The House of Favourite Newspapers

The Beginning of My End (Mwanzo wa mwisho wangu )- 12

0

Kijana mdogo, Benjamin Semzaba, anafikishwa mbele ya mkono wa sheria akikabiliwa na kesi nzito ya mauaji. Baada ya kunguruma kwa kipindi kirefu, hatimaye kesi iliyokuwa inamkabili inaelekea kufika mwisho na hukumu kutolewa.
Ushahidi wote umeshakamilika na hakuna shaka kwamba Ben ndiye aliyeua kwani ukiachilia mbali ushahidi huo, yeye mwenyewe mara kwa mara amekuwa akikiri kwa kinywa chake kufanya mauaji hayo.

Hatimaye siku ya hukumu inawadia, Ben akiwa amedhoofika sana na kubadilika kutokana na mateso ya gerezani, anahukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia.

Upande wa pili, historia ya maisha ya Ben inaelezwa, tangu akiwa kijana mdogo kabisa, akiishi na mama yake pamoja na wadogo zake, Mtaa wa Maporomoko kwenye mji mdogo wa Tunduma.

Licha ya maisha ya kifukara anayopitia, anaonesha uwezo mkubwa darasani, anafaulu kwa kiwango cha juu na baada ya kuhitimu kidato sita, anaenda kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Akiwa chuoni hapo, anakutana na msichana mrembo, Gladness anayetokea kumpenda sana.
Je, nini kitafuatia?

SONGA NAYO…

Ooh! Karibu Gladness, pole na masomo,” alisema mlinzi huyo huku akimpokea msichana huyo mkoba wake mdogo aliokuwa amebeba, akawaongoza kuelekea ndani. Ben ambaye alikuwa nyuma, alibaki amepigwa na butwaa, akiwa haamini kama hapo ndiyo nyumbani kwa msichana huyo.
Kila kitu kilikuwa katika ubora wa hali ya juu, kuanzia nyumba yenyewe, mandhari ya kuzunguka nyumba hiyo mpaka magari yaliyokuwa yameegeshwa kwenye maegesho ndani ya nyumba hiyo, akabaki amepigwa na butwaa. Alijaribu kufananisha na maisha aliyokulia, akajikuta akizidi kukosa kujiamini.

“Vipi mbona umepooza ghafla? Mi sipendi kukuona ukiwa kwenye hali hiyo bwana,” alisema Gladness na kumsogelea Ben, akambusu kwenye shavu lake na kumfanya ashushe pumzi ndefu, kidogo hofu ikapungua ndani ya moyo wake.
Waliingia mpaka kwenye sebule nadhifu na ya kisasa, iliyokuwa imepangiliwa kwa namna iliyoifanya ivutie mno, akakaribishwa kwenye masofa mazuri ya kisasa, akakaa huku akiendelea kushangaashangaa.

Muda mfupi baadaye, msichana aliyekuwa amevalia kwa namna ambayo ilimfanya Ben asipate shida kugundua kwamba alikuwa ni mfanyakazi, alimfuata na kumsalimia kwa adabu, akamuuliza angependa kutumia kinywaji gani?
“Maji tu yanatosha,” alisema Ben huku akijiweka vizuri pale kwenye sofa. Muda mfupi baadaye, msichana huyo alirejea akiwa na maji pamoja na glasi, akammiminia na kumkaribisha, akaenda kuendelea na majukumu yake.

Muda mfupi baadaye, Gladness alitoka akiwa amebadilisha nguo na kuvaa nyingine, tofauti na zile alizokuja nazo, akaenda kuwasha runinga kubwa ya ukutani (flat screen) na kurudi kukaa pembeni ya Ben, akawa anampigisha stori za hapa na pale huku akimtaka kutokuwa na hofu kwa sababu wazazi wake hawana shida kabisa.
“Sasa utanitambulishaje?”
“Nitawaambia wewe ni mume wangu mtarajiwa,” alisema Gladness na kuangua kicheko kwa furaha. Mazungumzo yao yalikatishwa na mlango uliokuwa unafunguliwa, mwanamke aliyevaa kinadhifu akatoka ambapo bila hata kuuliza, Ben alijua kwamba ni mama yake kwa jinsi alivyokuwa amefanana na Gladness.

Akasimama na kumsalimu kwa adabu, mwanamke huyo akamuonesha uchangamfu ambao hakuutegemea. Gladness alimtambulisha Ben kwamba ndiye rafiki yake wa karibu kuliko mtu mwingine yeyote chuoni kwao, wakawa wanazungumza mambo mbalimbali ambapo mama yake Gladness alimuuliza Ben kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu familia yao na masomo kwa jumla.
Tofauti na Ben alivyokuwa akimfikiria, mwanamke huyo alikuwa mkarimu sana, hakuwa sawa na watu wengi wenye uwezo mkubwa wa kifedha ambao huwa na kasumba ya kuwadharau watu wenye uwezo wa chini kiuchumi.

Wakiwa wanaendelea na mazungumzo, walisikia geti kubwa likifunguliwa na mlinzi, gari la kifahari likaingia ambapo mwanaume wa makamo aliyekuwa akifanana na Gladness aliingia, msichana huyo akatoka mbio kwenda kumlaki kwani zilikuwa zimepita siku nyingi bila kuonana.
Kwa jinsi Gladness alivyokuwa akideka kwa baba yake, ungeweza kudhani ana miaka chini ya kumi! Picha ile ilitosha kumuonesha Ben jinsi msichana huyo alivyokuwa akipendwa na familia yake.

Naye alijumuika sebuleni ambapo alitambulishwa kwa Ben kama rafiki wa karibu wa binti yake, akampokea kwa uchangamfu na kuanza kuzungumza mambo mbalimbali. Kama ilivyokuwa kwa mkewe, baba yake Gladness naye alikuwa mchangamfu sana kwa Ben, ile hofu kubwa aliyokuwa nayo ndani ya moyo wake ikayeyuka kama theluji iyeyukavyo juani.
Walikaa pamoja kwa muda mrefu, wakizungumza mambo mbalimbali, chakula kikaandaliwa ambapo walikula pamoja kisha baada ya hapo, Ben na Gladness wakaanza kujiandaa kurudi chuoni kwani muda ulikuwa umeyoyoma sana.
Wazazi wa Gladness waliwasindikiza mpaka nje ya nyumba yao ambapo waliwakodia teksi ya kuwarudisha chuoni huku wakiwa wamewafungashia zawadi mbalimbali. Wakawa wanamsihi Ben aendelee kuwa karibu na binti yao na kumsaidia kwa chochote ambacho kitamsumbua wakiwa chuoni.

Huo ukawa mwanzo wa kijana huyo kufahamiana na familia hiyo, ukaribu kati yake na Gladness ukawa umeingia kwenye hatua nyingine, taratibu akaanza kujiamini mbele ya msichana huyo mrembo, wakaendelea kupendana maradufu huku mara kwa mara wakizungumzia jinsi maisha yao yatakavyokuwa baada ya kufunga ndoa na kuanza kuishi kama mume na mke.
Waliendelea na masomo yao huku Gladness akiendelea kuwa msaada mkubwa kwa Ben, mara kwa mara akawa anampa fedha za matumizi ambazo kijana huyo alikuwa akizibana na kuzituma nyumbani kwao kwa ajili ya kuisaidia familia yao.
“Ben!”
“Kwa nini huwa hupendi kuzungumza na mimi kuhusu familia yenu na kila nikikuuliza unanijibu kwa mkato?” Gladness alimuuliza Ben swali ambalo hakulitegemea, jioni moja wakiwa wanapunga upepo kwenye bustani za maua chuoni hapo.
Licha ya kujifanya mjanja wa kubadilisha mada linapokuja suala la familia yake, Gladness aliendelea kumshikia bango mpaka akakosa ujanja, akamtazama msichana huyo usoni huku machozi yakimlengalenga.
“Najua kuna kitu hakipo sawa na unanificha, ina maana mpaka leo huniamini Ben?”
“Hapana! Siyo hivyo Glad lakini naogopa kukupoteza.”
“Kivipi? Mbona sikuelewi?”
“Najua nikikwambia ukweli kuhusu familia yangu utanikimbia,” alisema Ben kwa huzuni, kauli iliyouchoma sana moyo wa Gladness, akaanza kumbembeleza Ben na kumtaka kuwa huru kwake kwa sababu alikuwa akimpenda kwa dhati kutoka ndani kabisa ya moyo wake na alikuwa tayari kuwa naye katika hali zote.

Ilibidi Ben amueleze ukweli, akamsimulia kila kitu katika maisha yake, kuanzia jinsi alivyosoma kwa shida na jinsi familia yao ilivyokuwa ikiishi maisha ya dhiki. Hakuacha kitu, alimueleza mambo yote yaliyowahi kumtokea maishani mwake, jinsi alivyompoteza mdogo wake kwa sababu ya ufukara na jinsi mama yake alivyokuwa akiteseka kwa maradhi ya kifua, yaliyosababishwa na kukaa muda mrefu kwenye moto akipika vitumbua.

Simulizi hiyo iliugusa mno moyo wa Gladness, akashindwa kuzificha hisia zake, akawa analia kama mtoto mdogo huku akiwa amemkumbatia Ben kifuani. Ilibidi kijana huyo ndiyo aanze kazi ya kumbembeleza na kumtaka achukulie kawaida kila kitu.

“Nataka kwenda kuiona familia yako, wikiendi hii nitamuomba baba atukatie tiketi mbili za ndege, tutaenda Ijumaa na kurudi Jumapili,” alisema Gladness huku akifuta machozi. Hakuna kitu kilichomuumiza moyo wake kama kugundua kwamba kumbe Ben alikuwa akimficha hayo yote kwa sababu aliamini kwamba atamdharau na kumkimbia, akaamua kumdhihirishia kwa vitendo kwamba anampenda kwa dhati kutoka ndani ya moyo wake.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumamosi kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave A Reply