The House of Favourite Newspapers

TRENI HAITEMBEI KWENYE LAMI

SHOGAA eeeeh kwanza una kifua? Nisije sema neno hapa ukadondoka kwa kukosa pumzi bureee! Heee heeeiyaa wanakwambia kigodoro hakina muziki laini bibi weeee!  Kuku hachunguzwi afya hadi afariki mwenyewe, upo nyonyo? Ukitaka kujua pasi kama inachoma au inaunguza iwashe kisha iweke kwenye nailoni, halooo eeeehhhh! Shoga baada ya udambwiudambwi tuelekee kuleee kwenye kile kilichonifanya niwe na wewe kwenye kolamu hii! Najua maji ya barafu hayapikiwi chai lakini shoga ifike mahali tuelezane ukweli ati! Siyo umevimba macho kama papai lililoanza kubadilika rangi! Shuutuuu!

Leo nipo na nyie kina mama ambao kutwa kushinda kijiweni na kanga moja, utakuta mumeo akiondoka tu kwenda kazini huku nyuma ni kuwatega wanaume wa wenzio mwanzo mwisho! Jamaaani! Nikisema jambo namaanisha ati! Siku zote mate ya uzee hayana utamu na ukikutana na utamu basi ujue huyo bado kijana, uongo shoga? Basi mwenzako juzi nimepata meseji kutoka kwa baba mtu mzima, baba mwenye malalamiko kama yoteee! Mwenzangu kwanza anasema anajuuutaa hata kuishi uswahilini maana ndiko kumechangia mkewe kumbadilikia.

Anasema alimuoa mkewe miaka miwili iliyopita baada ya kupata naye mtoto mmoja! Waliishi maisha mazuri tu japo walipanga chumba na sebule uswahilini. Mkewe alianza kubadilika siku moja baada ya nyingine kwa kuanza kujiachia kihasara kila akienda kazini lengo likiwa kuwashika wapangaji na kutoka nao kimapenzi.

Siku aliyokuja kushtukia ni ile ambayo hakwenda kazini. Anasema siku hiyo alishinda ndani lakini kama ujuavyo tabia ya kubabuka ngozi usipoitibia lazima irudi tena! Mkewe akajisahau, kaamka asubuhi na kufanya usafi na kanga moja! Akasahau kabisa kama mumeo yupo akamtega jirani yake wa siku zote akamvutia chumbani na kuanza kuvunja zile amri.

Unaambiwa mumewe akagongewa hodi na majirani wapenda wema, majirani wachukia maovu! Majirani waliomchoka kama siyo kumtapika kabisa! Wakamng’ata sikio yule mumewe akang’atika! Acha waongozane hadi chumba kimoja cha yule mpangaji na kumfumania! Bibiye jicho likamganda kama msukule aliyemwagiwa unga mwili mzima! Hivi ninavyokwambia jamaa kamwaga mboga, kachukua watoto na kuanzisha maisha mapya peke yake!

Nikugeukie na wewe mwanamke mwenzangu mwenye tabia kama za mwanamke huyu! Tangu lini treni ikatembea kwenye lami! Unajua kabisa una mume kwa nini kujipitisha au kujivalisha kanga moja, inahu? Shuuuuutuuuuu!

Badilika basi, kukaa uswahili kusikufanye ukawa na tabia za kiswahili mwenzangu! Maisha ya sasa siyo ya kutegana, unaweza kuwatega watu wasiotegeka mwisho wa siku ukawa na matege, halooo eeeh siyo kama nacheka ukajua mazuri atu, mwenzenu limenifika hapa natamani hata kumtapika huyo mwanamke nikimuona. Kwa leo shoga naomba niishie hapa, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine tamu zaidi. Ni mimi Shangingi Mstaafu Anti Naa!

Comments are closed.