The House of Favourite Newspapers

Tulipofikia, Wanawake ni Hatari Kwa Vizazi Vijavyo!

0

KWANZA nianze kwa kutoa pole kwa familia ya marehemu, wanafunzi wa shule ya Atlas, na waombolezaji wote walioguswa na msiba wa mtoto Norah aliyefariki juzi julai 23, na kuagwa jana nyumbani kwao Sinza-Mori, kisha kupumzishwa kwenye nyumba yake ya milele katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Hakika Mungu ni mwema, atawapa nguvu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu kwenu, cha msingi endeleeni kuwa na imani naye na msiache kumtumikia.


Kuna kitu kikubwa nimejifunza kupitia msiba huu, na nimeona si vyema kukaa kimya, ili wewe unayesoma makala hii kama una tabia nitakazoziongelea basi usiache kubadilika na uwe balozi mzuri wa kutoa elimu kwa wengine ili nao wabadilike kwa faida ya vizazi vyetu vya sasa na vijavyo.
Nimegundua kwamba asilimia kubwa ya wanawake hawajui tofauti kati ya mavazi ya msibani na harusini na muonekano kwa ujumla. Na kama wanajua basi wanafanya makusudi, na ipo haja ya wao kubadilika.
Hivi unawezaje kwenda msibani ukiwa umevaa mavazi ya kutamanisha? Yaani unadiriki kuvaa suruali ya kubana, imekuchora mwili wote kwa sababu tu umejaliwa umbo lenye mvuto basi unaona ni vyema kulianika hadi kwenye msiba!
Sijawasahau wale mliovaa vimini, blauzi zinazoangaza {transparent} hivi lengo lilikuwa ni kutuonyesha jinsi Mungu alivyoumba vifua vyenu kwa ustadi mkubwa au nini? Haya, na nyie mliojikwatua mithili ya bibi harusi mlisahau kama ule ni msiba au mmeamua tu kujizima data?
Tukubaliane kwamba msibani siyo sehemu ya kufanya maonyesho ya mavazi wala kujionyesha ni kwa kiasi gani unaweza kuupamba mwili wako. Yapo matukio husika yanayoruhusu vitendo hivyo, kama vile kwenye harusi.
Simaanishi kwamba uende msibani ukiwa mchafu au uvae nguo chafu, lakini ni utamaduni wetu Watanzania kujistiri mahali popote pale, ukishindwa basi jitahidi tu kwenye misiba, ili kuepuka aibu na kunyooshewa vidole vinavyoambatana na maneno ya kuwa “dunia imekwisha”.


Pia tunatakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa vizazi vyetu, msiba wa Norah ulijaa watoto ambao ni wanafunzi wenzake. Hivi wamejifunza nini kwenu nyie wazazi mliokuja nusu uchi msibani Kesho unaanzaje kumkanya mtoto wako asivae kama wewe? Huo ndiyo mwanzo wa mtoto kukosa maadili, jambo ambalo litakwamisha mafanikio yake.
Nimalizie kwa kuwaomba mbadilike na kuachana na tabia hiyo inayodhalilisha wanawake wote, kujistiri siyo dhambi na ndiyo jambo ambalo hata vitabu vya dini zote vinasisitiza ili kuwaepushia wanaume dhambi ya kutamani.
Pia namuombea mtoto Norah apumzike kwa amani katika nyumba yake ya milele, Mwenyezi Mungu amfungulie milango ya pepo. Hakika ameacha pengo kwa wazazi wake kwa sababu alikuwa ni mtoto pekee kwa baba na mama yake.
Na Isri Mohamed/GPL

Leave A Reply