Tusikubali ‘mabadiliko badiliko’ kabla ya ‘mabadiliko’

Ikiwa ni mara ya kwanza tangu kupatikana kwa uhuru, uchaguzi wa mwaka huu nchini umekuwa wa kipekee zaidi kwa upepo wa kisiasa  kuvuma kwa kasi kuliko chaguzi zote zilizopita, hii inatokana kuwa katika uchaguzi huu kumekuwa na mambo mbalimbali ambayo kwa kiasi fulani yamechangia morali ya wananchi kufuatilia masuala ya kisiasa kuwa kubwa.

Hapo zamani kidogo ilikuwa ni rahisi mtu kutoa kauli kama: ‘Sipendi siasa.’ au ‘Mambo ya siasa waachie wenyewe’, lakini sasa hivi kila mtu ameamka na kujihusisha na siasa moja kwa moja iwe kwa kuzungumzia, kwa kujiandikisha katika daftari la kudumu la kupiga kura, kwa kusikiliza sera za wagombea kwenye mikutano mbalimbali, kwa kushiriki kabisa ndani ya kinyang’anyiro hicho wengine kama wagombea wa ngazi mbalimbali za uongozi au kwa vyote kwa pamoja.

Lakini katika kile ambacho unaweza ukasema kwenye msafara wa mamba kenge nao wamo, pia katika upepo huu wa kisiasa, kumekuwepo kwa watu wengi wanaofuata mkumbo hasa kwa kujifanya wazungumziaji wa masuala ya kisiasa hata kama hawajui chochote ilimradi tu nao waonekane kama wanaendana na wakati.

Langu siyo hilo; leo ningependa nizungumzie neno ambalo nimelisikia likizungumziwa na watu wengi sana ambalo awali liliasisiwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi ‘Ukawa’ neno lenyewe ni ‘Mabadiliko’.

Neno hili limekuwa maarufu sana midomoni mwa watu hasa wafuasi wa Ukawa ambao japo kuwa wengi hawana uelewa mkubwa wa mambo ya siasa lakini nao wamelikariri neno hili na kuliweka akilini kiasi kwamba hata kama utakuwa na hoja gani dhidi yao, wenyewe watasimamia kuwa, wanataka mabadiliko huku wakionesha ishara ya kuzungusha mikono ikiwa ni tafsiri ya lugha ya ishara ya neno mabadiliko.

Kwa tafsiri ya Ukawa, neno mabadiliko linatajwa kusadifisha kusudio la vyama hivyo kutaka kubadilisha mfumo mzima wa utawala kwa kuanza na kuking’oa chama tawala madarakani. Kama hiyo haitoshi Ukawa wanaenda mbele zaidi kwa kulitumia neno hilo kama ‘slogan’ yao ya ‘Movement For Change’ na kuahidi kufanya mapinduzi ya kiuchumi na kijamii zaidi ya yale yaliyofanywa na chama tawala tangu kupatikana kwa uhuru.

Neno hili hatimaye likawa maarufu huko lakini baadaye neno hilo likahamia kwa mahasimu wao ambao ni chama tawala,

CCM, huko neno hilo likasadifishwa na tafsiri kubwa moja ambayo ni mabadiliko kwenye nyanja za uchumi na kijamii, lakini kwa kujipambanua kuwa mabadiliko hayo lazima yaanzie kwa mwananchi mwenyewe na chama kilichopo madarakani ambacho kupitia makada wake kimejinasibu kuwa na uwezo wa kufanya mabadiliko ndani ya chama kutokana na kuwa na wagombea wachapakazi hasa katika nafasi ya urais; huko slogan imekuwa ‘Magufuli For Change’.

Hofu yangu ni kwamba wakati wanasiasa hawa wakihubiri neno mabadiliko sisi wananchi inabidi tukae pembeni tukiwa na tafsiri imara ya Kamusi ya Kiswahili ‘TUKI’ inayotafsiri neno ‘Mabadiliko’ kama nomino yenye maana 1. badili 2. badilisha 3.geuza 4. geuka.

Kwa tafsiri hizo zote naamini sote tumeshuhudia neno hilo likitumika zaidi katika tafsiri ya namba 4 ambayo ni ‘geuka’. Neno ambalo ni kitendo cha mtu au kitu binafsi kubadili msimamo, muonekano au hali yake.

Hapa ndipo ambapo tumekuwa tukishuhudia wanasiasa wakibadilikabadilika yaani kugeuka kwa kuvihama vyama vyao huku wengine wakiwa wameshawatumikia serikali bila kufanya mabadiliko yoyote ya kimsingi, lakini kwa kubadilikabadilika kwao au kugeukageuka kwao wamehama na kutaka nafasi nyingine kupitia nguvu ya neno mabadiliko ili waendelee kujineemesha na keki ya Watanzania.

Ningependa kuwashauri Watanzania wanaotegemea kupiga kura Oktoba 25, mwaka huu, kuwapigia viongozi wanaohubiri neno mabadiliko kwa kulenga zaidi kufanya mapinduzi ya kiuchumi na kuongeza kasi ya maendeleo na kuwang’oa viongozi waliobadilikabadilika na wanaoendelea kubadilikabadilika ambao hawana historia yoyote ya kufanya mabadiliko wakati wa utumishi wao serikalini na kuwaweka viongozi ambao walionesha mabadiliko bila kujali chama cha siasa wanapotokea ili tusije tukajiingiza katika mtego wa kugeukwa na viongozi hao pindi tutakapowaweka madarakani kwa kuwa wanakasumba ya kubadilikabadilika au kugeukageuka.


Loading...

Toa comment