The House of Favourite Newspapers

True Memories Of My life – 44

0

Wiki iliyopita niliishia pale nilielezea jinsi Watanzania wengi walivyoridhika na kuukubali uongozi wa Rais Maguli pamoja na nchi jirani ikiwemo Kenya ambapo wananchi wake walifikia mahali kusema wanahitaji kiongozi wa aina hiyo angalau kwa mwezi mmoja tu kupambana na ufisadi uliokuwa umekithiri nchini humo.
SASA ENDELEA…

Ujio wa Dk. John Pombe Magufuli na utendaji wake wa kazi ndani ya siku chini ya hamsini, ulianza kufanya mtangulizi wake, Jakaya Mrisho Kikwete aonekane kama hakufanya kazi, jambo ambalo mimi napingana nalo kabisa na hapa ninaomba niseme yaliyomo moyoni mwangu bila woga wala hofu.

Viongozi hawa wawili kwa kumbukumbu zangu wanaamini katika mitindo ya aina mbili tofauti ya uongozi, mmoja (Jakaya Mrisho Kikwete) anaamini katika filosofia ya kubadilisha mambo taratibu akitumia kusihi zaidi (persuasion) na mwenzake (John Pombe Magufuli) ni muumini wa filosofia ya matokeo ya haraka hata kama ikibidi kulazimisha (compulsion).

Mitindo hii miwili ya uongozi ina faida na hasara zake, katika mtindo wa kwanza huwa mtangulizi Jakaya Mrisho Kikwete ambapo kusihi zaidi ndiyo hutumika katika kuongoza watu badala ya nguvu, viongozi walio chini ya mkuu watampenda na kumfurahia mkuu wao kwani hushirikishwa katika kufanya maamuzi yote, tatizo la mtindo huu ni pale ambapo viongozi watamchukulia mkuu wao kama rafiki au kwa lugha ya kisasa “mshikaji” na kuanza kufanya kazi kwa mazoea.

Jambo hili linapotokea katika mtindo huu wa uongozi, yaani ‘urafiki’ na ‘kusihiana’ kunapozidi, mambo huwa hayaendi, malengo huwa hayatimii, mwisho wa siku walio wengi yaani wanaoongozwa (wananchi) huishia kumchukia kiongozi mkuu na kwa sababu wao ndiyo wafanya maamuzi, mwisho wa siku kwenye boksi la kura, humuadhibu kiongozi mkuu ambaye alifurahia kupendwa na viongozi wa kati akasahau kwamba mwisho wa siku angeadhibiwa na wananchi kwenye boksi la kura.

Katika mtindo wa pili ambao mimi naona Rais John Pombe Magufuli anautumia, wa kulazimisha mambo yatokee hata kama watu hawataki (compulsion) viongozi hulazimishwa kufanya kazi na kutimiza lengo, asiyefanya hivyo huondolewa madarakani bila kusubiri! Mtindo huu wa uongozi unazifaa zaidi nchi za Afrika ambazo watu wake walitawaliwa na wakoloni na kuzoea kusimamiwa kufanya kazi kinyampara.

Akili ya kusimamiwa na kulazimishwa kufanya vitu bado haijafutika kwenye akili za Waafrika ingawa wakoloni walishaondoka, tumekuwa tukirithishana kizazi hata kizazi, ingawa nafuu inapatikana kidogo tunavyozidi kwenda mbele! Nchi kama Rwanda ambayo leo hii inasifika Afrika, imetumia mtindo huo wa uongozi kufika hapo ilipo.

Tatizo kubwa la aina hii ya uongozi ni kiongozi mkuu kuchukiwa na watu waliomzunguka, ambao wengi wao walizoea mtindo wa uongozi wa kirafiki badala ya kusukumwa kwa nguvu! Watamwona kiongozi mpya kama mtu anayetaka kuwaletea utaratibu ambao wao hawakuuzoea, hivyo baadhi wataanza kuweka “kizuizi” au kufanya migomo ya ndani ya mioyo (resistance)

Kiongozi yeyote duniani anayetaka kupendwa na watu anaowaongoza anashauriwa kutumia njia ya kwanza (persuasion) lakini kiongozi anayetaka kuona mabadiliko yanatokea ni vizuri akatumia njia ya pili (compulsion) lakini ahakikishe anajiimarishia ulinzi na mfumo mzima wa Usalama wa Taifa kwa sababu atakuwa na maadui wengi sana ndani ya mfumo watakaokuwa wanamchekea mdomoni lakini mioyoni mwao wakifikiria kumwondoa.

Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete amefanya mambo mengi mazuri ambayo yatakumbukwa katika nchi yetu, sihitaji kuyataja hapa yote lakini wote tunafahamu kuwa nchi yetu imeunganishwa kwa barabara, umeme upo mpaka vijijini, shule za sekondari zimesogea mpaka kwenye kata, huduma za afya zimeboreka hata kama hazijafikia kiwango kilichotakiwa.

Mfumo wake wa uongozi wa kusihi, kuvumilia ndiyo ambao naweza kusema kwamba uliwapa nafasi watu wabaya ndani ya serikali yake kufanya mambo yasiyostahili, mwisho wa siku alipokuja John Pombe Magufuli na mtindo wake wa kulazimisha (compulsion) mambo yatokee, kila mtu amelazimishwa kufanya kazi kama alikuwa mvivu, kuwa mwadilifu kama alikuwa fisadi nk.

Tofauti hii ya mtindo wa uongozi ndiyo imewafanya Watanzania waone kumbe wakilazimishwa, wakisukumwa wanaweza kufanya kazi na kubadili hatima ya nchi yao, hiki ndicho kilichokuwa kinatakiwa kufanyika katika awamu zote, kuwalazimisha watu kufanya mambo ya manufaa kwao hata kama hawataki! Hivi ndivyo nchi hii inavyotakiwa kupelekwa, mwisho wa siku watu waliokuwa wakisukumwa wakiwa wamekasirika watakapoona maisha yao yamekuwa bora, watamsifia waliyemwita “dikteta” na hata kufikia uamuzi wa kubadilisha Katiba ili aongezewe muda wa kutawala.

Rais Kagame wa Rwanda, kwa sababu ya kutumia mtindo wa kuwalazimisha watu (compulsion) aliitwa dikteta na nchi za Magharibi, lakini kwa sababu wananchi wanaona mambo yanatokea, mabadiliko na maendeleo yanakuja, wamefikia uamuzi wa kupiga kura kubadili Katiba ili Rais Kagame aendelee kutawala Rwanda na hakuna atakayepinga hilo kama wananchi wa nchi hiyo wamelitamka.

Kumbukumbu zangu zinanionesha kuwa niliposema wakati ule kwamba Dk. John Pombe Magufuli ndiye alifaa kuwa rais wa taifa hili na si Edward Lowassa, uamuzi wa kijasiri kabisa kufanywa na mfanyabiashara ambaye kama maneno yake yasingetimia angepata madhara, nilitukanwa sana mitandaoni, watu wakasema nilikuwa najipendekeza kwa CCM, leo hii Dk. John Pombe Magufuli anapoonekana kutimiza matarajio ya Watanzania wengi mpaka wapinzani, moyo wangu unafarijika.

Leo nataka niseme tena maneno mazito na magumu, ambayo yanaweza yakanifanya nitukanwe na Watanzania wenzangu lakini sitaogopa wala kusita kusema kile ninachokiamini; KAMA DK. JOHN POMBE MAGUFULI ATAONGOZA MIAKA KUMI KWA MTINDO WAKE HUU WA COMPULSION NA NCHI HII IKAPIGA HATUA, WATANZANIA MWAKA 2025 WATAPIGA KURA YA KUOMBA WABADILISHE KATIBA KUMPA NAFASI YA KUTAWALA KWA MIAKA MINGINE MITANO ILI AMALIZIE KAZI AMBAZO ATAKUWA AMEZIBAKIZA, KUMBUKENI MANENO HAYA NA IPO SIKU MTAKUJA KUYAWEKEA MUHURI.

Nikiwa katika kipindi hicho cha kushuhudia utendaji wa Rais Dk. John Pombe Magufuli na moyo wangu kufurahi, ghafla nikapokea habari za kusikitisha kwamba mpiganaji wangu, mwandishi wa habari za uchunguzi ofisini kwetu, Pacha wa Makongoro Oging’ kikazi, Haruni Sanchawa alikuwa mgonjwa, mfanyakazi mwenzake ambaye ni mhasibu alikuwa amempeleka Hospitali ya Amana.

Taarifa zilizonifikia tena baadaye ni Sanchawa kupimwa damu na kukutwa ilikuwa imeshuka ghafla mpaka gramu 4, ambazo kwa asilimia ni sawa na ishirini na nane! Habari hizo zilimshtua kila mtu ofisini sababu Sanchawa alikuwa kazini akiendelea na majukumu yake kama kawaida siku chache kabla ingawa kweli alikuwa dhaifu na wengi walidhani ni kwa sababu hakuwa mtu wa kupenda kula chakula mchana.

Nilichokifanya ni kumpigia simu rafiki yangu, Dk. Meshack Shimwela, ambaye ni Mkuu wa Hospitali ya Amana na kumwomba atusaidie kumhudumia Sanchawa, Dk. Shimwela aliahidi kulifanya jambo hilo na vipimo vikafanyika kisha Sanchawa kuanza kuwekewa damu! Siku iliyofuata usiku nilikwenda Hospitali ya Amana kumwona Sanchawa, ilikuwa kazi kidogo kumfikia kwa sababu muda wa kuona wagonjwa ulishakwisha lakini kwa msaada wa daktari mmoja, nilifika kitandani na kumwona Sanchawa.
“Karibu sana Mkurugenzi!”

“Ahsante unaendeleaje Haruni?”
“Niko vizuri kabisa ila tu huu mpira ndiyo unanisumbua!”
Ulikuwa ni mpira wa kukojolea aliokuwa amewekewa, ikabidi nimtafute muuguzi mmoja na kuzungumza naye wakakubali kuuondoa kwa sababu alikuwa na uwezo wa kwenda msalani mwenyewe! Niliongea mengi na Sanchawa, baada ya hapo, ninachoweza kukumbuka ni kwamba baadaye aligundua simu yake ilikuwa haionekani, akaanza kupekua kila mahali akidai inawezekana mgonjwa aliyekuwa jirani yake ameichukua.

“Hapana Haruni, haiwezekani akaichukua!”
“Nilikuwa nimesinzia mkurugenzi.”
“Hapana, fuatilia vizuri pengine ndugu zako wamekutunzia!”

Baadaye tulisali pamoja na nikaondoka nikimuacha Sanchawa apumzike, siku iliyofuata nilisikia kuwa simu yake ilipatikana, mjomba wake alikuwa ameitunza baada ya kumkuta amesinzia kitandani. Hali ya Sanchawa siku chache baadaye akiwa bado yuko Hospitali ya Amana ilibadilika ghafla ikalazimika ahamishiwe Hospitali ya Taifa Muhimbili Kitengo cha Wagonjwa wa Dharura (Emergency)

Nakumbuka ilikuwa ni siku ya kazi nyingi sana ofisini, sikuweza kuondoka mara moja kwenda Muhimbili lakini baadhi ya viongozi wenzangu walikwenda Hospitali ya Muhimbili kufuatilia, mchana kama saa nane hivi taarifa zilitufikia ofisini, Sanchawa alikuwa amefariki dunia akiwa Muhimbili! Dah! Lilikuwa ni pigo jingine tena kwangu ikiwa ni miezi kadhaa tu tangu nimpoteze dereva wetu mahiri, Robert Tillya.

“Msiwaeleze kwanza wafanyakazi, mtavuruga kabisa kila kitu, acheni wamalize kazi zao ndipo muwape taarifa hizo jioni, wakati huo ninyi endeleeni kushirikiana na familia ya Sanchawa katika suala zima la msiba” nilimwambia Richard Manyota, Mhariri Mtendaji wa Global Publishers alipokuja ofisini kwangu kunipa taarifa hizo.

Leave A Reply