The House of Favourite Newspapers

Timothy; Mtoto Weah Anayeichezea Marekani

SOKA ndiyo mchezo unaopendwa zaidi duniani kwa sasa na umekuwa ukizalisha wachezaji wengi sana maarufu.

Rais wa Liberia, George Weah, ni mchezaji wa zamani mahiri na anafahamika duniani kote kutokana na rekodi zake wakati akicheza soka.

 

Staa huyo alifanya mambo makubwa na ndiye mchezaji pekee Mwafrika ambaye aliweza kupata nafasi ya kuwa Mchezaji Bora wa Dunia kwa kipindi chake na hadi sasa bado hakuna matumaini kama kuna mwingine anaweza kutokea.

Rais wa Liberia, George Weah akiwa na mwanae Timothy Weah maarufu kama Tim

Lakini baada ya staa huyo kuachana na soka sasa kuna mtoto wake, Timothy Weah maarufu kama Tim ambaye ameonekana kuanza kutikisa ulimwenguni kutokana na kiwango cha juu ambacho amekuwa akikionyesha uwanjani.

 

Kinda huyo ambaye anakitumikia kikosi cha PSG, tayari ameshaonyesha kuwa ni mchezaji ambaye atatikisa kwenye soka pamoja na kwamba ameshacheza michezo miwili tu kwenye timu ya wakubwa ya PSG ya nchini Ufaransa.

Hata hivyo, ajabu ni kwamba pamoja na mchezaji huyo baba yake kuwa rais wa Liberia lakini juzi alitangaza kuwa ataichezea timu ya taifa ya Marekani na hana mpango wa kwenda nchini kwao.

 

Kinda huyo mwenye umri wa miaka 18 alizaliwa kwenye Mji wa New York hali ambayo inampa nafasi ya kuwa Mmarekani.

Timothy juzi aliitwa kwenye timu ya wakubwa ya Marekani, kwa mara ya kwanza na mwenyewe alisema kuwa amefurahishwa na taarifa hiyo.

Mshambuliaji huyo alikuwa anatarajiwa kuanza kwenye benchi katika mchezo wa jana wa kirafiki kati ya Marekani na Paraguay, ukiwa ni mchezo wake wa kwanza wa kimataifa.

Katika michuano ya vijana mchezaji huyo alionyesha kiwango cha juu kwenye michuano ya vijana chini ya miaka 17 ambapo kwenye mchezo dhidi ya Paraguay alifanikiwa kufunga mabao matatu ‘hat trick’.

 

Mmoja wa makocha wa Marekani, Dave Sarachan, alipoulizwa kwa nini amemuita mchezaji huyo pamoja na kwamba ni mdogo sana alisema:

“Tim amekuwa mchezaji muhimu kwenye timu za vijana, naamini kuwa anaweza kufanya mambo makubwa kwenye timu ya taifa.

 

“Amekuwa akiitumikia klabu bora duniani na amekuwa akicheza angalau dakika kadhaa kwenye kikosi cha kwanza, ni mchezaji mahiri,” alisema kocha huyo.

Timothy alizaliwa kwenye mji wa Brooklyn, New York, Februari 22, mwaka 2000, baba yake wakati huo bado alikuwa akicheza soka.

Awali kabla hajajiunga na PSG, Timothy alizichezea timu za Brooklyn, Pembroke Pines na baadaye alikwenda Florida ambapo aliichezea timu ya West Pines United.

 

Baada ya kuichezea US Soccer Development Academy, kwa miaka mitatu, aliondoka na kwenda kujiunga na timu ya vijana ya New York Red Bulls, kabla hajaenda nchini Ufaransa.

Mwaka 2014, akiwa na umri wa miaka 13 tu, Weah alifanya majaribio kwenye kikosi cha Chelsea, lakini kabla hata majibu hayajatoka aliondoka na kwenda zake PSG.

 

Moja ya jambo ambalo linamfanya akumbukwe ni kitendo cha kufunga mabao matatu ‘hat-trick’ kwenye Ligi ya Uefa ya vijana wakati PSG walipokuwa wakicheza na Ludogorets.

Baada ya kukaa kwa muda mfupi na timu ya vijana alijiunga na PSG mwaka jana mwanzoni.

Tim Weah alicheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Troyes ambao walishinda mabao 2-0 na nusura afunge bao dakika za mwisho baada ya kupiga shuti kali lakini kipa akaokoa.

 

Kuanzia 2015, Timothy amefanikiwa kucheza michezo 14 ya timu za vijana za Marekani akiwa amefunga mabao sita.

Amekuwa akitajwa kuwa mshambuliaji mwenye kasi ya hali ya juu lakini mwenye uwezo wa kucheza upande wa kulia na kushoto.

 

Mbali na kuwa mwanasoka, inaelezwa kuwa kinda huyo amekuwa akipenda muziki.

Kuanzia mwanzoni mwa mwaka jana, kijana huyo amefanikiwa kurekodi nyimbo sita na ana mpango wa kufungua studio nchini Liberia.

Comments are closed.