The House of Favourite Newspapers

Tulivyoteseka Kwenye Mianzi ya Kichawi – 2

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:
Alitokea mzee mmoja ambaye alikuwa chotara, alikuwa na ndevu nyingi nyeupe na karibu kichwa chake chote kilikuwa na mvi.

“Karibuni wajukuu zangu,” alisema mzee huyo.
Kwa kuwa mimi ndiye nilikuwa mkuu wa msafara nilimsogelea. Aliponishika mkono mwilini nikaona kama nimepigwa shoti ya umeme! Nikapiga yowe!

Je, nini kitatokea?

SONGA NAYO…

Nilimuangalia usoni baada ya kuniachia akawa anatabasamu, nikajua kuwa alikuwa na mapengo na meno yake yalikuwa meusi kama vile anakula ugoro.

“Nisikilizeni. Mimi naitwa Mzee Mavaka. Huyu kiongozi wenu nimemuonesha kuwa katika bustani hii hakuna mchezo. Kila unachokiona kiheshimu. Ukitaka kuchuma chochote ni lazima uniambie mimi ili niweze kutoa baraka za kufanya hivyo.

Hii ni bustani iliyohifadhiwa na himaya ingine ili kutoa funzo kuwa mazingira yanapaswa kutunzwa hivi. Kwa hiyo usichume kitu bila ruhusa yangu, nawajua nyinyi vijana wa Dar mlivyo wabishi, ubishi wenu uishie kulekule kabla ya kuingia katika bustani hii tukufu ya Nangose, sawa?”

Tukaitikia kwa pamoja “Sawaaa.” Ilikuwa kama vile tuliambiana.
“Mianzi hii mnayoiona ni ya aina yake, imepandwa kwa mstari na kwa umaridadi kama mnavyoona na kila kitu kilichomo ndani ya bustani hii ni fahari ya dunia hii. Ogopeni, heshimuni. Ona jinsi nyasi zilivyofyekwa na vipepeo wanavyofurahia mandhari hii.

aribuni zingatieni sheria hiyo ya kutochuma chochote bila ruhusa yangu,” alionya.
Alitupeleka kwenye mgahawa wa bustani tukala chakula bure. Ajabu ni kwamba tulikuta ‘bufee’ yenye kila aina ya chakula na kila mtu alikuwa anajipakulia mwenyewe chakula akipendacho.

Pia kulikuwa na vinywaji baridi vya kila aina. Tulimuuliza yule mzee Mavaka nani analipia bili ya chakula, akasema hiyo analipa mwenye bustani. Tulimuuliza ni nani? Hakujibu akawa anatabasamu tu!

Vijana wa Dar kama unavyowajua ni wabishi, wakaanza kuchuma ‘maembe ya kusini’ wenyewe huziita embe mali, wakawa wanakula, ulikuwa ni msimu wa maembe. Wengine hasa wasichana wakawa wanachuma maua yenye harufu nzuri na kuyatunga kwenye nyuzi zao kisha kuzivaa shingoni bila kupata idhini ya yule mzee.

Tuliendelea kutembelea bustani ile na kugundua kuwa kulikuwa na sehemu ambayo ilikuwa na maji yametuama ni kama bwawa kubwa na kulikuwa na mtu ameketi kando yake, tulikwenda kuangalia anafanya nini, kumbe alikuwa anavua samaki ajabu ni kwamba alikuwa hatuangalii, alikuwa anavua samaki mmojammoja kwa kutumia ndoana na kuwaweka kwenye kapu kubwa.

“Mzee shikamoo.” Nilimuamkia.
“Siwezi kukujibu salamu yako,” alijibu kijeuri yule mzee.
“Sasa mzee mbona unajibu hivyo, tumekukosea nini? Sisi ni wageni hapa.”
“Makosa mliyoyafanya mnajifanya hamyajui mpaka mimi niwaambie?”
“Tuambie mzee, sisi ni kama wajukuu zako.”

“Kwanza ondokeni hapa kwenye bwawa la samaki, watoto wajinga sana nyie, wajukuu zangu gani msiosikiliza mnachoambiwa na wakubwa wenu? Nasema ondokeni!” alizidi kufoka, alituangalia, macho yake yalikuwa mekundu kama mtu aliyevuta bangi!
Tuliondoka eneo hilo, mbele yake tuliona kuna mianzi mizuri sana na watu wanaikata ile iliyokomaa tu na kuipakia kwenye gari.

“Jamani habari za hapa,” niliwasalimia watu wale.
“Nzuri. Mnataka mianzi? Kuna masharti ya kuikata,” alijibu mmoja wa wale vijana waliokuwa wakikata na wengine walikuwa wakiipakia kwenye gari aina ya Canter.

“Masharti gani? Hayo ni mambo ya kizamani bwana,” mwenzetu mmoja akasema.
“Siyo mambo ya kizamani, kuna masharti msipoyatekeleza mtapata madhara mazito. Tunaambiwa ni hatari na unaweza kupoteza wenzako wote uliofuatana nao.”

“Watapoteaje? Acheni hayo, uongo mtupu,” akadakia kijana mwingine miongoni mwetu.
“Wewe unayetueleza habari hizo umewahi kushuhudia mtu akiadhibiwa kwa kula matunda au kukata mianzi katika bustani hii tangu uzaliwe?” akadakia dada mwingine.
“Mimi sijashuhudia lakini kuna simulizi nzito sana nimesimuliwa na wazee kuhusu bustani hii ya mianzi ya Nangose.”

“Kwanza tueleze kwa nini inaitwa bustani ya mianzi ya Nangose wakati kuna matunda mengi kama vile miembe na maua ya kila aina?”

“Hilo mimi siwezi kujibu, kwa kuwa mimi siye mwenye bustani,” alijibu kijana huyo.
Yupo kijana miongoni mwetu alichuchumaa na kuchukua mundu na kwenda kukata mianzi michanga ili aone kama inatoa pombe ya ulanzi kwani yeye ni mtu wa Iringa.
Mara nilimuona mzee Mavaka aliyetupokea akitoka kwenye ule mgahawa akiwa ametoa macho na mwili kumtetemeka.

“Nani kakata mianzi michanga na kuchuma maembe na maua bila idhini yangu? Nyinyi vijana wa Dar habari zenu nimezisikia ndiyo maana nikawaonya kabla, nimeona kwenye chombo ndani mkichuma embe na maua na sasa mmekata mianzi, sasa mtaona cha mtema kuni,” alifoka mzee Mavaka.

Huku akitetemeka, sekunde chache tukashuhudia tetemeko la ardhi! Bustani yote ikawa inatetemeka! Mianzi ikawa inatupiga, yowe zilikuwa nyingi na hatukuwa na uwezo wa kukimbilia kwenye basi.

Nilishuhudia ardhi ikizama huku baadhi ya wenzangu wakiwa wamezimia kutokana na kupigwa na mianzi. Kipande cha ile bustani kiliendelea kuzama huku tukiwa juu yake, nikawa naona giza linaanza kuingia kadiri tulivyokuwa tunazama nuru ya jua ikawa inapotea machoni mwangu badala yake nikawa nasikia sauti za kutisha.

Mshangao uliniingia baada ya kuona kutitia huko kwa bustani kuliendelea kwa saa nzima nikawa sioni chochote isipokuwa giza lilikuwa totoro. Moyo wangu ulinienda mbio nikijua kuwa sasa utakuwa mwisho wa maisha yetu.

Nilianza kutetemeka wakati ardhi ikizidi kuzama, ilikuwa kama tupo kwenye lifti na tunashushwa chini kutoka ghorofani, swali likawa tunazamishwa na nani na je, tutapona au mwisho wa yote ni kufunikwa na ardhi? Moyoni niliwalaumu wenzangu kwa kutofuata masharti ya bustani ile ya Mianzi ya Nangose.
Je nini kitatokea? Fuatilia Jumanne ijayo.

Leave A Reply