The House of Favourite Newspapers

The World You Left Behind 38

0

Matumizi mabaya ya fedha za serikali na ubadhirifu mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, vinamsababishia waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa matatizo makubwa na kufanya roho yake iwindwe kwa udi na uvumba.

Wanaomuwinda ni viongozi wenzake na wafanyabiashara waliokuwa wakimuona kama kikwazo kutokana na tabia yake ya kukemea ufisadi.

Mpango wa hatari wa kuyakatisha maisha yake unaandaliwa na kwa bahati nzuri, Grace, mwanamke aliyekutana naye kwenye mazingira ya kutatanisha, anamueleza kuhusu mpango huo na kumpa mbinu za nini cha kufanya ili kunusuru maisha yake.

Hatimaye siku ya tukio inawadia na kwa utaalamu wa hali ya juu, Grace anamuokoa Magesa huku watu wengine wote wakiamini kwamba waziri huyo amekufa kwenye ajali hiyo. Wawili hao wanatorokea mafichoni Mombasa, Kenya ambako Magesa analazimika kuanza maisha mapya kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.

Grace anasafiri kuelekea Israel kikazi na Magesa anaitumia nafasi hiyo kumpekua mwanamke huyo akitaka kuujua ukweli wa maisha yake. Anachokutana nacho kinamshangaza sana.

Je, nini kitafuatia?

SONGA NAYO…

“Vipi mbona umeshtuka sana Grace?”

“Umenishtua Magesa, kumbe nimekuamini na kukuacha hapa nyumbani kwangu matokeo yake unaanza kunipekua?”

“Samahani kama nimekosea Grace lakini naomba uniambie ukweli. Unajua ni kwa kiasi gani haya mambo yanayotokea yalivyoniathiri kisaikolojia. Sijui nani nimuamini na nani nisimuamini, tafadhali nakuomba uniambie ukweli,” alisema Magesa huku akionesha kuwa na wasiwasi mkubwa ndani ya moyo wake.

“Unataka kuujua ukweli?”

“Ndiyo Grace! Nahitaji kuujua ukweli kuhusu wewe na yote ninayokuuliza. Nahitaji kukuamini lakini haiwezi kuwa rahisi kwa sababu nina maswali mengi ndani ya kichwa changu ambayo yanahitaji majibu na wewe ndiyo mtu pekee unayeweza kunipa majibu,” alisema Magesa, Grace akashusha pumzi ndefu na kumsogelea Magesa.

“Unamfahamu Bertha Sapula?”

“Ndiyo namfahamu, nilisoma naye Shule ya Sekondari Tunduma, mpakani mwa Tanzania na Zambia.”

“Unakumbuka nini kuhusu yeye?”

“Alikuwa rafiki yangu sana, nilimpenda na yeye alinipenda sana, tukaishia kuwa wapenzi. Nakumbuka siku nilipohamia shule hiyo, nikitokea Iringa, yeye ndiye aliyenipokea na kunionesha mazingira ya shule. Tulipendana sana kiukweli.”

“Nini kilichokuja kuwatenganisha?”

“Sijui ni akili za kitoto au ni nini?Tulipofika kidato cha nne kuna mwanafunzi mwingine wa kike alihamia shuleni kwetu, akatokea kunipenda sana bila kujali kwamba nilikuwa tayari nina mpenzi, jambo ambalo lilikuwa likimkasirisha sana Bertha, huo ndiyo ukawa mwanzo wa uhusiano wetu kulegalega.”

“Msichana mwenyewe aliyehamia alikuwa anaitwa Tusekile Mwankenja, si ndiyo?”

“Grace! Umemjuaje? Kwani na wewe ulisoma Tunduma? Umelijuaje jina la msichana huyo?” alisema Magesa huku akionesha kupatwa na mshtuko mkubwa ndani ya moyo wake. Ni kweli msichana aliyehamia shuleni hapo alikuwa anaitwa Tusekile Mwanjenja na ndiye aliyesababisha kwa kiasi kikubwa uhusiano wake na Bertha ulegelege na baadaye kuvunjika kabisa.

Kitendo cha Grace kulitaja jina kamili la msichana huyo kilimshtua mno Magesa, akazidi kuwa na maswali mengi yaliyokosa majibu.

“Ni kweli ulikuwa unampenda Bertha?”

“Nilikuwa nampenda sana na tuliahidiana kwamba tukimaliza masomo tutaishi pamoja kama mume na mke, sema akili za utoto ndiyo zilizotutenganisha.”

“Unajua kwa sasa Bertha yuko wapi?”

“Sijui chochote kuhusu yeye, nimejaribu kumtafuta kwa kipindi kirefu lakini sijawahi kupata taarifa zozote zinazomhusu tangu tulipohitimu kidato cha nne.”

“Ukipata nafasi ya kukutana naye leo utamwambia nini?” alihoji Grace huku akisimama na kuelekea kwenye friji, akafungua na kutoa chupa ya ‘wine’ ya Red Cape aliyokuwa anapenda kuitumia, akachukua glasi mbili na kurudi pale Magesa alipokuwa amekaa.

“Hujanijibu, ukipata nafasi ya kukutana naye leo utamwambia nini?”

“Nitamuomba radhi kwa yote yaliyotokea, hakustahili kuumizwa moyo wake kwa sababu alikuwa na mapenzi ya dhati kwangu, nakumbuka sana yote tuliyoyafanya tukiwa bado vijana wadogo,” alisema Magesa na kujiinamia, Grace akamimina ‘wine’ kwenye glasi mbili, ya kwake na ya Magesa kisha akanywa funda moja na kumtazama Magesa usoni.

“Abbas! Unakumbuka Bertha alikuwa na alama gani kwenye mwili wake ambayo ukiiona hata leo huwezi kuisahau?” Grace aliuliza swali lingine lililozidi kumuweka Magesa kwenye wakati mgumu, akamtumbulia macho Grace kwa mshangao, mwanamke huyo akasimama na kuvua gauni alilokuwa amelivaa safarini.

Akavua blauzi aliyokuwa ameivaa ndani, juu akabaki na sidiria iliyokuwa imekisitiri vizuri kifua chake kilichojaa vizuri na kupendezeshwa na ‘vifuu’ viwili, chini akabaki na ‘skin tight’ iliyombana na kuonesha vyema umbo lake zuri lenye mvuto wa kipekee.

Akageuka na kumpa Magesa mgongo, macho yake yakatua moja kwa moja kwenye kovu lililokuwa upande wa bega la kushoto la mwanamke huyo mrembo, mapigo ya moyo yakamlipuka Magesa na kuanza kwenda mbio kuliko kawaida.

Akili zake zilimrudisha miaka mingi nyuma, akakumbuka kuwa Bertha, mpenzi wake wa sekondari, alikuwa na kovu kama hilohilo na mara kwa mara alipokuwa naye faragha, hakuisha kumtania kwamba amejichorwa tatuu ya asili na Mungu ambayo haiwezi kufutika maisha yake yote.

Akiwa katika hali ya taharuki kubwa, Grace alimgeukia na kuachia tabasamu pana, taratibu akamsogelea Magesa pale alipokuwa amekaa, kijasho chembamba kikimtoka, akamuinamia na kumbusu kwenye paji la uso, akamkalia kwenye mapaja na kumkumbatia kimahaba.

“Umeshapata majibu uliyokuwa unayatafuta?” alihoji Grace huku akiinua glasi yake na kupiga funda jingine kisha akamnywesha na Magesa na kumbusu tena mdomoni.

“Unataka ku..sema we…we ni Bertha?” Magesa alihoji huku akibabaika, hofu kubwa ikiwa imetanda kwenye uso wake, Grace akainuka pale alipokuwa amemkalia na kukaa pembeni yake, akashusha pumzi ndefu na kuanza kumfafanulia Magesa kila kitu kilichotokea tangu walipoachana.

Mwanamke huyo alieleza jinsi alivyoendelea na masomo ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Iringa (Iringa Girls High School), jinsi alivyojiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea shahada ya kwanza ya sheria kabla ya baadaye kujiunga na jeshi.

“Uwezo wangu mkubwa jeshini ulisababisha nichukuliwe na maafisa wa Israel waliokuwa wakitufundisha mafunzo ya kijeshi, nikapelekwa Tikva nchini Israel kujiunga na chuo cha ujasusi cha Israeli College for Security and Investigation au kwa kifupi ICSI, nikasomea kozi maalum ya Investigations and Intelligence Program.

“Huko nako nilionesha uwezo mkubwa, nikapata nafasi nyingine ya kwenda kuendelea na masomo ya kupambana na ugaidi wa kimataifa, rushwa na ufisadi kwenye Chuo cha Glavnoye Razvedyvatel’noye Upravleniye (GRU) jijini Moscow, Urusi. Hivi sasa nafanya kazi na Polisi wa Kimataifa, Interpol,” alisema Grace, Magesa akabaki amepigwa na butwaa akiwa ni kama haamini kabisa alichokisikia.

“Sasa mbona umebadilika sura umekuwa tofauti kabisa na Bertha ninayemfahamu?”

“Nipo kwenye kazi maalum, hii ni sura maalum ya kazi lakini nitakapomaliza ninachokifanya, nitaenda tena nchini Thailand kurekebishwa na kurudishiwa sura yangu halisi.

Je, nini kitafuatia? Usikose kufuatilia siku ya Ijumaa kwenye Gazeti la Uwazi Mizengwe ya Uchaguzi.

Leave A Reply