The House of Favourite Newspapers

Top 10 ya Mabondia Bora Tanzania

0

UKIACHANA na mchezo wa soka ambao umekuwa na wafuatiliaji wengi zaidi duniani, mchezo ambao pia unafuatiliwa na mashabiki ni ule wa ngumi za kulipwa ambao pia una fedha ya kutosha licha ya kuchukua dakika chache tu ndani ya ulingo tofauti na soka.

 

Kawaida mchezo wa ngumi ni mchezo wa matajiri, lakini asilimia kubwa ya mabondia wanaoshiriki wametokea kwenye familia za hali ya chini ambao wamekuwa wakisaka fedha kupitia mchezo huo. Angalia historia ya Manny Pacquiao, Floyd Mayweather, Canelo Alvarez, Anthony Joshua, Michael Maidana au ukija Bongo angalia mabondia wa zamani kama Rashid Matumla, Francis Cheka na wengineo, wote wametokea kwenye maisha ya msoto.

 

Hali hiyo imesababisha kuwa bora na kushika nafasi za juu kitaifa na kimataifa katika viwango vya ubora, kwa kuwa muda mwingi walifanya kazi yao kwa kutaka kuwa bora kiviwango. Championi Jumatatu, linakuchambulia mabondia kumi bora wa Tanzania kwa sasa kutokana na rekodi zao na ubora ambao wamekuwa wakionyesha katika mapambano yao.

 

1. HASSAN MWAKINYO

Kutoka Tanga, Makorora, bondia Hassan Mwakinyo anayecheza kwenye uzito wa Super Walter ndiyo bondia namba moja kwa ubora nchini akiwa na nyota nne, hii ikiwa ni katika ujumla wa madaraja yote ya uzito. Mwakinyo mwenye rekodi ya kucheza mapambano 22, ameshinda 20 kati ya hayo 14 ni kwa KO na amepoteza mapambano mawili pekee kati ya hayo moja ni kwa KO.

 

 2.IBRAHIM CLASS

Hakuna asiyetambua kazi na ukubwa wa Ibrahim Class katika mchezo wa ngumi za kulipwa Bongo kutokana na kuwa na kiwango na uwezo mkubwa miaka yote. Kwa mujibu wa Boxrec ambao ni mtandao unaotumika kuhifadhi kumbukumbu za mabondia, Class mwenye rekodi ya mapambano 32 akiwa ameshinda 26 kati ya hayo 11 kwa KO, amepoteza mapambano sita kati ya hayo matatu ni kwa KO ndiyo bondia namba mbili kwa ubora Bongo.

 

3. FADHILI MAJIHA

Mara nyingi huwa hatajwi sana na wengine huenda wakawa hawamtambui, lakini Fadhili Majiha ‘Stopper’ ndiyo bondia wa tatu kwa ubora nchini. Majiha ndiye bondia aliyeshinda mapambano mengi nje ya Bongo kuliko bondia yeyote akiwa na rekodi ya kucheza jumla ya mapambano 46 akiwa ameshinda 28 kati ya hayo 14 ni KO na amepoteza 14, kati ya hayo matatu ni kwa KO na ametoka sare mara nne.

 

4. SALIM MTANGO

Bondia mwingine kutoka Makorora mkoani Tanga, Salim Mtango ndiye anayekamata nafasi ya nne katika mabondia bora wa Tanzania. Mtango siyo jina geni kwa wapenzi wa ngumi kutokana na kipaji chake katika mchezo huo. Bondia huyo amecheza jumla ya mapambano 21 akiwa ameshinda 16 kati ya hayo kumi ni kwa KO, amepoteza mapambano manne kati ya hayo mawili ni kwa KO na ametoa sare moja.

 

5. TONY RASHID

Kutoka Mbezi ndani ya Gym ya Amoma Boxing Academy, Tony Rashid AK47 ameikamata nafasi ya tano. Bondia huyo ambaye ni bingwa wa zamani wa ABU anapanda ulingoni Februari 25, mwaka huu kugombania mkanda wake na Bongani Mahlangu wa Afrika Kusini. Tony ana rekodi ya kucheza jumla ya mapambano 17 akiwa ameshinda 13 kati ya hayo kumi yakiwa ni KO na amepoteza mapambano mawili, moja likiwa ni KO na kutoka sare mapambano mawili.

 

6. MUSKIN SWALEHE

Mtaani kwa sasa anatambulika kwa jina Alkasusu kutokana na staili yake ya kuachia ndevu na kuvalia kanzu fupi kama wale wauza Alkasusu, huyu anashika nafasi ya sita katika mchezo wa ngumi za kulipwa Bongo. Alkasusu ana rekodi ya kucheza mapambano 11 akiwa ameshinda tisa kati ya hayo moja ni kwa KO, amepoteza pambano moja na ametoka sare moja.

 

7. INNOCENT EVARIST

Innocent Evarist, huyu jamaa wengi hawamtambui kabisa, lakini ndiyo bondia anayekamata nafasi ya saba kwa mabondia bora wa Bongo. Bondia huyu ana rekodi ya kucheza mapambano 15 akiwa ameshinda 11 kati ya hayo tisa ni kwa KO, amepoteza moja kwa KO na sare moja. Mbali ya kuwa bondia, Evarist ni ‘match-maker’ ambaye ameweza kuandaa mechi saba mpaka sasa.

 

8. ISMAIL GALIATANO

Kutoka katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ‘JWTZ’, bondia mwenye cheo cha Koplo, Ismail Galiatano ndiye anayekamata nafasi ya nane kwenye listi hii. Galiatano mwenye rekodi ya kucheza mapambano 15 akiwa ameshinda kumi kati ya hayo mawili ni kwa KO, amepoteza mawili kati ya hayo moja ni kwa KO na ametoka sare matatu.

 

9. LOREN JAPHET

Kwa sasa amehamishia makazi yake Ghana lakini anakamata nafasi ya nane katika mabondia bora wa Bongo. Japhet licha ya kuwa bora lakini ni mmoja kati ya mabondia wenye vipaji vikubwa kwenye mchezo huo. Japhet amecheza jumla ya mapambano 18 akiwa ameshinda 11 kati ya hayo matatu ni kwa KO na amepoteza mapambano matano kati ya hayo mawili ni KO.

 

10. TWAHA KIDUKU

Hadi watoto wadogo mtaani wanamtambua kama Mzee wa Showshow, Twaha Kassim Rubaha maarufu zaidi kwa jina la Twaha Kiduku ndiye anayefunga dimba kwa kushika nafasi ya kumi akiwa ni bondia aliyecheza mapambano 27 na kati ya hayo, ameshinda 18, nane kwa KO na amepoteza mapambano nane ambapo moja ni kwa KO na ametoka sare pambano moja.

IBRAHIM MUSSA, Dar es Salaam

Leave A Reply