The House of Favourite Newspapers

Timu Ya Afya Ilemela Yapewa Siku 30 Kujitathmini

0
Mkurugenzi wa huduma za Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais -TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume

Mkurugenzi wa huduma za Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais -TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume ametoa mwezi mmoja kwa timu ya usimamizi wa huduma za Afya ya halmashauri (CHMT) Ilemela kujitathmini na kujirekebisha katika kusimamia maeneo ya kutolea huduma za Afya ikiwamo kituo cha Afya Buswelu.

Dkt. Mfaume ametoa maelekezo hayo baada ya kukagua shughuli za uendeshaji na usimamizi wa shughuli za Afya katika kituo cha Afya Buswelu wilaya ya Ilemela mkoa wa Mwanza akiwa ameambatana na timu ya Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI.

Akifafanua kuhusu mapungufu yaliyobainika Dkt. Mfaume amesema kituo hicho hakina mfumo wa kielektroniki wa udhibiti wa taarifa za wagonjwa na mapato (GoTHoMIS),huduma isiyoridhisha ya maabara pamoja na kiwango cha chini cha ukusanyaji wa mapato.

« Ukiangalia mapato, kituo kimekusanya laki mbili na tisini na nne (294,000/=) kwa muda wa miezi tisa, kiuwajibikaji kwakweli mpo chini sana CHMT ya Ilemela yaani kuna ulegevu wa usimamizi wa huduma natoa mwezi mmoja mbadilike kiusimamizi yaani miezi tisa kukusanya laki mbili na tisini na nne haiwezekani » amesema Dkt. Mfaume

Aidha,amemwelekeza mganga mkuu wa halmashauri ya Buswelu kufanya mabadiliko ya mganga mfawidhi wa kituo cha Afya Buswelu baada ya kushindwa kusimamia shughuli za utoaji huduma za Afya na kuwaunganisha watumishi katika kituo hicho.

Akipokea maelekezo hayo mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Rutachunzibwa amesema mabadiliko hayo yanaanza kufanyiwa kazi mara moja na mrejesho utawasilishwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI.

Timu ya Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI ipo mkoa wa Mwanza kukagua shughuli za uendeshaji na usimamizi wa shughuli za Afya katika Mkoa wa Mwanza na itakutana na timu za usimamizi wa Huduma za Afya za Halmashauri CHMTs za mkoa wa Mwanza pamoja na ile ya mkoa RHMT.

Leave A Reply