The House of Favourite Newspapers

Tumuenzi Nyerere kwa Namna Gani?

0

MIAKA 22 imepita tangu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere atutoke na kutuachia mema ambayo tumejipa jukumu la kuyaenzi.

 

Kuenzi maana yake ni kutunza na kuyaendeleza mema aliyofanya Hayati Nyerere. Pengine cha kujiuliza nani anaweza kupita mbele ya umma na kusema “Mimi hapa nayaenzi ya Mwalimu kwa vitendo?”

 

Na kama atakuwepo kati yetu wa kufanya hivyo, watu watampigia makofi na kusema “ndiyo” huyu anamuenzi kweli Nyerere au watabaki wakimtazama usoni na kughadhibika moyoni kwa hasira?

 

Ninachokiona ni kama baadhi yetu tunataka kuitumia siku ya kumbukumbu ya kifo cha Nyerere Oktoba 14, 1999 kama sehemu ya sherehe mfano wa Sikukuu ya Iddi, Krismas au Mwaka mpya, tupumzike majumbani kwetu tule wali na kunywa mvinyo na kulewa kidogo.

 

Nikumbushe mambo matano yaliyokuwa dira ya Nyerere katika uongozi wake:

Moja; kukomesha ukabila, pili kuzika udini, tatu; kuondoa ujinga, maradhi na umaskini, nne; kusimamia maadili ya uongozi na mwisho ni kudumisha muungano.

 

Mambo manne kati ya hayo yanaweza kuwa ni majukumu ya Watanzania wote, lakini hili moja la maadili ya uongozi linawahusu zaidi wenye dhamana ya kuongoza watu, wenyewe watajitafakari.

 

Nyerere alisema katika hotuba yake mwaka 1995 kwenye mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwamba:

“Nchi yetu hii ni ya maskini, wakulima wetu, wafanyakazi wetu maskini. Nchi hii bado ni nchi ya wakulima na wafanyakazi ambao wote ni watu maskini. Nchi hii haijawa nchi ya matajiri. Chama hiki (CCM) hakijawa chama cha matajiri. (Makofi). Tunataka tuendelee kushughulika na umaskini wa watu wetu. Tushughulike kwa dhati na matatizo ya wananchi; ya hali yao ya uchumi, hali yao ya viwandani, hali yao ya mashambani, hali yao ya shuleni, hali yao ya hospitalini,” mwisho wa kunukuu.

 

Kati yetu nani anayaenzi haya kwa vitendo kwamba anapiga vita kila siku udini, ukabila, ujinga maradhi na umasikini na kwa moyo wa dhati mahali alipo; anashughulika na hali za Watanzania wote wapate kuinuka kimaisha na siyo kujiinua yeye na familia yake?

 

Nyerere hakutumia ukubwa wake kuonea watu, hakutumia madaraka yake kujitajirisha, hakuthubutu kuivunja katiba ili ajipatie faida yoyote.

Nani kati yetu anayaenzi haya ya mwalimu kwa vitendo? Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Iweke Roho ya Hayati Julius Nyerere mahali Pema Peponi.

 

Ujumbe huu naomba uweke chapa kwa kila Mtanzania, tangu viongozi hadi wananchi wa kawaida ili tuwe watendaji wa maneno yetu na siyo wasemaji tu.

Imeandikwa na Richard Manyota.

Leave A Reply