kikenya na kumfanya Arianna atabasamu kwani alikuwa anapenda kusifiwa, akaingiza mkono kwenye pochi yake na kutoa noti ya dola kumi na kumkabidhi, mlinzi huyo akaangua kicheko cha furaha na kumsindikiza Arianna kuondoka eneo hilo.

Ilibidi Arianna amuulize namna ya kupata usafiri wa kumuondoa kwenye mji huo usiku huohuo, mlinzi huyo akamwambia kwamba ana rafiki yake ambaye huwa anafanya kazi ya kuendesha bodaboda lakini hana uhakika kwamba kwa muda huo atakuwa hajalala.

“Ngoja nijaribu kumtafuta kwa rununu yake,” alisema akimaanisha ampigie simu, akatoa simu yake chakavu na kubonyeza namba fulani, muda mfupi baadaye, simu ilipokelewa. Akazungumza na rafiki yake huyo ambaye muda mfupi baadaye, alifika akiwa na bodaboda yake.

Arianna alipomueleza kwamba anataka kuondoka usiku huohuo, dereva huyo wa bodaboda alimgomea katakata huku akimwambia kwamba mji ulikuwa umechafuka usiku huo kutokana na magaidi kuvamia kituo cha polisi na kusababisha maafa makubwa.

Kwani nyie hamna taarifa? Wakora wamevamia ‘police station’ na kufanya maasi makubwa, huku kwa nje hakupitiki usiku huu, waweza kutupiga risasi, isitoshe nasikia wanajeshi wanakuja kwa wingi usiku huuhuu, tusubiri kupambazuke, nitakupeleka mpaka kwa ‘township’ ya Bisil lakini ako na ‘distance’ ndefu sana kutoka hapa,” alisema dereva huyo wa bodaboda, kauli ambayo ilimmaliza nguvu Arianna.

***

Vijana wengi wa jijini Arusha waliingia kazini kufuatia dili la nguvu lililotangazwa na Msuya la kumtafuta mkewe ambaye mpaka muda huo kila mtu alikuwa anaamini kwamba ametekwa. Picha za Arianna zilibandikwa kila sehemu, kuanzia kwenye nguzo za umeme, kwenye kuta za nyumba za watu, pembezoni mwa barabara, kwenye vituo vya daladala na kila sehemu watu wanapopita.

Msichana huyo akawa gumzo huku kila mmoja akimuonea huruma Msuya kwani kwa dau alilotangaza, ilionesha wazi ni kwa kiasi gani alikuwa anampenda mkewe na alikuwa tayari kufanya chochote kwa ajili yake.

Wapo waliohusisha tukio hilo la mkewe kutekwa na biashara zake, wakihisi huenda kuna watu alidhulumiana nao madini na ndiyo walioamua kulipiza kisasi kwa kumteka mkewe. Kila mtu alizungumza lake lakini ukweli ulibakia kwamba Arianna alikuwa ametoweka.

Kwa upande wa Diego, alitumia mwanya wa bosi wake kuchanganyikiwa! Akajifanya naye yupo bize kuhaha huku na kule kumtafuta, wakati mwingine akiongozana naye mpaka kwenye vituo vya redio na runinga vya jijini humo kulipia gharama za matangazo ya kupotea kwa Arianna.

Kwa jinsi alivyokuwa akishirikiana naye bega kwa bega, haikuwa rahisi kwa Msuya kuhisi kwamba Diego alikuwa anajua kila kitu kinachoendelea.

“Mi nafikiri ili kurahisisha kazi, tugawane kila mmoja aelekee upande wake kuliko kuongozana. Lazima Arianna apatikane,” alisema Diego, wazo ambalo Msuya alilikubali lakini wakakubaliana kuwa karibu kwa kupigiana simu ili kujuzana kinachoendelea.

Diego akautumia mwanya huo kufunga safari mpaka Namanga, malengo yake yakiwa ni kuvuka mpaka na kuelekea moja kwa moja sehemu waliyokubaliana amkute Arianna ili waondoke pamoja na kwenda kuanza maisha mapya, mbali kabisa na Msuya.

Cha ajabu, kila alipokuwa akipiga namba mpya ya Arianna waliyopeana kwa ajili ya kuwasiliana wao wawili tu, haikuwa ikipatikana hewani, jambo lililoanza kukichanganya kichwa chake. Akahisi labda amebadilisha namba na kuendelea kutumia ile aliyokuwa akiitumia siku zote lakini kila alipoipiga, nayo haikuwa ikipatikana hewani.

Hata hivyo, alijipa moyo kwamba huenda simu yake ilikuwa imeisha chaji, akavuka mpaka na kuingia upande wa Kenya ambako alitafuta usafiri wa kuelekea Lianai, Taveta, mahali walipokubaliana kwamba Arianna atamsubiri.

Diego aliendelea na safari kwa muda mrefu na hatimaye aliwasili Lianai lakini tayari muda ulikuwa umeenda sana na tayari ilikuwa ni usiku. Kwa kuwa Diego hakuwa mwenyeji kwenye mji huo mdogo, ilibidi atafute gesti na kupumzika kusubiri siku ya pili ili aanze kazi ya kumtafuta Arianna, hoteli moja baada ya nyingine kwani bado simu yake haikuwa ikipatikana hewani.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave A Reply