The House of Favourite Newspapers

Uchaguzi Zanzibar; wapiga kura wagawanyika

0

151025111302_tanzania_woman_zanzibar_512x288_bbcMwananchi wa Zanzibar akipiga kura.

Stori: Mwandishi Wetu, Zanzibar

UCHAGUZI wa marudio uliofanyika jana Machi 20, Zanzibar umegawa wapiga kura kwani wapo waliodai kujitokeza kupiga kura licha ya vyama vyao kupinga marudio ya uchanguzi huo na wengine msimamo wao kubaki majumbani, Ijumaa Wikienda limegundua.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kisiwani Unguja umebaini kuwa, maeneo mbalimbali mjini hapo kumekuwa na ulinzi wa polisi hali iliyoashiria kuwepo kwa tahadhari.

Maeneo kama Michenzani, Mji Mkongwe, Mkunazini, Marikiti, Darajani, Magomeni, Uwanja wa Ndege, Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na Daraja Bovu, askari polisi walionekana wakifanya doria kuimarisha ulinzi wakati wa zoezi la kupiga kura.

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdani Omar Makame alipoulizwa kuhusiana na ulinzi huo alisema hilo ni jambo la kawaida.“Hili ni jambo la kawaida, tunapaswa kulinda raia na mali zao… ni jukumu la majeshi yote bila kujali mipaka ya kimajukumu,” alisema Makame.Mwananchi mmoja aliyekataa kutaja jina lake lakini huku akidai kuwa ni mfuasi wa Chama Cha Wananchi (CUF), alisema licha ya viongozi wake kuwakataza kupiga kura, yeye aliamua kupiga kwa sababu ni haki yake ya msingi.

“Mimi kupiga kura ni haki yangu ya msingi na ya kikatiba. Sijakubaliana na walichosema viongozi wangu wa CUF kwa sababu ni haki yangu ya msingi na kikatiba,” alisema mtu huyo akiwa Mkunazini.
Uchaguzi wa Zanzibar ulipangwa kurudiwa Machi 20, mwaka huu baada ya ule uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana kufutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jecha Salum Jecha kwa madai kuwa, kulikuwa na kasoro nyingi.

Nafasi zilizokuwa zikirudiwa kwa kura ni kumchagua Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani. Oktoba 25, mwaka jana walipiga kura ya Rais wa Tanzania na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Leave A Reply