The House of Favourite Newspapers

Tundu Lissu Amjibu Job Ndugai Kuhusu Matibabu Yake

Tundu Lissu (kushoto)na Job Ndugai.

MBUNGE wa Singida Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amefunguka na kumjibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuhusu kauli yake ya kusema kuwa utaratibu uliotumika kumsafirisha Tundu Lissu kwenda Nairobia ulikwenda kinyume na mfumo wa serikali na bunge.

 

Tundu Lissu anadai kuwa kauli hiyo haina ukweli hata kidogo kwani kitendo cha yeye kusafirishwa kwa ndege mnamo Septemba 7, mwaka huu majira ya usiku kuelekea katika matibabu nchini Kenya, ni wazi kuwa kibali kilitolewa na serikali pamoja na bunge kwani bila hivyo yeye asingeweza kusafirishwa.

 

“Mimi sikuamua kuja Nairobi, sikuwa najitambua, watu walioamua mimi kuja Nairobi ni pamoja na Spika Ndugai mwenyewe.  Watu wameniambia kwenye hicho kikao cha nipelekwe wapi Ndugai alikuwepo, naibu wake alikuwepo, Katibu wa Bunge wakati huo Kashilila alikuwepo, Mwenyekiti wa chama changu alikuwepo.  Ile ndege iliondoka saa sita usiku sasa ingerukaje kama haikuruhusiwa na serikali ya Tanzania kuruka kuja Nairobi? Kwa hiyo hii habari ya kwamba amepelekwa wapi ni mambo ya kujishikizashikiza tu ni Bunge kujaribu kukwepa wajibu wake wa kisheria,” alisema Tundu Lissu

 

Aidhaa Tundu Lissu aliendelea kufafanua kuwa: “Nimesema mimi siombi fadhila, hakuna mtu anaomba kufadhiliwa hapa, mimi naomba haki ambayo anatendewa mtu aliye mbunge anayeumwa na ambaye amelazwa nje ya kituo chake cha kazi.  Hicho tu.”

 

Mbali na hilo, Tundu Lissu amesikitishwa na upelelezi unaofanywa na jeshi la polisi kuhusu shambulio lake la kutaka kuuawa na kusema anashangaa mpaka leo jeshi la polisi halijasema linamshuku nani kuhusika na shambulio hilo na mpaka leo jeshi la polisi halijaweza kumhoji japo aweze kutoa maelezo yake.

 

Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi mnamo Septemba 7 mwaka huu akiwa mjini Dodoma na baadaye kupelekwa nchini Kenya jijini Nairobi kupatiwa matibabu ambapo mpaka sasa yupo huko kwa matibabu

Comments are closed.