The House of Favourite Newspapers

Trump Asema Yeye Si Mbaguzi

RAIS  wa Marekani, Donald Trump,  amesisitiza kuwa yeye si mbaguzi.

 

Trump amesema hivyo baada ya mashambulizi yake  kupitia Twitter dhidi ya wabunge wanne wanawake aliowakemewa vikali.

 

Katika ukurasa wa Twitter aliwataka wanawake hao wasio na asili ya Marekani, ”kuondoka” kuelekea kwenye nchi zao walipotoka.

”Sina asili yoyote ya ubaguzi mwilini mwangu!” alisisitiza Trump kupitia mtandao huo.

 

Bunge la Wawakilishi linajiandaa kupigia kura makubaliano ya pamoja ya kukemea kauli zake, huku hatua hiyo ikitegemewa kupita kutokana na kuwepo wawakilishi wengi wa Democrats.

Awali, wabunge Alexandria Ocasio-Cortez, Ilhan Omar, Ayanna Pressley na Rashida Tlaib walitangaza kupuuza matamshi ya Trump wakidai yanalenga kuwaondoa kwenye mstari.

 

Wabunge hao waliwataka watu nchini humo kupuuza maneno yake. Rais Trump hakutamka majina ya wanawake hayo kwenye ukurasa wa Twitter, lakini yaliyokuwemo kwenye matamshi yake yalionyesha wazi kuwepo kwa uhusiano na wabunge hao.

 

Alisababisha hasira baada ya kusema wanawake  ”ambao asili yao wanatoka kwenye nchi ambazo serikali zake  zina machafuko” warejee makwao.

 

Wakizungumza na waandishi wa habari,  wanawake hao wamesema, hivi sasa watu waweke akili zao kwenye sera za nchini Marekani na si maneno ya Rais Trump.

Bi Pressley amezitupilia mbali jitihada za rais ”kutukandamiza na kutunyamazisha”, akisema walikuwa ”zaidi ya watu wanne.”

 

”Kikosi chetu ni kikubwa. Kikosi chetu kinahusisha mtu yeyote aliye tayari kujenga ulimwengu wa usawa na haki,” alisema.

 

Wanawake wote wanne wamesisitiza kuwa huduma za afya, matumizi mabaya ya silaha, pia kushikiliwa kwa wahamiaji katika mpaka kati ya Marekani na Mexico ni masuala ya kutazamwa.

 

Bi Omar amesema maneno ya Trump yanadhihirisha kuwa ”mashambulizi ya ubaguzi wa rangi” dhidi ya wanawake wanne,  maneno ambayo ”hayana maana yoyote isipokuwa kuigawa nchi yetu.”

 

Awali rais huyo alisema kwa Bi Omar alikuwa akiunga mkono kundi la wanamgambo wa al-Qaeda.

 

”Ninajua kuwa kila muislamu aliyeishi nchini humu na duniani kote amesikia kuhusu kauli hiyo, hivyo sitaipa nafasi kwa kuijibu,”aliongeza kuwa hakutegemea jumuia ya watu weupe kujibu baada ya mtu mweupe ”kuua kwenye shule au jumba la sinema, msikiti au sinagogi”.

 

Bi Ocasio-Cortez alisimulia jinsi alipotembelea  jiji la Washington DC akiwa mtoto, akisema watu wawaambie watoto wao kuwa ”chochote kile atakachosema rais, nchi hii ni yenu”.

 

Mgogoro umeanzaje?

Siku ya Ijumaa, Bi Ocasio-Cortez, Bi Tlaib na Bi Pressley walitoa ushuhuda mbele ya wabunge kuhusu hali za wahamiaji wanaoshikiliwa kwenye vituo ambavyo walivitembelea.

 

Wabunge wa Democrat kwa kiasi kikubwa wameushutumu utawala wa Trump hasa namna anavyodhibiti mpaka, wakisema wanawashikilia wahamiaji ambao sasa wana hali mbaya.

 

Trump amewatetea maofisa wake walioko mpakani .Utawala wake ulitangaza sheria mpya inayoanza kutumika Julai 16 mwaka huu, inayokataa kutoa hifadhi kwa mtu yeyote anayevuka mpaka wa kusini ambaye hajaomba kupatiwa hifadhi kwenye ”nchi ya tatu”.

 

Wabunge wa Democratic na Republican wamesemaje?

Wana-Democrat wamekemea vikali kauli ya Trump, na wengi kwa haraka walisema ni shambulio la kibaguzi.

Viongozi wa Republican, hata hivyo, hawajazungumza sana. Seneta Mitch McConnell amesema atajibu maswali siku ya Jumanne.

Waziri wa Fedha, Steven Mnuchin,  amesema: ”Sioni kama matamshi hayo ni ya kibaguzi, rais amefafanua kauli yake.”

Seneta na aliyewahi kuwania urais, Mitt Romney,  amesema kauli za Trump ”zinaharibu, kukandamiza na kuwagawa watu.”

Comments are closed.