The House of Favourite Newspapers

Uchaguzi 2020: Majina 5 CCM Yanayopewa Nafasi Urais Zanzibar

0

KAZI ya kutabiri kuhusu nani atabeba kijiti cha kuipeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar katika ngazi ya urais ingekuwa rahisi zaidi kama makamu wa sasa wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan angeonesha nia ya kukibeba kijiti hicho.

 

Aliweka wazi alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara visiwani Zanzibar mwishoni mwa mwezi Agosti, 2019 kuwa hana nia ya kugombea urais wa Zanzibar. Sababu aliyoitoa ni kuwa: “Katika kazi za uongozi kwa Tanzania mimi ni namba mbili, hivyo sina sababu ya kugombea urais wa Zanzibar ambao ni namba tatu.”

 

Rais wa sasa Dkt. Ali Mohamed Shein anamaliza miaka yake kumi ya kuiongoza Zanzibar, nchi ya visiwa na yenye mamlaka ya ndani pekee. Kwa mazingira hayo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu CCM inahitaji kuwa na mgombea mpya wa kiti cha Urais.

 

Kabla ya swali la nani ataibeba bendera ya CCM. Kwanza ni muhimu kuzielewa siasa za ndani za chama hicho kikongwe unapofika wakati wa kumtafuta mwakilishi wao Zanzibar. Watangaza nia wa kiti cha urais hugawika katika makundi mawili. Wale wenye ushawishi mkubwa Zanzibar lakini ushawishi wao ni mdogo bara na wale wenye ushawishi pande zote za muungano.

 

Kamari ya kisiasa inaonesha wale wenye ushawishi pekee Zanzibar wana uwezekano finyu wa kupitishwa. Na wale wenye ushawishi pande zote mbili huhesabiwa kuwa nafasi kubwa kupita katika vikao vya juu vya CCM Dodoma. Ingawa siasa zinabadilika muda wowote.

 

Jambo jingine muhimu kulielewa, CCM ya sasa haipendelei kuwa na mgombea anayeegemea siasa kali za kihafidhina. Siasa za chuki na ubaguzi zimeleta mparaganyiko mkubwa ndani ya Zanzibar kwa miaka mingi. Zinaonekana kutokuwa na tija kwa ustawi na maslahi ya chama hicho visiwani.

 

Lakini ukiacha hao na kuangalia upande mwingine wa shilingi, wale wenye siasa za kujitegemea na wasiotaka kuburuzwa, nao hawana nafasi kubwa ya kupita, kwa sababu CCM ya sasa haitaki historia ya akina Aboud Jumbe ijirudie. Kwa maneno mengine ni kusema, chama hicho kinahitaji zaidi mtu mwenye siasa za utiifu.

 

Nani anatazamiwa kuiongoza CCM Zanzibar?

Prof. Makame Mbarawa

Ni msomi katika fani ya Uhandisi wa Baharini. Alitumia muda wake mwingi katika nchi za Urusi, Australia na Afrika Kusini kwa masomo na kazi. Ukirudi nyuma muongo mmoja utakuta Prof. Mbarawa hakuwa mtu aliyejuuliakana katika medani ya siasa za Tanzania.

 

Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete, ndiye aliyemtambulisha Mbarawa kisiasa baada ya kumteuwa kuwa mbunge na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.

 

Katika awamu hii ya Rais John Pombe Magufuli, Prof. Mbarawa ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji. Anatajwa katika wale walio mstari wa mbele kuibeba bendera ya CCM Zanzibar katika kiti cha urais. Na karata yake kubwa ni utiifu.

 

Dkt. Hussein Mwinyi

Ni Mbunge wa jimbo la Kwahani, Zanzibar na Waziri wa Ulinzi katika serikali ya muungano. Huyu ni mtoto wa Rais mstaafu wa awamu ya pili ya serikali ya Jamhuri ya Mungaano wa Tanzania, Mzee Ali Hassan Mwinyi.

 

Katika nyakati hizi zenye vijana wengi wanao hoji mara kwa mara maslahi ya Zanzibr katika Muungano na Tanganyika, Dkt. Mwinyi ambaye ni tabibu kitaaluma, anaonekana kuwa kichwa muhimu kuipeperusha bendera ya CCM Zanzibar, si kwa sababu tu ya siasa zake za utiifu, pia ni kwakuwa uhusiano wake kisiasa na kidamu uko pande zote mbili za muungano.

 

Yuko katika shughuli za kisiasa tangu mwaka 2000, hapa ni kusema sio mgeni katika uwanda wa siasa za Tanzania. Ametumikia nafasi ya ubunge pande zote za Muungano, alikuwa Mbunge katika jimbo la Mkuranga, mkoa wa Pwani kabla ya kuwa Mbunge wa Kwahani. Hii ina maana safari yake ya kisiasa inafanana na ya baba yake aliyetumikia nafasi ya urais pande zote za Muungano.

 

Meja Jenerali Issa S. Nassor
Hili ni jina geni katika masikio ya wengi panapohusika siasa za Tanzania, lakini sio geni katika uwanja wa kijeshi.

 

Jenerali Nassor amelitumikia Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa miaka mingi kabla ya kuteuliwa kuwa Balozi nchini Misri kutoka mwaka 2017 hadi 2019.

 

Japo si jina kubwa katika siasa, duru visiwani Zanzibar zinamuelezea kama mtu asiye na mafungamano na siasa za makundi. Naye anatajwa kubebwa na karata ya utiifu wake lakini hana umaarufu katika siasa za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

 

Hatima ya nafasi yake ikiwa ataingia katika kinyang’anyiro itaamuliwa na CCM yenyewe.

 

Dkt. Mahadhi Juma Maalim
Alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Kuwait. Kabla ya hapo alikuwa Mbunge wa jimbo la Muyuni, Zanzibar 2010-2015. Pia amehudumu kama Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati wa utawala wa Dkt. Kikwete.

 

Kitaaluma ni mwanasheria na mwandishi wa habari. Anatajwa kuwa na siasa safi lakini ushawishi wake kisiasa bado ni mchanga kwa pande zote za jamuhuri. Licha ya mazingira hayo naye anatajwa kuwa miongoni mwa wenye nia ya kuwania nafasi ya kuiwakilisha CCM Zanzibar katika ngazi ya urais.

 

Mohammed Abood Mohamed
Kwa sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar. Ni mzoefu wa siasa za Tanzania, ameanza siasa tangu mwaka 2000. Amehudumu katika Wizara za muungano na zile za Zanzibar. Pia, amehudumu akiwa Mbunge katika Bunge la Tanzania na mwakilishi katika baraza la wawakilishi Zanzibar.

 

Kitaaluma amesoma masomo ya biashara. Uzoefu wake wa kuhudumu katika serikali zote mbili unamuweka katika nafasi ya ushindani katika mchuano huu. Siasa zake ni za utiifu lakini ushawishi wake mkubwa kisiasa unabaki katika mipaka ya Zanzibar.

 

Siasa za CCM ya Zanzibar huamuliwa Dodoma’. Huo ni msemo maarufu sana katika medani ya siasa za visiwani. Wakati huu ambao CCM imeshatoa ratiba kamili kuhusu mchakato wa kumpata mgombea wa nafasi ya urais na nafasi nyingine, kusubiri hatima ya majina hayo na majina ya watangaza nia wengine ndio jambo pekee muhimu.

CREDIT: BBC SWAHILI

Leave A Reply