The House of Favourite Newspapers

Tigo Yaadhimia Kupanda Miti 28,000 Kuadhimisha Siku ya Mazingira Juni 5

0

Siku hiyo huleta pamoja serikali, mashirika ya biashara, wananchi na makampuni mbalimbali kwa ajili ya kushughulikia masuala nyeti yanayoathiri mazingira.

Siku ya Mazingira Duniani ni jukwaa la kimataifa la kuleta mabadiliko chanya, huhimiza watu mbalimbali kutafakari kuhusu masuala yanayohusu mazingira na kuhakikisha wanaendelea kuyatunza kwa manufaa yao.

Makampuni na mashirika mbalimbali wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanabuni mifumo isiyochafua mazingira na kuyatunza ikiwemo kupanda miti kila wakati.

Pia kwa kiasi kikubwa hutumika kuelimisha jamii kwa namna moja au nyingine kuhusu suala la kutunza mazingira kwa manufaa mbalimbali.

Kampuni inayoongoza kwa maisha ya kidijitali ya Tigo Tanzania, imeadhimia kuipanda miti 28,000 mwaka huu katika eneo la kuzunguka Mlima Kilimanjaro.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo, Simon Karikari, yeye binafsi, amefanikiwa kuchangia miti 100 katika kufanikisha suala kwa mwaka huu.

Anasema ameongeza miti 100 katika miti 10,000 nambayo ilishatolewa na Kampuni ya Tigo kwa ajili ya kuboresha zaidi mazingira yanayozunguka Mlima Kilimanjaro.

Kampeni hiyo iliyopewa jina la Tigo Green For Kili iliyozinduliwa Februari 27, mwaka huu.

Karikari anasema anafurahia kwa kiasi kikubwa kuchangia kiasi hicho cha miti na kuwashawishi Wakurugenzi wenzake ikiwemo wa Bank ya Standard Chartered, Sanjay Rughani kuchangia kampeni hiyo kwa kutoa miti 100 ambapo mti mmoja gharama yake ni sh. 5,000.

“Februari 27 mwaka huu, tulizindua kampeni ya kupanda miti ya Tigo Green For Kili ambayo malengo yake ni kupanda miti 28,000 katika eneo la kuzunguka Mlima Kilimanjaro.

“Ninafurahia kuchagia miti 100 baada ya kampuni yangu kuchangia miti 10,000 kwa ajili ya kufanikisha kampeni hiyo.

“Pia nimewashawishi na wakurugenzi wenzangu ikiwemo wa Bank ya Standard Chartered Tanzania, Sanjay Rughani kuchagia miti 100 ambapo kila mti mmoja unauzwa kwa sh. 5,000,” anasema Karikari.

Anasema kampeni hiyo inaenda sambamba na kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani ambayo imekuwa ikifanyika kila mwaka.

“Kwa niaba ya Tigo Tanzania, ninachukua fursa hii kuwashukuru wote waliojitokeza kutuunga mkono kuchangia katika kufanikisha suala la kupanda miti ambayo itakuwa sehemu mojawapo ya kulinda na kuendeleza mazingira kwenye eno la Mlima Kilimanjaro.

Anawataja Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa na Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Clouds Media Group, Joseph Kusaga ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha suala hilo.

Kuelekea maadhimisho ya siku ya mazingira duniani ambayo yatakua tarehe tano mwezi wa sita yenye kauli mbiu isemayo ‘Kurejesha Mfumo wa Ikolojia’, ninapenda kuwafahamisha wadau wetu kwamba Tigo tutakuwa na hafla ya kupanda miti,katika viwanja vya Half London,jijini Moshi. Vile vile bado tunaendelea kupokea michango ili kufikia lengo letu la kupanda miti 28,000 mwaka huu.

Gharama ya mti mmoja ni sh. 5,000 na hii inajumuisha utunzaji wa ukuaji wa mti huo kwa muda wa miezi kumi na nane. Unaweza kuchangia miti mingi uwezavyo kwa kupitia Tigo Pesa, Lipa kwa Simu namba 9867912.

Kwa niaba ya Tigo Tanzania, napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru wadau wote walioitikia wito huu na kuchangia ili kuifanya Kilimanjaro iwe ya Kijani tena.

Anasema wanatambua umuhimu wa Mkoa wa Kilimanjaro katika uchangiaji wa uchumi na ustawi wa nchi ya Tanzania kwa ujumla.

Anasema mkoa wa Kilimanjaro ni wa kipekee, ni maarufu kutokana na uwepo wa Mlima Kilimanjaro, mlima mrefu zaidi barani Afrika. Mlima ambao ni tunu ambayo kwa wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro na nchi nzima wanajivunia.

Aidha, anasema Mkoa wa Kilimanjaro ni kitovu cha utalii kwa eneo la Kaskazini mwa nchi ambako ni lango la kuelekea maeneo mengi ya kuvutia kama Hifadhi ya taifa ya Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa Mkomazi, Milima maarufu ya Pare, Ziwa Jipe pamoja na Ziwa Chala. Pia, kuna misitu ya kuvutia ya kitropiki, maporomoko ya maji na mandhari za kuvutia.

Anasema kama haitoshi, Mkoa huo una fursa nyingi za kilimo na uwekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi kuanzia elimu, afya, usafirishaji, huduma za usafiri wa anga na nyingine nyingi.

Anasema lengo kuu la mradi huo ni kusaidia uhifadhi wa Mlima Kilimanjaro kwa kupanda miti mingi iwezekanavyo na kwa kuanzia Tigo imejitolea jumla ya miti 10,000.

“Ni imani yetu kuwa miti hii itasaidia kurejesha sehemu ya theluji kwenye Mlima Kilimanjaro ambayo tumeshuhudia ikipungua kwa miaka minne iliyopita kwa sababu ya ongezeko la joto duniani,” anasema.

Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Kaskazini, Henry Kinabo, anasema wanafurahia kushirikiana na wadau mbalimbali katika kufanikisha kampeni hiyo.

Anasema wanaamini miti hiyo ikitunzwa vizuri italeta manufaa makubwa ikiwemo kutunza mazingira yanayozunguka Mlima Kilimanjaro.

“Tunafurahia kushirikiana na wadau mbalimbali katika kufanikisha kampeni hii ambayo itakua endelevu, na miti ikitunzwa vizuri ni faida kwetu kwa baadaye.

“Hii ndio sababu kama Tigo, tuna kauli mbiu isemayo “One step,One0 Tree”  kwa ajili ya kuunganisha nguvu ili kuhifadhi Mlima Kilimanjaro ambao utasaidia kuleta maendeleo endelevu ya mkoa na taifa kwa ujumla.

Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake la VOEWEFO anasema kuwa wanaishukuru Tigo kwa kuwaamini na kwamba wanaahidi kuitunza miti hiyo katika Wilaya ya Hai.

“Tuna imani kuwa nia yetu njema ya mradi wa Tigo Green for Kili ni kuhakikisha inaendana na mipango ya maendeleo ya mkoa huu,” anasema.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Maiputa Wilaya ya Hai, Benson Ndosi, anasema wanashukuru kwa ujio wa Tigo kwa kufanikisha mradi huo.

Anasema anawaomba wananchi kuhakikisha wanaendelea kuitunza miti hiyo ikiwemo Mlima Kilimanjaro kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.

Leave A Reply