The House of Favourite Newspapers

Tusitengeneze Tatizo Makusudi

1

Tanzania's President elect John Pombe Magufuli addresses members of the ruling Chama Cha Mapinduzi Party (CCM) at the party's sub-head office on Lumumba road in Dar es Salaam, October 30, 2015. Tanzania's ruling party candidate, John Magufuli, was declared winner on Thursday of a presidential election, after the national electoral body dismissed opposition complaints about the process and a demand for a recount. The election has been the most hotly contested race in the more than half a century of rule by the Chama Cha Mapinduzi Party, which fielded Magufuli, 56, a minister for public works. REUTERS/Sadi Said Rais Dk. John Magufuli.

NCHI ilimaliza uchaguzi miezi saba iliyopita na sasa ipo katika mwendo wa kawaida kuhakikisha maisha ya Watanzania yanabadilika. Malumbano ya kisiasa ambayo yalikuwa ya kiwango cha juu kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya taifa hili, yalimalizika mara tu baada ya kuapishwa kwa Rais Dk. John Magufuli pale Novemba 5, 2015.

Siku chache tu baada ya Magufuli kuanza kazi, wazalendo wa kweli wa nchi hii walisahau tofauti zao kisiasa, wakaungana pamoja baada ya kiongozi huyo kuonesha kuwa ni mtu aliyejitolea kwa dhati ili kuwatumikia watu wote, hasa wanyonge.

Vitu alivyovifanya, vilisababisha aungwe mkono hata na watu ambao miezi michache nyuma walimuona adui na ambaye asingebadili lolote, hasa kwa kuwa wengi wanaamini chama tawala, CCM, kimekosa mbinu za kuinua hali ya maisha ya Watanzania ambao licha ya nchi yao kuwa na maliasili nyingi, lakini wanaishi maisha mabovu.

Uzalendo wake, chuki zake za wazi dhidi ya wabadhirifu, kudhibiti matumizi yasiyo na tija, mafisadi na uwajibikaji katika utumishi wa umma, ni vitu ambavyo vimemfanya kuwa nuru katikati ya giza nene ambalo lilikuwa limewagubika Watanzania ambao walifikia kipindi cha kuamini kuwa kama ataendelea na moto huo, uchaguzi ujao utakuwa rahisi mno kwa CCM kuliko wakati mwingine wowote tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi.

Lakini katikati ya mazuri haya, kuna mambo machache yanayofanyika, yanayoonesha kuwa mbele ya safari, kutatokea matatizo kama yasipodhibitiwa mapema.

Kuna kauli za viongozi zinazoonesha kuwa siasa zimekwisha, kilichobakia hivi sasa ni kazi tu. Ni jambo jema, kwamba tuache blahblah, tupige kazi. Kama ni hivyo, tunapozuia mikutano au mikusanyiko, tufanye hivyo kwa haki.

Haileti picha nzuri, mikutano na mikusanyiko inayolengwa ni ile ya wapinzani pekee, wakati hata wale wa chama tawala nao wanafanya. Maisha ni siasa, hauwezi kuvitenganisha hivi vitu.

Unapomzuia mwanasiasa kukutana na watu, maana yake hana sababu ya kuwepo. Inanikumbusha wakati f’lani Augustine Mrema alipokuwa akibebwa na wananchi kila alipoonekana, kutokana na wao kuwa na ‘mahaba’ naye.

Jambo lile lilionekana kuwakera wakubwa, wakampiga marufuku kubebwa, kana kwamba yeye alikuwa anaandaa watu ili wambebe. Lakini busara za Mwalimu Nyerere ndizo zilizomnusuru akaendelea kubebwa hadi wabebaji walipokuja kumshtukia, baada ya kuwataka polisi wamuache abebwe kama maiti.

Tunapozuia mikusanyiko ya wapinzani, tunatengeneza tatizo. Ni sawa na kujaribu kuyazuia maji katika mkondo wake, mwishowe yatasababisha mafuriko yanayoweza kuwa na hasara kubwa zaidi kuliko kuyaacha yapite katika njia yake ya kawaida.

Tusiwape wapinzani sababu ya kutafuta njia mbadala ya kukutana na watu wao, ambayo kwa vyovyote itakuwa haina afya kwa taifa. Tuwaache wakusanyike, waongee ilimradi wasivunje sheria tulizokubaliana. Ni wananchi ndiyo wataamua, kama wanachoambiwa kiko sawa au la, vinginevyo mikusanyiko hiyo itakufa yenyewe kifo cha kawaida.

1 Comment
  1. Urio says

    Ushauri mzuri mnoo na tena umeanza kwa maneno ambayo yanaleta mwanga. Big up!!

Leave A Reply