The House of Favourite Newspapers

Tunachojifunza Mauaji ya Kimbari Rwanda – Part 01

WATANZANIA wengi hawajui nini kilisababisha mauaji ya Kimbari ya nchini Rwanda yaliyosababisha maelfu ya watu kuuawa. Naamini msomaji wa makala haya atajifunza kitu na kuona umuhimu wa mshikamano na amani tulionao hapa nchini. Tafadhali tuwe pamoja.

Mauaji ya Kimbari ya Rwanda ni mgogoro ambao vyombo vya habari vya Magharibi vimekuwa vikiuzungumzia kama kisa na mateso makubwa waliyoyapata watu, lakini wakati huo huo vinakwepa kulipa nafasi suala la kuzungumzia wahusika halisi wa kutokea mauaji hayo ya kutisha.

 

Leo tutaanza kwa kuangalia wasababishaji wa mauaji ya Kimbari yaliyotokea katika nchi hiyo ya katikati mwa Afrika, nchi isiyo na bahari (Land locked Country) na ambayo imezungukwa kila upande na nchi nyingine Tanzania ikiwemo.

Historia inaonesha kuwa mwaka 1918, Ubelgiji iliivamia nchi hiyo na kuanza kuifanya koloni lake na kuikalia kwa mabavu. Kabla ya hapo ilijulikana kwa jina la Rwanda-Urundi wakati ilipokuwa ndani ya makoloni ya dola jingine la Ulaya, yaani Ujerumani.

 

Mwaka 1933 Ubelgiji ilifanya sensa ya nguvu ya kuhesabu watu nchini humo na kumpa kitambulisho kila mkazi wa nchi hiyo. Ikiwa ni katika njama zake zenye malengo ya muda mrefu za kikoloni, wakoloni hao wa Ulaya waliwagawa Wanyarwanda kwenye vitambulisho hivyo katika makabila matatu; Wahutu, Watutsi na Watwa.

Wakoloni wa Ubelgiji hawakuwa na nia njema katika mgao huo. Walitumia mgao huo kuchochea hisia za kikabila nchini Rwanda. Waliwapa nguvu watu wa kabila la Kitusti walio wachache na kuwaonesha kuwa ni bora kiheshima na kwa kila kitu mbele ya makabila mengine mawili yaliyobakia, ikiwa ni kuandaa mazingira ya kuzuka ugomvi na vita vya wenyewe kwa wenyewe miaka mingi iliyofuata.

 

Miaka 20 tangu kufanyika njama hiyo mbaya, Watutsi wakawa wana nafasi nzuri zaidi katika upande wa elimu, kazi na nafasi za juu katika utawala ikilinganishwa na ndugu zao Wahutu na Watwa.

Hivyo wakoloni wa Ubelgiji wakawa wametengeneza tabaka moja jipya la watu huko Rwanda na kuwapachika jina la watu weusi walio kamili. Mfumo wa masomo wa mkoloni Mbelgiji ulitilia mkazo suala la kuwasomesha watoto wa machifu na wakuu wa kikabila waliojulikana kwa jina la Mwami na wingi wake Abami kwa ajili ya kujidhaminia nguvu kazi waliyohitajia.

 

Mgao huo wa kikabila, kijamii na kisiasa umeleta madhara makubwa nchini Rwanda tangu mwaka 1920 hadi leo hii na mpaka leo bado kuna chembechembe za hisia hizo za kiuadui.

Mgao huo uliwafanya Wahutu ambao ni wengi kuwaona ndugu zao Watutsi kuwa ni vibaraka wa wakoloni. Ndio maana, mwaka 1959, Wahutu waliamua kuanzisha vita dhidi ya Watutsi na Wabelgiji.

Huo ukawa mwanzo wa uhasama baina ya makabila hayo ndugu na ambao ulipata nguvu baada ya Rwanda kupata uhuru wake kutoka kwa mkoloni Mbelgiji mwaka 1962.

 

Mauaji ya Kimbari ya Rwanda yalikuwa mauaji ya halaiki na yalitokea takriban siku 100, tangu kuuawa kwa Rais Juvenail Habyarimana na walau watu 500,000 waliuawa, au karibu asilimia 20% ya idadi ya watu wote nchini Rwanda wakati huo.

Kuuawa kwa Habyarimana tarehe 6 Aprili 1994 kulikuwa chanzo muhimu cha mauaji ya kimbari nchini humo. Kuhusiana na kuuawa Habyarimana, Wahutu wenye misimamo mkali walihusisha tukio la kutunguliwa ndege yake na wapinzani wa Kitutsi na kulitumia kama shambulio na mauaji makubwa na ya kutisha kwa wenye misimamo ya wastani.

 

Machi 21, 1994 maeneo ya Uganda ambayo yanapakana na Rwanda, katika Ziwa Victoria serikali ilituma vikosi vya jeshi kudhibiti eneo hilo kwa hali ya dharura.

Agizo hili la serikali kutuma jeshi halikuwa kwa ajili ya kidhibiti eneo hilo kutoka kwa adui bali agizo lilikuwa ni kudhibiti eneo hilo dhidi ya maiti za binadamu.

 

Siyo maiti mbili au tatu, si mamia bali maelfu ya maiti za binadamu ambazo zilikuwa zinaingia ziwani Victoria zikiletwa na maji ya Mto Kagera.

Maiti hizi zilikuwa nyingi kwa maelfu kiasi kwamba mpaka zilikuwa zinafanya maji yatoe harufu.

Serikali ya Uganda ilituma jeshi eneo hili ili kudhibiti eneo hili maji yake yasitumiwe na wananchi kwa matumizi ya nyumbani au shughuli za uvuvi.

 

Lakini jeshi lilikuwa eneo hili ili kuhakikisha kuwa taharuki iliyozuka baada ya maelfu ya miili hii kuonekana haigeuki na kuvuruga amani katika eneo hili.

Lakini pia jeshi lilikuwa hapa ili kubaini miili hii ilikuwa inatoka wapi na kufunika mto?

Je, nini kilifuata? Fuatilia Jumanne ijayo.

KUTOKA MATAKBA | NA ELVAN STAMBULI 0655 339 616

Comments are closed.