The House of Favourite Newspapers

Tumuunge Mkono Rais Samia, Tusimpuuze JPM

0

KWA takriban wiki nzima sasa, gumzo mitandaoni limekuwa ni kuhusu mambo mbalimbali aliyoyafanya Hayati Dk John Pombe Magufuli enzi za uhai wake.

 

 

Kila mmoja anasema lake hasa baada ya kuona Rais Samia Suluhu Hassan ameanza kushughulikia mambo ambayo yalikuwa yanawasibu watu. Suala la kwanza lililowafurahisha watu kwa Rais Samia ni kuhusu kutowasumbua walipa kodi.

 

 

Kwa takriban mara mbili katika hotuba zake, Rais Samia amezungumza kutowasumbua wafanyabiashara katika suala zima la kodi. Kutotumia nguvu katika kukusanya kodi. Akaenda mbali zaidi kwa kusema, wafanyabiashara wakubwa nchini wameondoka kwa sababu kodi ya nchi yetu si rafiki.

 

 

Akasema suala hilo ndilo linalofanya nchi isiwe na mzunguko mzuri wa pesa na matokeo yake, wananchi wanakuwa hawana fedha mifukoni. Lingine alilozungumza ni kuruhusu eneo la hifadhi ambalo lilikuwa haliruhusiwi kuchimba madini, sasa yachimbwe.

 

 

Pia aliwataka wanaotoa vibali vya uwekezaji kuacha urasimu. Wamekuwa wakiwasumbua wafanyabiashara ili watoe rushwa na matokeo yake wawekezaji wengi wamekuwa wakiondoka nchini na kusema Tanzania haina msimamo katika mambo yake.

 

 

Lingine alilozungumza ni kuhusu msimamo wa Taifa katika janga la Corona. Amesema, anakusudia kuunda timu ya wataalamu ambayo itaishauri Serikali nini cha kufanya katika kukabiliana na janga hilo ili kama taifa tuwe na msimamo wetu katika kushughulilikia suala hilo.

 

 

Alisema ni vizuri wataalam hao wakafanya utafiti wa kitaalam na kuishauri Serikali maana haiwezekani nchi nyingine zikawa na takwimu za wagonjwa au vifo wakati kwetu tunaonekana hakuna kitu.

 

 

Pamoja na mambo mengine mengi, alimuagiza bosi mpya aliyemteua TCRA, Dk Jabir Bakari Kuwe kusimamia vizuri mamlaka hiyo ili kusiwepo na kelele za malalamiko kutoka kwa wananchi kama zilizoibuka hivi karibuni kuhusu vifurushi vya mitandao ya simu.

 

 

Sasa kutokana na mambo hayo aliyoanza nayo Rais Samia, baadhi ya watu wameanza kumkejeli Hayati Magufuli kana kwamba hakufanya kitu. Ndugu zangu hii sio sawa. Hayati Magufuli amefanya mengi mema kwenye hii nchi.

 

 

Amegusa mioyo ya watu wengi hususan wale wa hali ya chini na ndio maana hata kwenye mazishi yake, tumeshuhudia rekodi ya umati mkubwa wa watu kutaka kumuaga. Watu walitandika kanga barabarani, walivunja hadi geti la Uwanja wa Ndege kutaka tu kumuaga kiongozi wao.

 

 

Ndugu zangu tusiwe na vichwa vya kusahau haraka, tusimdharau mtu kwa kuwa tu ametoweka duniani. Uongozi ni kama kitabu kila mmoja ana ukurasa wake. Tangu awamu ya kwanza, ya pili hadi ya tano kila mtu amefanya kwa sehemu yake.

 

 

Yapo mambo ambayo yalikuwa yanaonekana hayawezekani lakini kwenye utawala wa Hayati Magufuli yaliwezekana. Nchi kujenga miradi mikubwa kwa fedha zake za ndani hili si jambo la dogo.

 

 

Nchi kufikia uchumi wa kati hata kama ni wa chini lazima tukubali kazi ilifanyika.

Nchi ilikuwa haina ndege hata moja, sasa hivi siko tisa na nyingine mbili tayari zimeshaagizwa. Hii ni historia. Kwenye kila kona ya nchi hii, ujenzi mkubwa wa miundombinu umefanyika na unaendelea kufanyika.

 

 

Nidhamu Serikalini hii ni ‘asante Magufuli’ tukubali au tukatae. Sheria za madini zilizokuwa kandamizi zimebadilishwa wakati wake. Umejengwa mpaka ukuta kule Mererani kulinda madini yetu yasitoroshwe kiholela hizi zote ni juhudi zake.

 

 

Rais Samia ndio kwanza anaanza kuunda safu mpya ya uongozi, anaanza kutuonesha dhamira yake hatupaswi kuibeza ile iliyopita. Unabeza ulipotoka ukiwa hujui unapokwenda? Tuwe waungwana, tumuunge mkono Rais Samia lakini tusimpuuze Hayati Magufuli.

Makala: Erick Evarist

Leave A Reply