The House of Favourite Newspapers

The Angle of The Darkness (Malaika wa Giza)-67

0

Watoto wawili mapacha, Arianna na Brianna wanatenganishwa wakiwa bado wadogo kufuatia tukio baya la kigaidi linalotokea wakiwa mapumzikoni na wazazi wao nchini Kenya, kwenye kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi.
Katika tukio hilo, baba wa watoto hao, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa wanapigwa risasi na magaidi hao na kupoteza maisha, wakiwaacha watoto wao wakiwa bado wachanga.
Kila mmoja anapitia maisha tofauti kabisa, Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anaokotwa na mwanamke mwendawazimu, Mashango ambaye anaishi naye kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.
Arianna anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kuamua kumuoa. Baadaye, Arianna ananasa ujauzito wa Diego na wanapanga njama za kutoroka.

Msichana huyo anafanikiwa kutorokea nchini Kenya, jambo linalomfanya Msuya atangaze dau nono.
Hatimaye, pacha wa Arianna, Brianna aliyekulia kwenye mitaa ya watu maskini Mathare, Nairobi nchini  Kenya anapatikana na kuchukua nafasi ya Arianna  lakini anaonesha tofauti kubwa ya kitabia, jambo linalomshangaza kila mtu. Kutokana na mambo anayofanyiwa, taratibu Brianna anaanza kumzoea Msuya.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Mke wangu!” aliita Msuya kwa sauti ya chini, mikono yake ikiwa inafanya utalii kwenye maeneo mbalimbali ya mwili wake, hali iliyomsisimua sana Brianna kwani hiyo ndiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kukumbatiwa na mwanaume akiwa kwenye hali hiyo.
“Abee,” aliitikia Brianna kwa sauti ya kukatakata iliyokuwa inatokea kwenye pua, pumzi zikiwa zinamtoka kwa fujo kama mtu aliyetoka kukimbia mbio za mita mia moja.
“Nakupenda sana mke wangu, yaani kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo ninavyozidi kukupenda, hata sijui umenipa nini,” alisema Msuya kwa sauti nzito huku pumzi zake zikisikika vyema, Brianna akazidi kusisimka mwili wake.

Katika hali ambayo hata Brianna mwenyewe hakuelewa imekuwaje, alijikuta akianza kumpa ushirikiano Msuya, alipomgusa hapa na yeye alimgusa pale, japokuwa hakuwa akijua chochote katika ulimwengu huo, alijitahidi kuuficha ushamba wake, joto la kila mmoja likazidi kupanda.
“Mume wangu!” Brianna aliita kwa sauti ya chini, mdomo wake ukiwa sentimeta chache kutoka kwenye sikio la Msuya ambaye alionesha kuzidiwa kabisa na hisia za mapenzi.”
“Naam mke wangu!”
“Mwenzio bado sijapona tumbo, usione kama nakufanyia makusudi,” alisema Brianna, kauli ambayo ilikuwa ndiyo silaha yake ya mwisho kwani kwa hali ilivyokuwa, kusingekuwa na sababu nyingine yeyote ambayo ingemzuia Msuya kumuingilia kimwili.

“Usijali mke wangu, najua kwamba bado haupo sawa lakini hata ukikaa na mimi kama hivi naridhika, nakupenda sana,” alisema Msuya na kumbusu tena Brianna, msichana huyo akawa na uhakika kwamba Msuya hawezi kufanya chochote kwa siku hiyo. Ilikuwa kazi ngumu sana kwake kuzoea kuguswa sehemu mbalimbali za mwili wake na Msuya.
Siku hiyo ilikuwa ndefu sana kwa Brianna kwani muda wote Msuya alitaka wakumbatiane na kugandana kama ruba, jambo ambalo lilimpa sana shida Brianna kulizoea. Hata muda wa kulala ulipofika, Msuya alitaka walale kwa mfumo huohuo, tofauti na siku zote ambapo Brianna alikuwa akijitenga na kugeukia ukutani.

Usiku huo ulikuwa mrefu sana kwa Brianna, ni mpaka Msuya alipopitiwa na usingizi ndipo nafsi yake ilipotulia, muda mfupi baadaye na yeye akapitiwa na usingizi mpaka alfajiri ya siku ya pili.
Kwa kuwa walikubaliana kukaa kwa siku moja tu hotelini hapo, asubuhi walianza maandalizi ya kurejea nyumbani ambapo baada ya kupata kifungua kinywa, walijiandaa na kutoka mpaka kwenye maegesho ya magari ambapo gari la kifahari la mzee huyo lilikuwa limeegeshwa.

“Namshukuru sana Mungu kwa sababu angalau umeanza kurudi kwenye hali yako ya kawaida, nakupenda sana mke wangu,” alisema Msuya na kumbusu Brianna wakiwa ndani ya gari, msichana huyo akaachia tabasamu pana huku akijitahidi siri kubwa iliyokuwa ndani ya moyo wake isifichuke haraka.

Hatimaye waliondoka na kurejea nyumbani kwao, Msuya akionesha kuwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake. Kile alichokiona kama mabadiliko mazuri ya mkewe kilimfurahisha sana ndani ya moyo wake.
Baada ya kuwasili nyumbani, Brianna aliwasabahi watu wote ndani ya nyumba hiyo, kuanzia Diego, wafanyakazi mpaka watoto wa Msuya, tena kwa uchangamfu mkubwa, tofauti kabisa na Arianna.

Baada ya kupumzika kidogo, Msuya alitoka na kwenda kwenye shughuli zake za kila siku, huku nyuma Brianna akaanza kushirikiana na wale wafanyakazi kwenye shughuli mbalimbali za nyumbani na baada ya kumaliza, alikaa na watoto wa Msuya kwenye bustani zilizokuwa nje ya nyumba hiyo, akawa anawasimulia mambo mbalimbali yaliyowafurahisha sana.
Kwa siku zote hizo, Diego alikuwa akitafuta upenyo wa kumuingia Brianna ili ikiwezekana, aanzishe naye uhusiano wa kimapenzi kama ilivyokuwa kwa Arianna lakini kila alipokuwa anamtazama jinsi anavyojiheshimu, alikuwa akigwaya, moyoni akawa anajiapiza kwamba lazima ipo siku atamueleza suala hilo ingawa hakutaka kuwa na haraka.
***
Baada ya safari ndefu na ngumu, hatimaye Arianna aliwasili kwenye Mji wa Mandera uliokuwa Kaskazini mwa Kenya, jirani na mpaka wa nchi hiyo na Somalia. Hakuwahi kufika hata mara moja kwenye mji huo na hakuwa na mtu yeyote aliyekuwa anamfahamu lakini kwa kuwa alikuwa na fedha za kutosha, aliamini kila kitu kitaenda kama alivyopanga.
Baada ya kuteremka kwenye basi la Nyayo Express kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi cha Mandera akitokea Naairobi, Arianna alikodi teksi na kumuelekeza dereva kumpeleka kwenye hoteli yoyote nzuri iliyokuwa jirani na eneo hilo. Muda mfupi baadaye, teksi aliyopanda ilisimama mbele ya jengo la kifahari lililokuwa na maandishi makubwa yaliyosomeka; Kornesh Hotel and Lodging!
“Marwo soo dhaweyn Kornesh!” (Karibu sana dada hapa Kornesh) mhudumu wa kike alisema kwa lugha ya Kisomali, akiwa amechangamka huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake, Arianna akabaki kumtazama kwani hakuelewa anamaanisha nini.
“You are welcome madam at Kornesh” alirudia msichana huyo kwa Kiingereza, safari hii Arianna alimuelewa, wakapeana mikono kwa uchangamfu kisha akamsaidia kubeba begi lake dogo na kuingia mpaka mapokezi, akalipia chumba na kupelekwa na mhudumu yule.

Alipoingia chumbani kwake, hakukaa sana kutokana na jinsi alivyokuwa anasumbuliwa na arosto ya madawa ya kulevya. Baada ya kuweka vitu vyake vizuri na kuhakikisha mzigo wake wa fedha uko salama, alioga na kutoka mpaka nje ya hoteli hiyo, akaanza kusaka machimbo anayoweza kupata madawa ya kulevya.
Kutokana na maumivu aliyokuwa anayapata, hakuona hatari kuuliza sehemu ambazo hata haziingiliki. Muda mfupi baadaye, alikutana na kijana mwenye asili ya Kisomali aliyeahidi kumpeleka yanapouzwa madawa hayo lakini akataka alipwe kabisa ujira wake.

Kwa kuwa alikuwa na fedha za Kenya, Arianna alitoa fedha na kumpa kijana huyo, wakaongozana kuelekea mahali yanakouzwa madawa hayo. Baada ya kukatiza mitaa mingi, hatimaye walitokea nyuma ya ukumbi mkubwa wa mikutano wa Mandera Town Hall, wakaingia kwenye vibanda vilivyokuwa vimejengwa kwa mabati mpaka ndanindani kabisa.
Kutokana na mazingira jinsi yalivyokuwa hatarishi, Arianna alipopewa madawa na muuzaji aliyekuwa amefuga ndevu nyingi alizozipaka rangi, huku kichwani akiwa hana nywele hata moja, Arianna aliondoka na kijana yule na kurudi mpaka kwenye Hoteli ya Kornesh alikofikia.
Akapitiliza mpaka kwenye chumba chake, akajifungia milango yote na kutoa bomba la sindano kwenye begi lake, akaanza kuandaa madawa hayo mwisho akatoa kamba aliyoifunga kwenye mkono wake wa kushoto na kuanza kutafuta mshipa mkubwa wa damu.

Alipoupata, alijidunga na muda mfupi baadaye, alikuwa akielea kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa. Hata hivyo, tofauti na madawa aliyozoea kutumia tangu akiwa nchini Tanzania, Cocaine aliyouziwa kwenye mji huo unaosifika kwa matukio mengi ya kihalifu, ilikuwa tofauti kabisa.
Muda mfupi baadaye, alianza kuhisi hali ya tofauti, kichwa kikawa kinamgonga kwa nguvu huku damu zikianza kumtoka mdomoni na puani. Ukichanganya na jinsi madawa hayo yalivyokuwa yamemlewesha, Arianna alikosa cha kufanya zaidi ya kujikongoja mpaka bafuni, akafungulia maji na kuingia kwenye sinki la kuogea, damu zikawa zinaendelea kumtoka kwa wingi huku maji yakijaa kwenye sinki hilo.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply