The House of Favourite Newspapers

Twiga Stars yachapwa na Zimbabwe, yazikosa Sh mil. 15

0

BBB-(2)Stumai Abdallah wa Twiga Stars akimdhibiti Emmaculate Msipa wa Zimbabaw leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.


TIMU ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania, Twiga Stars imeanza vibaya michuano ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kufungwa mabao 2-1 na Zimbabwe.

Twiga Stars inayofundishwa na Kocha  Nasra Juma ilipokea kipigo hicho jana kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo, Twiga Stars ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Mwanahamisi Omari ‘Gaucho’ aliyepiga shuti nje ya 18 lililomshinda kipa wa Zimbabwe, Chido Dzingira na kujaa wavuni.

Bao hilo la Twiga Stars halikudumu kwani Zimbabwe ilisawazisha dakika moja baadaye kupitia kwa Erina Jeke aliyefunga kwa kichwa.

Katika mchezo huo, timu zote zilishambuliana kwa zamu hadi zinakwenda mapumziko matokeo yakiwa ni sare ya bao 1-1.

Kipindi cha pili, mchezo huo ulianza kwa presha na Zimbabwe ilipata bao la pili katika dakika ya 46 mfungaji akiwa ni yule wa bao la kwanza, Erina. Mfungaji alitumia vyema uzembe wa mabeki wa Twiga Stars na kuunganisha krosi ya Eunice Chibanda.

Dakika ya 74 Twiga ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Maimuna Khamis na nafasi yake kuingia Fatuma Khatib, hata hivyo mabadiliko hayo hayakuweza kubadili kitu.

Kabla ya mchezo huo, Naibu Waziri wa Habari wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura aliahidi kutoa Sh milioni 15 kwa Twiga Stars endapo ingeshinda mechi hiyo.

Timu hizo zitarudiana baada wiki mbili nchini Zimbabwe.

Leave A Reply