The House of Favourite Newspapers

True Memories Of My life -158

0

Wiki iliyopita niliishia pale ambapo Waziri Nape aliposema ipo sababu ya kuendelea kuwajali na kuwatunza watumishi wa umma au watu waliotumikia taifa kwa uzalendo pale wanapokutwa na matatizo maishani mwao, kila mtu aliyemuona Athuman kitandani siku hiyo akiwemo Mhariri wa Gazeti la Championi, Saleh Ally na kukumbuka alivyokuwa ‘handsome boy’ roho ilimuuma, binafsi nilijikuta nikitamka moyoni mwangu “kweli hujafa, hujaumbika! Mungu nisaidie.”

sasa endelea nayo…

Hapa duniani hatuishi kwa nguvu zetu, akili zetu wala mali zetu, ni kwa neema ya Mungu tu, ni baraka ambayo tumepewa ili kutimiza yale tuliyokusudia, nilipomwona Athuman Hamisi kitandani na kukumbuka alivyokuwa mchapakazi, hakika roho iliniuma, kichwani nikajiuliza mimi ni nani hasa mpaka niwe vile nilivyo?

Swali hilo lilizunguka kwa muda ndani ya kichwa changu, nikitafuta jibu ambalo lingeendana na swali, tulitoka na kuingia ndani ya gari, muda wote nikiwa kimya,  jambo lililowashangaza wenzangu wote tuliokuwa nao na hata walipojaribu kubadilisha maongezi, mimi bado niliendelea kubaki kimya.

Ndugu zangu, wengi wetu tunaishi maisha ya ujanjaujanja, tukiwa tumesahau kabisa kwamba lipo kusudi la kila mmoja wetu hapa duniani, nilichojifunza mimi binafsi na ambacho ningependa na wewe msomaji unayesoma hapa leo ujifunze kumcha Mungu kwa kutenda yale yaliyo mema siku zote, kwetu na kwa wengine wanaotunzunguka.

Unaweza ukaishi maisha mazuri na hata mabaya lakini jifunze kuishi maisha ya kumpendeza Mungu, siku zote unapokuwa na furaha, furahiana, unapokuwa na huzuni pia huzunika, hata mimi mwenyewe upo wakati wa kuishi maisha ya furaha na huzuni, pia tofauti na watu wengi wanavyofikiria kwamba mimi huishi maisha ya furaha tu, jambo ambalo si kweli.

Ninaumia na kufurahi kama ilivyo kwa watu wengine. Jambo moja ambalo nimejifunza ni kuishi maisha ya kumpendeza Mungu katika hali zote, hatimaye gari likaendeshwa na kufika ofisini ambako nilishuka na kuingia ofisini kwangu kwa muda nikiyatafakari maisha na namna dunia ilivyoweza kumfanya mtu kutoka katika hali moja kwenda nyingine.

Nilimfikiria sana rafiki yangu, Athuman Hamisi, kijana mchapakazi aliyejitoa kutumikia taifa kwa moyo mmoja lakini leo alikuwa kitandani akiwa hawezi tena kufanya chochote, akihudumiwa kila kitu na familia yake, akiwa mtu wa kuomba kila kitu na si kutafuta kama ilivyokuwa zamani.

Ndugu zangu, ndiyo maana nasema yatupasa kuishi maisha kwa hali zote, kikubwa ni kumcha Mungu. Nilikaa ndani ya ofisi yangu, mambo mbalimbali yakiendelea kupita akilini mwangu, hatimaye muda wa kwenda nyumbani ukawadia, nikanyanyuka na kuondoka.

Kama kawaida yangu, baada ya kufika nyumbani kwangu ni kupata muda kidogo wa kukaa na watoto wangu nikizungumza nao kuhusu maisha na nilipomaliza niliwasaidia kufanya kazi zao za shule ndipo tukala, kusali na kwenda vyumbani kwetu kulala.

Baada ya maandalizi yote, nilipanda kitandani lakini ghafla usingizi ukinimendea simu yangu iliita, nikanyanyuka kisha kusogea na kuichukua, nilipotupa macho kwenye kioo niliifahamu namba ya mtu aliyenipigia, alikuwa ni Hoyce Temu, rafiki yangu wa siku nyingi, moyoni nikahisi tatizo kwani haikuwa kawaida yake kunipigia simu usiku kama ule.

Nikaiweka sikioni kisha kuanza kuongea sauti yake tu ilinipa ishara kwamba hakuwa sawa, kwani kwa jinsi tulivyozoeana na Hoyce, muda wote alikuwa ni mtu wa utani lakini siku hiyo aliongea kama mtu aliyekuwa na tatizo fulani. Nikamsalimia  naye akajibu.

Kwa sauti ya upole kabisa, Hoyce akaanza kunieleza tatizo alilokuwa nalo, akidai kwamba kuna msichana anamtukana  kupitia mitandao ya kijamii, akaendelea mbele na kunieleza kila kitu kwa masikitiko makubwa, nikamwonea huruma na kwa sababu mimi binafsi sisomi wala kufuatilia mitandao ya kijamii, nilijua ni kiasi gani Hoyce aliumizwa.

Niliongea naye kwa muda mrefu kidogo nikimkumbusha kwamba yeye ni nani katika jamii iliyomzunguka, kwa umaarufu wa Hoyce Temu hakutakiwa kabisa kujibishana na msichana (jina linahifadhiwa) ambaye alifanya hivyo ili kutafuta umaarufu wa  kutoka kwenye magazeti.

Niliongea na Hoyce mambo mengi nikimsihi kuachana naye lakini kwake ilionekana kuwa ngumu, alishadhamiria kuchukua hatua nyingine kwani alikuwa ameumia mno, nikajaribu kumtolea mfano na kumweleza kwamba hata mimi mwenyewe nilishawahi kukutwa na jambo ambalo limemkuta la kutukanwa kwenye mitandao ya kijamii na mmoja wa watu waliofanya hivyo alikuwa ni huyohuyo msichana, nikamtaka Hoyce amsamehe na kuachana naye kwani kuendelea kulumbana naye ni kujipotezea heshima aliyoijenga kwa muda mrefu katika jamii lakini aliniambia kwamba ilikuwa ni lazima ahakikishe jambo hili linafika mbele zaidi, ikiwezekana kwenye mkono wa sheria, nikamuahidi kumsaidia msaada wowote ambao angeuhitaji.

Katika maongezi yangu na Hoyce alinigusia pia kwamba msichana huyo alikuwa akinitukana kwa kuniita mlokole feki, jambo ambalo liliniumiza moyo, binafsi nikaapa kutokugombana na msichana huyo kwani kufanya hivyo kungenivunjia heshima niliyonayo, nikafikiria pia jamii iliyonizunguka kuanza kulumbana na msichana jamii isingenielewa, ingechukulia kitendo hicho kama uonevu kwa sababu ni mwanamke. Nikaona hakukuwa na sababu yoyote, moyoni mwangu nikamsaheme ili kuruhusu milango mingine ya baraka kufunguka kwani katika maandiko ya Kitabu Kitakatifu cha Biblia yanatuambia tujifunze kusamehe, hivyo ndivyo nilivyofanya.

 Nikageuka na kuangalia mahali nilipolala, mahali nilipotoka, nilipokuwa, furaha niliyokuwa nayo na jinsi Mungu alivyokuwa amenibariki, nikajikuta  nikisema. “Ulokole wangu feki au si feki anafahamu Mungu peke yake.” Hapohapo nikajikuta nikisahau kila kitu na kuendelea kuyafurahia maisha.

Baada ya kukata simu na kutafakari kwa kina mambo yote ambayo Hoyce alikuwa amenieleza, nilimgeukia mke wangu na kuanza kumsimulia kila kitu, naye pia akamwonea huruma Hoyce akiniomba kumsaidia kadiri ya uwezo wangu na ikiwezekana kuongea naye mara kwa mara ili kumfariji kwani alikuwa katika kipindi kigumu.

Nilimweleza wazi mke wangu kwamba ugomvi aliokuwa nao Hoyce kutoka kwa msichana huyo nami pia ilishatokea lakini kwa wakati huo kwangu haukuwa na maana na tayari nilishamsamehe kwa moyo wangu wote nikiyafurahia maisha ambayo Mungu alinipa na familia yangu. Tukalala.

Maisha yakaendelea, nami nikichapa kazi kama kawaida huku nikitimiza wajibu wa kuwa baba bora kwa watoto wangu. Kuwapeleka shule asubuhi kisha jioni niliporejea kuangalia madaftari yao na kusaidia pale walipohitaji msaada wangu.

Ndugu zangu, jambo moja naomba nisema tu hapa, kwa yeyote anayesoma hapa leo ni kwamba ili ufanikiwe hapa duniani katika kila jambo unalolifanya maishani mwako ni lazima ujifunze kusamehe na kusahau ili kufungua milango ya baraka.

Siku mbili baadaye, nilipokea simu kutoka kwa Waziri Mkuu akinihitaji kufika ofisini kwake mimi na wenzangu ambao tulifanya kazi ya kusaidia kutafuta misaada mbalimbali kwa lengo la kusaidia jimboni kwake, Ruangwa ambako kulipatwa na mafuriko yaliyosababisha wananchi wa jimbo lake kukosa huduma muhimu.

Nawashukuru sana wale wote waliojitolea kwa namna moja au nyingine, kusaidia zoezi hili na hatimaye kukamilika, wapo waliojitolea mabati, vitenge, mbegu, misumari, maji, chakula n.k. Mungu awabariki na muendelee kuwa na moyo  huohuo, ahsanteni sana.

Ofisini tukiwa kama kamati, tuliongea mambo mengi na mpangilio mzima wa safari kwenda Ruangwa, Lindi kwa ajili ya kukabidhi misaada iliyopatikana, binafsi katika maisha yangu, sikuwahi kwenda Lindi lakini sasa ilikuwa ni lazima twende ili kumaliza kazi tuliyoianzisha.

Baada ya kikao kilichofanyika tarehe 26 Februari, mwaka huu kwisha, sote na wanakamati wenzangu tuliondoka mimi nikiwa na hofu ya safari lakini nikitamani kwenda huko, nilirejea nyumbani na kumwambia mke wangu kwamba ilikuwa ni lazima nisafiri kwenda Lindi siku ya tarehe 27 kwa ajili ya kwenda kukamilisha kazi tuliyoianza, akaniunga mkono na kunitakia kila la kheri, jioni ya siku hiyo tulilala lakini kichwani nikifikiria safari tu na si kitu kingine, nikajikuta nikisema Mungu atakuwa pamoja nami mwanzo hadi mwisho.

Siku ya tarehe 27, niliamka asubuhi, nikaagana na mke na watoto wangu na kuelekea ofisini kukamilisha ratiba zangu, tayari kwa safari ambayo ilitarajiwa kuanza saa tano asubuhi nikiwa na dereva wangu, Nyange, taratibu tukaanza kuchanja mbunga ndani ya gari, tukiwa wawili tu, safari ilikuwa ndefu mno tukipita Ikwiriri, Rufiji, Nangurukuru na kuingia katika mapori mengi makubwa, tukiwa katikati ya pori, macho yangu yalimwona kijana mmoja mrefu aliyevalia Kimasai, pembeni akiwa na mtoto mdogo mzuri  wa kike, nikasikia sauti ikiniambia kijana yule hakuwa Mmasai ni lazima atakuwa Msukuma, hapohapo nikamwambia dereva wangu asimame kisha kurudi nyuma ili niongee na kijana yule.

Gari liliposimama haraka nikashuka na kumwita mtoto, nikitaka kuongea naye lakini akakimbia ndipo kaka yake akasogea na kuanza kuzungumza naye nikiwauliza walitokea wapi na kwa nini walikuwa pale? Alinipa habari ndefu sana, akaenda mbele zaidi na kunieleza walikuwa katika pori hilo miaka mingi mno wakiwa na mifugo yao na wao kwa kabila walikuwa Wasukuma, nikajisikia huruma kupindukia.

Muda wote huo, wakati nikiongea na kijana huyo macho yangu yalikuwa kwa mtoto mdogo, msichana mzuri kupindukia, akiteseka porini, nikahitaji kumsaidia kwa kusoma na nilipomuuliza anataka kuwa nani akikua, alinipa jibu moja tu, “nikikikua nataka kuolewa” unataka kuolewa? Akajibu ndiyo, nikamwambia mimi nataka usome, uje kuwa daktari au injinia na nataka nikusaidie usome, akacheka.

Nikakumbuka mfuko wetu wa E&V Foundation ambao tuliuanzisha mimi na mke wangu kwa ajili ya kusaidia watoto wasiojiweza kupata elimu. Nikamwambia Mungu nataka kumsomesha mtoto huyu nimwone akiwa daktari, injinia au mtu mkubwa maishani mwake. Nilikwenda mbele zaidi na kuwauliza majina yao, mvulana akaniambia anaitwa Lugola na msichana anaitwa Ngolo.

Nikiwa hapo nikatoa shilingi elfu kumi na kumpa mtoto lakini akaikataa akidai kwamba asingeweza kuitumia kwani porini hapo hapakuwa na duka lolote, nikambembeleza kwa muda akakataa, mwisho nikaamua kumpa kijana ambaye aliipokea.

Nikachukua karatasi na kuandika namba yangu ya simu kisha nikampa kijana huyo na kumtaka awaeleze wazazi juu yangu na nia yangu ya kumsaidia Ngolo ili asome na kuwa mtu fulani maishani mwake. Nilipomwangalia huyo mtoto nilikumbuka maisha yangu ya utotoni, nikajiona mwenye bahati kubwa nikiwa mtoto wa Msukuma pia.

Nikawafikiria pia watoto wangu na shule wanazosoma, moyo ukajawa na huruma na kujisikia nilikuwa na la kufanya kubadili maisha ya Ngolo, hakika nilielewa sababu ya mimi kusafiri kwenda Lindi haikuwa kupeleka misaada Ruangwa bali nilikwenda kumfuata Ngolo. Nikamsihi kijana yule ahakikishe  anampa mzazi namba yangu na anipigie kama angekuwa na wasiwasi basi angesafiri kwanza yeye kuja Dar kujionea mahali ambapo mtoto wake angekwenda kuishi na kusoma!

Baada ya kumaliza mazungumzo yangu na Lugola na Ngolo niliingia ndani ya gari kuendelea na safari, tukiondoka Nangurukuru  kuelekea Ruangwa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave A Reply