The House of Favourite Newspapers

Uamuzi Kesi ya Tundu Lissu Kutolewa Leo

 MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam, leo Septemba 9, 2019, inatarajiwa kutoa uamuzi wa kesi ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) Tundu Lissu, dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai.

Pamoja na mambo mengine, Lissu ameiomba mahakama kutoa zuio la muda kwa mlalamikiwa wa kwanza, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai, kusitisha tukio la kumwapisha Mtaturu katika Mkutano wa Bunge ulioanza Jumanne iliyopita  jijini Dodoma.

Hata hivyo, kutokana na mahakama kuahirishwa jioni ya Agosti 29, mwaka huu bila kutoa uamuzi, bunge lilimwapishwa mbunge mpya wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu, kwa mujibu wa ratiba.

Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019, dhidi ya spika na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Lissu anaomba kibali cha kufungua shauri la maombi maalum ikiwamo kumtaka spika awasilishe mahakamani taarifa aliyoitoa bungeni ya kumvua ubunge ili iweze kupitiwa na mahakama na kufanyiwa maamuzi.

Kwa mujibu wa hati ya maombi hayo mlalamikaji anaomba mahakama kusitishwa uamuzi uliofanywa na spika.

Wakili Peter Kibatala alidai kuwa sababu kubwa ya kuomba kibali ni kutokana na kazi ya mahakama kupitia nyaraka kama zinafaa kusikilizwa kama mlalamikaji anavyoomba.

“Katika kipindi cha miaka saba iliyopita Lissu alikuwa anafanya kazi zake za uwakili wa wananchi vyema, lakini alishambuliwa kwa risasi na kutibiwa jijini Nairobi, nchini Kenya na baadaye akahamishiwa Ubelgiji,” alifafanua  huyo akisema Lissu hakuwahi kupewa taarifa za kutenguliwa ubunge.

Comments are closed.