The House of Favourite Newspapers

Yatima Huyu Anahitaji Milioni 200 Kuokoa Maisha Yake – Video

 

KIJANA Constantine Nguma (17) mkazi wa Kunduchi Beach jijini Dar es Salaam mwenye gonjwa zito la ‘Aplastic Anemia’  tiba yake inahitaji dola 90,000 ambazo ni sawa na shilingi milioni 200 na kwamba zisipopatikana hawezi kupona.

 

Nguma ambaye hana baba wala mama kutokana na wao kufariki dunia kwa sasa anaishi chini ya uangalizi wa taasisi ya Help2Kids inayojishughulisha na uangalizi wa watoto wenye uhitaji.

 

MSIKIE MENEJA MRADI

Akizungumza jana (Jumatatu) na  +255Global Radio Meneja Mradi wa Afya wa taasisi hiyo Imerine Leonard alisema mbali na kusaidia watoto wengine wengi katika kituo chao wameona vyema wakamchukua na Nguma ili kuweza kumsaidia.

NGUMA AELEZA TATIZO LAKE

Aidha baada ya kupata utangulizi wa Imerine, mwandishi wetu alifanya mazungumzo mafupi na Nguma ambaye anapumua vizuri kwa msaada wa vifaa maalumu ili kujua ugonjwa ulivyoanza.

Mwandishi: Tatizo lako lilikuanza lini?

Nguma: Lilinianza Januari mwaka huu.

Mwandishi: Pole sana, wazazi wako wapo?

Nguma: Wazazi wangu walishafariki dunia muda mrefu.

Mwandishi: Ulikuwa unasoma?

Nguma: Ndiyo, nilikuwa nasoma elimu ya Sekondari, lakini nilipoanza kuumwa ikabidi nisitishe masomo.

Mwandishi: Una lipi la kuwaambia Watanzania?

Nguma: Nawaomba Watanzania wazidi kuniombea ili nipone, pia naomba wazidi kunichangia pesa ya matibabu ili nikatibiwe.

IMERINE AFAFANUA UGONJWA WA NGUMA

Mwandishi: Imerine ambaye umejitambulisha kama meneja afya wa taasisi; unaweza kutuambia kwa undani zaidi Nguma anasumbuliwa na tatizo gani?

Imerine: Nguma alianza kuumwa tangu Januari mwaka huu, akalazwa Muhimbili, ugonjwa wake ni Aplastic Anemia, mwili wake hauwezi kutengeneza damu wenyewe.

 

Mwandishi: Ok, nini kinachotakiwa kufanyika kuondoa tatizo hilo?

Imerine: Kwenye mifupa kuna kitu kinaitwa Bone Marrow (ute uliopo katikati ya mifupa hasa mikubwa) hii ndiyo haipo kwa kiwango kinachohitajika, hivyo anatakiwa kuwekewa maana bila hivyo hata ukimuongezea damu itaisha.

Mwandishi: Matibabu haya anaweza kuyapata hapa nchini?

Imerine: Kwa Tanzania hiyo tiba haipo ndiyo maana tunafanya mikakati aweze kupelekwa India au Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

MILIONI 200 ZATAJWA

Aidha, taarifa ambayo imetolewa na matabibu wanaoshughulikia matibabu ya Nguma zilisema kiasi cha shilingi milioni 200 zinahitaji kugharamia matibabu ya Nguma.

Hata hivyo kutokana na changamoto zinazokikabili kituo kinachomlea, kiasi hicho cha fedha ni kikubwa ndiyo maana walezi hao wamelazimika kupaza sauti ili kuomba msaada wa fedha kutoka kwa wasamaria wema ili Nguma aweze kusafirishwa kwenda nje ya nchi kimatibabu.

 

“Tunasaidia watoto wengi, hivyo ile pesa ambayo tunaipata tunaigawa kwa watoto mbalimbali, sasa kupata pesa ya kutosha kuweza kumpeleka Nguma India inakuwa ngumu, hivyo ndiyo maana leo tunaomba msaada kwa Watanzania,” alisema Imerine.

Aliongeza kuwa katika kipindi hiki ambacho wanasubiri fedha ziweze kupatikana wanaendelea kumpatia matibabu mengine hili kumwezesha Nguma kuendelea kuishi.

“Kwa sasa hivi kuna dawa anatumia ambazo kila siku anatakiwa ameze mara mbili, asubuhi na jioni na kila mwezi huwa tunampeleka kliniki kwa ajili ya kuangalia mwenendo wa damu mwilini mwake kama imepanda au imeshuka.

 

MENEJA WA HELP2KIDS NAYE ANENA

Naye Meneja Mradi wa kituo hicho, Tim Spooner alisema: “Ili Nguma  aendelee kuishi  kila mwezi inahitajika shilingi milioni 2 na zaidi fedha ambazo kituo kimekuwa kikitoa kwa ajili ya kuweza kusogeza mbele maisha yake wakati tukisubiri uwezo wa kumpeleka India upatikane.”

 

JINSI YA KUMCHANGIA NGUMA

Wakati huohuo Spooner alieleza utaratibu wa kufuata kwa mtu anayetaka kumsadia Nguma ambapo alisema:

“Mtu akihitaji kutoa msaada wowote atembelee tovuti ya taasisi hiyo WWW.HELP2KIDS.ORG ambako atakutana na maelezo kamili ya jinsi ya kufanya ili mchago wake umfikie mlengwa ambapo kwa maelekezo zaidi wasamaria wametakiwa kutumia namba ya simu ya mkononi 0763 905 038.

 

Comments are closed.