The House of Favourite Newspapers

True Memories Of My life -143

0

 

Wiki iliyopita niliishia pale nilipokuwa nikisisitiza kuwa tusichague rais atakayewekwa madarakani na mtandao pamoja na kuwakumbusha wazazi kupeleka watu wengi kwenye kupiga kura…nilisema katika sehemu ya hotuba yangu ingawa moyoni nilikuwa nikiwahofia Ukawa.

SASA ENDELEA…

Niliondoka ukumbini Don Bosco, Upanga ambapo mahafali ya Azania na Jangwani (Azajangwa) yalikuwa yakifanyika kwenye majira ya saa kumi hivi jioni, ndani ya gari nilikuwemo mimi wapwa zangu, Dk. James na Alex Mabula waliofuatana nami, James pamoja na kuwa daktari anapenda sana kuhamasisha watu, hivyo hupendelea kunifuata kila mahali ambako ninahutubia ili apate uzoefu wa kuongea mbele za watu, Alex aliniletea vitabu vya Siri Kumi za Mafanikio ambavyo niliamua kuwagawia wahitimu wote ili viwasaidie kuzifahamu mbinu za kufanikiwa katika maisha halisi, badala ya kutumia tu elimu ya darasani ambayo kwa kweli imeonekana kushidwa kuwasaidia wengi.

Mazungumzo ndani ya gari ambamo pia tulimpa lifti kijana mmoja aliyekuwa akielekea Mwenge, yalikuwa ni juu ya Ukawa na CCM na uchaguzi wa siku iliyofuata, sisi sote ndani ya gari tulijikuta mashabiki wa Chama Cha Mapinduzi, lakini wenye hofu kuhusu siku ya uchaguzi ambayo kwa hakika ilikuwa saa zisizozidi kumi kabla hatujaifikia.

Bendera za Ukawa zilikuwa nyingi mno barabarani, sijawahi kuona bendera nyingi kiasi hicho wakati wa kampeni kama kwenye uchaguzi wa mwaka 2015! Sitaki kusema uongo, sitaki unafiki, Chadema walitapakaza Jiji la Dar es Salaam kwa bendera nyingi mno kuliko CCM, asilimia kubwa ya bodaboda  na Bajaj zilikuwa na bendera za Chadema, kwa kweli roho iliniuma kupita kiasi.

Huko nyuma niliwahi kutengeneza stika nyingi za Magufuli nikawa nawalipa vijana wa Bajaj Sh. 15,000 ili zibandikwe kwenye Bajaj zao, walikusanya pesa yangu, wakazunguka nazo kwa siku chache kisha kuzibandua wakidai eti watu walikuwa wakiona Bajaj ina stika ya  CCM wanagoma kupanda, jambo ambalo nilikuja kulifanyia uchunguzi na kugundua lilikuwa ni uongo, ukweli ulikuwa ni kwamba Edward Lowassa na timu yake ya kampeni waliishawanasa waendesha bodaboda na Bajaj karibia wote nchini na kuwaweka upande wao.

“Tutashinda kweli?” niliwauliza vijana niliokuwa nao ndani ya gari baada ya kuona Bajaj moja iliyopita mbele yangu ikiwa na bendera kubwa ya Chadema.

“Tutashinda tu anko, wala usiwe na wasiwasi, Ukawa watoto wadogo hawajakomaa kukabidhiwa nchi!” aliongea Alex na kunitia moyo.

Ilivyoonekana ni kwamba familia yangu ilijua ni kiasi gani nilikuwa nimejitoa mhanga kwa ajili ya CCM, walikuwa wanaogopa kuniumiza moyo, najua walikuwepo vijana ndani ya familia yangu wapenzi wa Ukawa lakini hawakuweka hisia zao wazi wakijua wangeniumiza!  Kauli ya Alex kwamba tungeshinda ilinifanya nijiulize, kama alikuwa akiniambia ukweli au la.

Wiki chache kabla ya siku hiyo yalitokea mabishano kidogo na baadhi ya waandishi ofisini kwamba aidha Ukawa au CCM wangeshinda uchaguzi, tukafikia uamuzi wa kutoka hadi nje ya ofisi ambako watu wengi hupita wakitembea kwa miguu, tukakubaliana tuanze kusimamisha mtu mmoja baada ya mwingine na kumuuliza kama uchaguzi ungefanyika siku hiyo angemchagua nani, kati ya Lowassa na Magufuli, katika vijana kumi tuliowauliza, wawili tu ndiyo walisema wangemchagua Magufuli.

Hakika ilinitia hofu na kulazimika kuongeza nguvu ya mashambulizi kujaribu kubadilisha akili za watu hata kupitia kwenye ukurasa wangu wa Facebook ambako niliandika makala nyingi kuwaeleza watu juu ya John Pombe Magufuli niliyemfahamu ambaye nilikuwa na uhakika kabisa angewaletea Watanzania mabadiliko ya kweli, nilikutana na matusi mengi ambayo siwezi kuyaandika hapa, sikuvunjika moyo niliendelea kufanya ninachokiamini, nilikuwa vitani, hapakuwa na sababu ya kukata tamaa.

Ofisini nilifanya kazi zangu mpaka kumaliza, nikawaaga wafanyakazi wenzangu wakati giza linaanza kuingia nikiwatakia uchaguzi mwema, nikawakumbusha juu ya kufanya maamuzi sahihi ya kumchagua kiongozi ambaye angepeleka nchi yetu mbele, nikawasihi wasichague kwa chuki au kutumia historia bali wafanye maamuzi yatakayokuwa na maslahi kwa taifa kwa kumchagua mtu anayeaminika, mwenye sifa za kuongoza na mwadilifu wa kutosha.

Nyumbani kwangu siku hiyo sikuwa na maongezi mengi, nikaingia chumbani ambako niliendelea kufikiria juu ya siku iliyofuata, ambayo Watanzania wangefanya maamuzi, moyo wangu ulikuwa na wasiwasi sana kwa sababu Watanzania hasa wa mijini walikuwa wamechotwa sana na neno mabadiliko, kwao tafsiri ya mabadiliko ilikuwa ni kuiondoa CCM madarakani hata kama ilikuwa imefanya mambo mengi, ilimradi tu waingize chama kingine.

Nilimuomba Mungu katikati ya usiku azungumze na kila Mtanzania usiku huo na kumfanya auone ukweli kwa kuchagua kiongozi ambaye Mungu mwenyewe alimtaka, mwisho nikasema “nimefanya kila kilichowezekana ndani ya uwezo wangu, sasa namuachia Mungu, kama anamtaka Lowassa awe kiongozi wa taifa hili atakuwa na kama anamtaka Magufuli basi atakuwa!”

Sikufanya jambo lingine tena baada ya hapo, usingizi wangu ulikuwa ni wa mang’amung’amu na mpaka kulipokucha, mimi na mke wangu tukaondoka nyumbani kwenda kusalimia mgonjwa maana siku hiyo hapakuwa na ibada kanisani kwetu, tuliporejea tulikuta baadhi ya vijana wetu wamekwishaondoka kwenda kupiga kura, saa tisa alasiri ndipo nasi tukaondoka kwenda kwenye kituo cha kupigia kura tukiamini kwamba watu wangekuwa wamepungua kituoni. Hatukukuta watu wengi, tulipiga kura zetu, wote tukiwa tumekubaliana kumchagua Rais wa CCM, Mbunge wa CCM na Diwani wa CCM, tulisimamiana kuhakikisha hakuna usaliti, maana mke wangu ni Mchaga, ingawa namuamini kulikuwa na hisia zinanitembelea kichwani zikisema “mkeo ni wa Kaskazini asije aka…”

Ni utani ambao nilimtania mara kwa mara si kweli kwamba aliweza kufanya hivyo, baada ya kupiga kura tuliondoka kituoni kwenda nyumbani kwa mama yangu kumsalimia kwani siku hiyo tangu asubuhi hatukufanya hivyo na yeye huishi kilomita moja kutoka nyumbani kwangu, tulimkuta mama ameketi sebuleni akiwa na furaha na tukazungumza naye juu ya uchaguzi, akafurahi kwamba tulikuwa tumetimiza wajibu wetu.

Hatukukaa sana, tukarejea nyumbani, Jiji la Dar es Salaam lilikuwa kimya siku hiyo, hofu kwamba kama Ukawa wangeshindwa katika uchaguzi  huo lazima kungetokea vurugu ilikuwa ndani ya mioyo ya Watanzania wengi tukiwemo sisi! Siku chache kabla ya uchaguzi tulikaa chini kama mke na mume, baada ya kusikia rafiki zetu wengi walikuwa wanasafiri kwenda Dubai na Afrika Kusini kupumzika wakisubiri uchaguzi upite, kujadiliana kama na sisi tungechukua uamuzi huo.

“Eric utaondoka na nani umuache nani?” mke wangu aliniuliza.

“Hata sijui!”

Familia yangu ilikuwa kubwa sana jijini Dar es Salaam, hata kama ningeamua kuondoka nisingeweza kuwabeba wote, ningemchukua mke na watoto na mama, dada zangu je? Kaka zangu je? Binamu zangu je? Wapwa zangu je? Rafiki zangu je? Wafanyakazi wenzangu je? Kwa kweli uamuzi huo tuliuona si sahihi, tukaamua kubaki tukiomba Mungu aepushe balaa, hivyo tulivyorudi nyumbani siku hiyo kila mtu alikuwa akiendesha ibada mambo yaishe salama, ilifikia wakati tukawa tunasema “natamani kuona uchaguzi umeshapita, nchi imetulia na ni Krismasi!”

Ilionekana ni vigumu sana kuifikia Krismasi tukiwa salama kwa jinsi hali ilivyokuwa na mambo yaliyokuwa yakitamkwa na vijana wafuasi wa Ukawa mitaani, ilionekana kama vile vurugu kubwa zingetokea kama Ukawa wasingeshinda na Edward Lowassa kutangazwa mshindi.

Mimi na mke wangu tukamuamini Mungu tukisema, “historia ya nchi yetu na tabia za Watanzania si za watu wa vurugu kama nchi jirani, tutavuka, watu wamemuomba Mungu mno, hakuna baya litakalotokea.” Tukabaki na maneno haya huku tukisubiri matokeo.

Jiji lilikuwa tulivu mpaka matokeo yalipoanza kutangazwa saa 3 baadaye, yalianza ya ubunge na udiwani hapo ndipo tukaanza kusikia kelele mitaani, hasa maeneo yetu ya Tandale, vijana wakaanza kuingia mitaani wakiimba nyimbo za kusifia Ukawa na maneno ya “people’s power” yakawa yanasikika, mabomu yakaanza kupigwa mitaani usiku huo, wasiwasi na hofu ukaniingia, kichwani mwangu nikijiuliza kwa sababu nilishajiweka wazi kuwa shabiki wa CCM, angetokea mtu na kusema “twendeni kwa Shigongo” mimi na familia yangu tungekuwa hatarini.

Usiku mzima hatukulala, bahati mbaya umeme ulikatika, jenereta lilikuwa na tatizo ili kuliwasha lazima mtu ashuke chini jambo ambalo sikutaka kulifanya! Ikabidi nivumilie huku nikumuomba Mungu, moyoni mwangu nikiwa nimepanga kama tungeamka salama, ningehama kwanza nyumbani kwangu kwenda kuishi mahali pengine mpaka matokeo yakamilike, hali ilikuwa inatisha. Dalili za machafuko zilianza kuonekana.

“Udiwani na ubunge tu inakuwa hivi, je, Lowassa akitangazwa ameshindwa, itakuwaje?” nilimwambia mke wangu.

“Mungu atasimama.” Hilo ndilo lilikuwa jibu lake, hivyo ndivyo mke wangu alivyo, mtu wa kuchukulia vitu vikubwa na kuvifanya vionekane visivyotia hofu.

Leave A Reply