The House of Favourite Newspapers

True Memories Of My life

0

Wiki iliyopita niliishia pale nilipokuwa nikielezea namna nilivyojisikia furaha kwa mara nyingine tena nilimfanya mwanadamu mwenzangu aliyekuwa akiteseka acheke.

SASA ENDELEA…

Hauhitaji kuwa mwanasiasa, tajiri au mtu mwenye cheo na ushawishi mkubwa sana ili uweze kusaidia jamii yako, la hasha! Unachohitaji ni moyo na tabia ya kuwafikiria wengine ambao mimi naamini kila mwanadamu anayo kama tu atakuwa tayari kushirikiana na wenzake baraka ambazo Mungu amempa.

Watu wengi duniani walikufa au wanaendelea kufa bila kuacha alama kwa sababu tu walisubiri wapate cheo, wawe wanasiasa, watajirike au wawe na ushawishi mkubwa kwenye jamii ndiyo waanze kunyanyuka na kusaidia wengine! Si hivyo, anza na ulichonacho, kama una muda wa kutosha, tembelea wagonjwa hospitali kuwapa pole, kama unakula na kubakiza, chukua sehemu ya chakula unachobakiza na kuwapa wanaolala na njaa.

Kila siku  ukiamka asubuhi, jiulize leo nitamsaidia nani?  Badala ya leo nitasaidiwa na nani? Watu wengi walioacha alama duniani kama Yesu, Mtume Muhammad (SAW), Nelson Mandela, Mahatma Ghandi na wengi wengineo waliwafikiria wengine zaidi kabla hawajajifikiria wao, mtu yeyote anayefanya hivi hapa duniani ana nafasi kubwa sana ya kufanikiwa kwani atakuwa tofauti na watu wengi, maana binadamu tumeumbwa na nafsi ya kujifikiria sisi kwanza kabla ya wengine.

Lakini nikumbushe kitu kimoja, siamini kabisa kwamba hapa duniani unaweza kufilisika kwa sababu ulikuwa ukisaidia watu wengine, badala yake naamini mtu anayesaidia sana watu wengine, Mungu humbariki ili aweze kuendelea kutumika kama bomba au njia ya Mungu kupitishia misaada yake.

Nilijifunza jambo hili kwa mzee Mengi, ambaye kwa miaka mingi nilimshuhudia akitumia sehemu ya utajiri wake kusaidia watu masikini, siku nilipokutana naye aliniambia; ‘mwanangu Eric, binadamu ni kama bomba la maji, uzima wake hutegemea maji yanayopita ndani yake, yakiacha kupita bomba huota kutu na baadaye kutoboka, hivyo ni vyema kuendelea kutumiwa na Mungu kama bomba la kupitisha baraka za watu wengine!

Haya ndiyo yamekuwa maisha yangu, siku zote nasikiliza sauti ya Mungu kila ninapokutana na mtu mwenye shida, sitaki watu wanifanye  mjinga, mara zote husikiliza sauti inayotoka ndani yangu nami huitii sauti hiyo na kutekeleza kile Mungu alichosema.

Sifichi, wala sijigambi, nalisema hili ili watu wote waelewe na wale ambao hawataki kushirikisha watu wengine kwenye baraka zao wabadilike, Mungu amenibariki sana maishani mwangu, si kwa sababu nina akili nyingi, la hasha! Ni kwa sababu ya neema yake na njia rahisi ya kupata neema ya Mungu ni kumtii pale anapozungumza na wewe kwa sauti ya ndani,  hii ni siri kubwa sana ya mafanikio katika maisha ya mwanadamu, matajiri wengi wanaifahamu.

Nilishindwa kujizuia siku hiyo asubuhi nilipoamka na kumkuta binti mdogo Sikujua Mjalifu akiwa ameketi mbele ya nyumba yangu, kwenye maumivu makali! Nilimwonea huruma, nikafikiri; ‘jambo hili linaweza kunipata hata mimi na familia yangu’, hakika nilijisikia kupendelewa, moyoni nikaisikia sauti iliyoniamrisha nimsaidie.

Sasa hebu niambie, ni furaha kiasi gani niliyonayo ndani ya nafsi yangu pale  ninapomwona Sikujua akitabasamu tena? Watu walimdharau na kumpuuza, akajisikia mnyonge asiye na maana lakini leo hii amefanyiwa upasuaji na amepona, si jambo jema? Hakika hata huko mbinguni Mungu anafurahi, kwamba mwanangu Shigongo, pamoja na kwamba hajatimia, amefanya jambo moja jema la kutumia kile nilichombariki kuboresha maisha ya mtu mwingine.

Hakika nina furaha kubwa mno, hivi ninavyoandika kumbukumbu hii ya leo, Sikujua  ameruhusiwa kutoka hospitalini na tayari yupo kijijini kwetu, Bupandwamhela, akisubiri kurejea hospitalini kwa ajili ya kutolewa nyuzi, akisubiri kufanyiwa upasuaji mwingine tena baadaye.

Nachukua nafasi hii kutoka ndani kabisa ya moyo wangu na kwa niaba ya mfuko wa  Veneranda&Shigongo Education Fund, kuwashukuru madaktari wa Hospitali ya Bugando wakiongozwa na Dk Gustave Bunane na Dk Gitti waliofanya upasuaji wa mtoto huyu kutoka familia ya masikini wakijitolea kwa lengo la kumsaidia, Mungu awabariki sana.

Nawashukuru pia wauguzi wa hospitali hiyo ya Bugando kwa kazi njema waliyoifanya, sina cha kuwalipa, Mungu mwenyewe wa mbinguni anayeishi ndani ya mioyo yetu atawafungulia milango ya baraka, Amina.

Nikiwa katikati ya furaha hii, kama mjuavyo maisha hayana furaha ya  moja kwa moja, kuna kupanda na kushuka, kupata na kukosa, kulia na kucheka na mengineyo! Hakuna mwanadamu mwenye kufurahi siku zote, ili mwanadamu akamilike hata ungekuwa bilionea kama Bill Gates, kuna siku za kulia na kucheka.

Napokea simu kutoka kwa mtu aitwaye Dk Mponzi, bahati mbaya  jina lake la mwanzo nimelisahau, huyu ni miongoni mwa wafanyabiashara wa Kitanzania wenye mafanikio makubwa ambao wanafanya biashara ambazo huko nyuma tulizoea kuona zikifanywa na wazungu.

“Eric mzima?”

“Mzima Dk Mponzi!”

“Tuna semina pale kanisani kwetu ya mambo ya ujasiriamali, tungependa uje uongee na akina mama ili uwasaidie kujitambua na waweze kupiga hatua maishani mwao.”

“Haina tatizo daktari!”

“Basi mama Lwakatare atakupigia simu ili mpange vizuri!”

“Sawa.”

Nilifahamiana na Dk Mponzi kwenye semina za vijana wa GWT, kundi la uimbaji linaongozwa na Emmanuel Mabisa, huko nyuma waliitwa Glorious Celebration, ambazo zilikuwa zikifanyika kila siku ya Jumapili kwenye kituo cha Mafuta cha Victoria jijini Dar es Salaam ambapo mimi nilikuwa mzungumzaji mkuu kila wiki, siku moja Dk Mponzi alialikwa kuzungumza pamoja nami juu ya mafanikio yake ili vijana wapate cha kujifunza, hapo ndipo tulipokutana na kufahamiana.

Dk Mponzi alitaka niongee katikati ya wiki lakini nilipoongea na mama Lwakatare, yeye alitaka nikazungumze siku ya Jumapili kwenye ibada kuu, kwa kweli nilifurahi, maana kwa muda mrefu sana nilikuwa nimetamani kuzungumza na waumini wa Kanisa  la Mlima wa Moto lakini nilikuwa sijui jinsi ya kuingia mahali pale, hatimaye Mungu akawa amefungua njia.

Siku ya Ijumaa nikiwa nimejiandaa vizuri, nikisubiri Jumapili ifike, nilikuwa ofisini asubuhi nasoma magazeti kabla ya kuanza kazi, habari niliyoisoma kwenye moja ya magazeti  hayo ilinishtua; HELIKOPTA ILIKUWA IMEANGUKA, DEO FILIKUNJOMBE, MBUNGE  JEMBE WA LUDEWA ALIKUWA AKIHOFIWA KUFA! Moyo wangu ukapiga “paaa” na kujikuta nikisema “Huu ni uongo, Deo? Afe? Haiwezekani!” nilitamka maneno hayo moyo wangu ukiingiwa na huzuni.

Leave A Reply