The House of Favourite Newspapers

True Memories Of My life – 45

0

Wiki iliyopita niliishia pale nilipomwambia Mhariri Mtendaji wa kampuni yetu Richard Manyota asiwaeleze wafanyakazi wenzetu juu ya kufariki kwa mwandishi Haruni Sanchawa SASA ENDELEA…

Ingawa tulikubaliana na Mhariri Mtendaji kuwa taarifa za msiba wa Haruni Sanchawa zitangazwe jioni kazi zikimalizika kuepusha mshtuko ambao ungejitokeza na kusababisha watu kushindwa kufanya kazi, wakati naondoka ofisini majira ya saa tisa alasiri kuelekea Muhimbili ambako mwili wa Sanchawa ulikuwa umehifadhiwa, nyuma ya ofisi nilimkuta msaidizi wangu wa kiofisi Mariam Issa Kilukile amesimama akiwa ameegemea ukuta, machozi yakimtoka.
“Mariam vipi?”

“Moyo wangu unaniuma sana!”
“Kwa nini? Hujala? Huna mwekundu?” niliongea kwa utani kwani nimezoea sana kutaniana naye, mara nyingi nikimuuliza “huna mwekundu” hunijibu “sina” hii humaanisha hana fedha, kama mfukoni nina elfu kumi basi humpa.

Siku hiyo Mariam hakujibu swali langu ambalo mara nyingi hujibiwa kwa haraka tena akiwa na tabasamu, moyoni nikajua siri ya kifo cha Sanchawa imeshavuja, nikamsogelea na kumkumbatia huku nikimfariji kwa kumwambia asilie sana kwani Sanchawa alikuwa mahali pazuri baada ya kukamilisha kazi yake.

“Najua mkurugenzi lakini Sanchawa alikuwa muhimu sana kwangu, mdogo wangu aliwahi kuwekwa mahabusu, Sanchawa alijitolea nikahangaika naye polisi mpaka akatoka, naumia!” aliendelea kuongea machozi yakimbubujika.

Kwa sababu nilikuwa na haraka ya kuelekea Muhimbili, nilichokifanya ni kufungua mlango wa ofisi nikamwita mhasibu wetu Shamim Mshana na kumwomba aendelee kumfariji Mariam na ahakikishe taarifa hiyo haisambai ofisini na kuvuruga utendaji wa kazi, Shamim alikubaliana nami, nikamwacha akiongea na Mariam, nikiingia ndani ya gari kuelekea Muhimbili kuonana na ndugu wa Sanchawa.

Njiani nilikutana na magari ya ofisi, wakaniwashia taa, nikatoka barabarani na kuegesha pembeni wakaja mpaka mahali nilipokuwa na kunieleza kwamba mwili wa Sanchawa ulikuwa umehifadhiwa chumba cha maiti vizuri na ndugu zake tayari walishaondoka kuelekea nyumbani kwa mjomba wake Kitunda ambako msiba na mipango ya mazishi ingeendelea, sikuona sababu ya kuelekea Muhimbili tena nikageuza kurudi ofisini.

Ofisi ilisimamia msiba wote wa Sanchawa ikiwa ni pamoja na kumsafirisha kwenda kwao Serengeti mkoani Mara, nilikuwepo Kitunda wakati wa kuuga mwili wake, roho ikaniuma sana nilipomwona Sanchawa amelala ndani ya jeneza kama vile yu usingizini na angeamka muda mfupi baadaye, lakini huo ndiyo ulikuwa mwisho wake nisingemwona tena. Hakika ilikuwa inaumiza, kwa mara nyingine tena kampuni ilikuwa imepoteza moja ya silaha zake muhimu katika habari za uchunguzi.

Wiki chache kabla ya kifo cha Sanchawa siku moja nilijisikia tu moyoni mwangu nahitaji kukutana na wahariri kwenye hoteli moja iitwayo Safari Carnivore iliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam, nikampigia simu Erick Evarist, mmoja wa wahariri ofisini kwetu na kumwambia aratibu mkutano huo, katika maagizo yangu nashindwa kuelewa ni kwa nini nilijikuta natamka…

“Erick hakikisha Sanchawa hakosi.”
“Sawa mkurugenzi, atakuwepo!”

Nilisikia tu kutoka moyoni Sanchawa awepo, sielewi sababu ni nini lakini baada ya kifo chake muda mfupi baadaye ndipo nilielewa kwamba Roho wa Mungu alinielekeza niagane na Sanchawa kwenye tafrija hiyo ya mwisho pamoja naye! Siku hiyo alikuwa mkimya, akinywa kinywaji chake taratibu, kwa wanaomfahamu Sanchawa alivyomchangamfu na mtu anayetaka watu wacheke wakati wote, tabia yake ya usiku huo haikuwa ya kawaida.

Ninachoweza tu kusema ni kwamba kampuni yetu imepoteza mtu muhimu sana, ni kweli hapa na pale tulikuwa tukisukumana na Sanchawa ili afanye kazi nzuri, lakini ninachoweza kusema kwa ujumla wake ni kwamba mtu huyu alikuwa muhimu sana kwa maendeleo ya kampuni yetu, Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi, ametangulia yeye sisi tunafuata.

Kazi ya gazeti ni kazi moja ‘mbaya’ huwa naifananisha na mfugaji wa ng’ombe, hata kama mwenye ng’ombe atakufa, mifugo hao ni lazima wakachungwe, huwezi kusema “mwenye ng’ombe kafa, basi ng’ombe leo hawapelekwi machungani!” ni lazima wakachungwe, wala wao hawajali kuwa mwenye mali amekufa, ndivyo ilivyo kazi ya gazeti, lazima litoke hata siku ambapo mimi mwenyewe nitakuwa nimekufa, lazima wapatikane watu ofisini wa kuchonga vizuri picha yangu na kuiweka gazetini chini ya kichwa cha habari watakachoona kinafaa.

Nasema hivi kwa sababu baada ya kifo cha Sanchawa hakuna kitu kilichobadilika, watu wawili waliteuliwa kuiwakilisha kampuni kwenye maziko huko Serengeti, wengine tukakubaliana na hali na kuendelea na kazi, habari mbalimbali zikichapishwa za watu maarufu, Magufuli na serikali yake, Baraza la Mawaziri, Ziara za Kushtukiza nk.

Tulikuwa katika safari ya kuelekea mwishoni mwa mwaka, kipindi ambacho huwa ni kigumu sana kwangu mimi na biashara yetu, niseme wazi hali ilikuwa ni ngumu, ilikuwa ni lazima kufanya kazi kwa juhudi kubwa na kuhimiza watu kujituma! Kuna wakati katika maisha ya kampuni watu hujisikia wamechoka, kama kiongozi unalazimika kuhamasisha.

Hicho ndicho kipindi tulichokuwa nacho, mauzo yanashuka na gharama za uendeshaji zinaongezeka, hapo hulazimu kusimama na kujiuliza ni kitu gani kifanyike! Nikakutana na viongozi na kuwaeleza mahali tulipo na tunapokwenda, ikaonekana wote wamenielewa na kwa pamoja tulikuwa na wajibu wa kupambana kila mtu katika nafasi yake, kuiokoa kampuni lakini pia kuokoa wenzetu ambao kama tusingebadilisha upepo tungelazimika kuwapunguza, jambo ambalo nilikuwa sitaki kabisa litokee.

Kampuni ikaamua ili kuchochea mauzo ibadilishe maisha ya Mtanzania mmoja kwa kutoa Zawadi ya Nyumba, ilikuwepo nyumba ambayo kampuni ilikuwa imejenga maeneo ya Salasala, tukaamua tuitoe nyumba hiyo kwa wasomaji wetu kwa njia ya Bahati Nasibu ambayo wasomaji wetu wangekata kuponi kwenye gazeti, kuijaza na kuituma kwenye ofisi yetu au kuipeleka kwa Mawakala wa Magazeti yetu waliyo karibu yao, mwisho wa siku tuchezesha Bahati Nasibu na mtu mmoja ajishindie nyumba hiyo jijini Dar es Salaam.

Mtu yeyote kutoka sehemu yoyote ya nchi yetu ana nafasi ya kumiliki nyumba jijini Dar es Salaam, tulishatoa zawadi nyingi kwa wasomaji wetu lakini hii ni zawadi kubwa kuliko zote tulizowahi kuzitoa kama shukrani kwa kuungwa mkono na Watanzania.

Haikuwa rahisi kwa Watanzania kuamini kwamba Global Publishers ilikuwa imetoa nyumba kama zawadi kwa wasomaji wake, tukalazimika kumualika Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mheshimiwa Paul Makonda aje atuzindulie Bahati Nasibu yetu, nafurahi alifika na kuifanya kazi hiyo ndani ya ofisi ya Global Publishers, Bamaga jijini Dar es Salaam.

Kilichofuata baada ya hapo ni watu kununua magazeti, kukata kuponi na kutuma jambo ambalo linaendelea kila kona ya nchi yetu hivi sasa. Global Publishers haitoi nyumba hii kwa sababu ni kampuni tajiri bali inafanya hivi kwa sababu inaamini katika kuwashirikisha wengine kwenye baraka ambazo Mungu amenimwagia.

Mara nyingi nimesema siku nitakapokufa na kufika mbinguni, naamini Mungu hataniuliza “Shigongo mwanangu ulijenga nyumba ngapi au umeacha fedha kiasi gani kwenye akaunti, Mungu hatavutiwa na hayo bali ataniuliza “Ulishirikiana vipi na wenzako katika baraka nilizokupa, ulilisha wajane wangapi? Ulitunza yatima wangapi? Uliwatembelea hospitali wagonjwa wangapi?”

Hayo ndiyo yatakuwa maswali ya Mungu na ninataka niyajibu kabla sijaenda kwake ndiyo maana mimi na wenzangu tunafanya mambo tunayoyafanya katika jamii tukijiwekea akiba kwa Mungu, kwa kufanya hivi Mungu amezidi kutukuza na kutuimarisha, hii ni siri nyingine ya mafanikio ambayo wanadamu wanatakiwa kuifahamu, Mungu huwapa watu ambao anaamini watavitumia vitu anavyowapa na watu wengine.

“Ngrii!Ngriii!” ulikuwa ni mlio wa simu yangu nikiwa ofisini mchana wa tarehe 21/12/2015 siku ya Jumatatu.

Nilipoinyanyua na kupokea, rafiki yangu Hassan Ngoma alikuwa hewani akinijulisha kwamba mama yake alikuwa mgonjwa sana, amelazwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo. Nilikuwa katikati ya kazi nyingi, nikamwambia baada ya muda mfupi ningekuwa pale na ndivyo ilivyokuwa mara nilipokamilisha kazi niliyokuwa nikiifanya.

Hassan na mimi si tu marafiki bali tumekwishakuwa ndugu, kijana huyu ni mmiliki wa chuo kiitwacho Mlimani School of Professional Studies kilichopo jijini Dar es Salaam, mimi na yeye tulifahamiana miaka mingi wakati huo akisoma nchini Uingereza, alipokuja nchini wakati akiandika andiko lake la digrii ya pili alifika ofisini kuniona na kukiri kwamba mimi nimekuwa ni miongoni mwa watu wanaomvutia sana hapa duniani na alitamani kuwa kama mimi.

Mtu wa darasa la saba anamvutia mtu anayesoma digrii ya pili nchini Uingereza! Haikuwa rahisi sana kuamini lakini nilipokea sifa hizo kwa mikono miwili, wiki chache baadaye nilialikwa kwenda kuzungumza na akina mama wa Gongo la Mboto kuhamasisha kuhusu kupambana na umasikini, Hassan akaomba kuongozana na mimi, nikampitia yeye na rafiki yake aitwaye Seif Chomoka eneo la Ubungo.

Ndani ya gari nilikuwa na kazi ya kupanda mbegu ya ushindi mioyoni mwa vijana hao, Hassan alionekana kunielewa sana lakini rafiki yake, Seif Chomoka ambaye walisoma pamoja Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakati huo akiwa mwajiriwa wa ofisi ya rais alionekana kutokukubaliana na mambo niliyokuwa nikizungumza, yeye alikuwa miongoni mwa vijana walioamini katika kuajiriwa si kujiajiri wenyewe.

“Hakuna shida, ili mradi tu umenisikiliza ninachokiongea, maneno haya yataendelea kufanya kazi ndani ya moyo wako maisha yote mpaka utakapochukua uamuzi, cha muhimu ni kunisikiliza, hilo ndilo kosa kubwa ulilofanya…” nilimwambia kijana huyo.

Nilifanya semina hiyo Hassan akiwa ameketi na mimi mbele, baadaye nikampa nafasi ya kuzungumza na akina mama wale, jambo ambalo sikufahamu ni kwamba kumbe niliyekwenda kuongea naye siku hiyo ni Hassan na rafiki yake, kwani alipomaliza tu masomo yake nchini Uingereza hakutaka kuajiriwa akaanzisha chuo chake mwenyewe, leo hii ana wanafunzi zaidi ya mia tatu.

Urafiki wangu na Hassan ulikua sana baba yangu alipofariki dunia miaka minne iliyopita, alikuwepo kijijini kwetu kumzika! Kitendo hicho sikukichukulia kiwepesi, maana jijini Dar es Salaam watu wana shughuli nyingi, mtu kuamua kuacha kazi yake kwenda kumzika baba yako ni heshima kubwa, ndiyo maana aliponiambia mama yake anaumwa haraka niliiacha kazi na kwenda kuungana naye Lugalo hospitali.

Nilimkuta mama anaumwa, nikapata bahati ya kumbeba kutoka kitandani kumweka kwenye machela ili apelekwe wodini ambako hatukuruhusiwa kuingia, tukaketi kwenye mabenchi mahali fulani karibu na maabara ya Hospitali ya Lugalo kwa karibu saa mbili, ndipo nikamwomba Hassan nirejee ofisini ambako baadaye nilielekea Muhimbili kumwona shemeji yangu ambaye alikuwa amelazwa hapo.

Nilipoondoka tu, saa nzima baadaye nikiwa Muhimbili, mama yake na Hassan alifariki dunia, sikuweza kufahamu mapema sababu simu yangu ilizima, niliporejea ofisini kutoka Muhimbili na kuichaji simu yangu ndipo nikaupokea ujumbe huo! Moyo wangu ulisikitika sana, nikaondoka moja kwa moja hadi Hospitali ya Jeshi Lugalo ambako nilikuta mwili umeondolewa kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti cha Muhimbili.

Siku mbili baadaye tulikuwa Kijiji cha Makanya Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro kwa mazishi ya mama yake Hassan, nilifurahi kukutana na ndugu zake, lakini nilifurahi zaidi kukutana na rafiki yake Hassan, Seif Chomoka tuliyekuwa naye ndani ya gari miaka minne kabla tukielekea Gongo la Mboto kuongea na akina mama, nikamweleza juu ya ujasiriamali akanipinga.

“Uko wapi siku hizi? Ofisi ya rais bado?”
“Ahaa wapi! Niliacha kazi kaka, maneno yako ya siku ile yaliniingia!”
“Uko wapi?”
“Niko Morogoro, nilianzisha chuo pale kinaitwa St. Joseph College, kimekuwa kikubwa sasa!”

“Kweli?”
“Kabisa kaka, niko pale, ukitembelea Morogoro usiache kuniona mdogo wako!”
Moyo wangu ukajawa na furaha! Mtu mwingine tena alikuwa amekombolewa na Injili ambayo kwa miaka ishirini nimeihubiri…

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave A Reply