The House of Favourite Newspapers

Kijana Adaiwa kufa, Azikwa, Apatikana Akiwa hai

1

Simiyu: Mshtuko! Kijana Nyabongo Manosa (22) mzaliwa wa Mwabuma wilayani Meatu mkoni Simiyu, anayedaiwa kufariki dunia mwaka 2013 kisha akazikwa, ameibua sintofahamu ya aina yake baada ya kupatikana akiwa hai.
Kwa kawaida, mtu akishafariki dunia na kuzikwa ni vigumu kumuona akiwa hai lakini kwa Nyabongo hali hiyo ilikuwa tofauti baada ya kupatikana akiwa hai ambapo baba yake mzazi amelisimulia Ijumaa Wikienda kisa na mkasa:
“Nyabongo alizaliwa mwaka 1991 katika Kijiji cha Mwabuma wilayani Meatu, alisoma shule ya msingi na sekondari kijijini hapa lakini hakufanikiwa kuendelea na masomo hivyo aliamua kufanya biashara ya viatu.

“Baada ya kupata mafanikio, alioa na kujaliwa mtoto mmoja. Baadaye alipatwa na homa iliyomsumbua kwa mwezi mmoja.
“Nilihangaika naye sana, kila hospitali tuliyokwenda madaktari hawakutoa majibu kamili.
“Mwili wake uliendelea kudhoofika siku hadi siku na ilipofika Juni 6, 2013, alifariki dunia katika Kituo cha Afya wilayani Kishapu.

“Tulifanya taratibu za kusafirisha mwili hadi kijijini Mwabuma na kuupumzisha katika makaburi ya familia.
“Baada ya hapo maisha yaliendelea, miaka miwili na zaidi, nilishangaa kupokea simu kutoka kwa jamaa yangu aishiye Kijiji cha Masubwe akisema kuna watu watatu waliokuwa wamekufa lakini wamepatikana akiwemo mwanangu (Nyabongo).

“Nilishtuka sana, nilidhani ni utani kwani haikuwa rahisi kukubali, ninavyojua mtu akishakufa na kuzikwa ndiyo inakuwa imeishia hapo. Nilijiuliza imekuwaje apatikane akiwa hai wakati nilishiriki kila kitu katika kifo chake na kaburi lake lipo?
“Simu zilizidi kupigwa na watu mbalimbali wakiniambia Nyabongo amepatikana na amepelekwa kituo cha polisi.

“Ilibidi nimtume mtoto wangu kwenda kumtambua, alipofika alimtambua ndipo nikaamini taarifa hizo na kweli nilipokwenda nilimuona mwanangu akiwa hai.”
Kwa upande wake Nyabongo, huku akiwa hawezi kuzungumza vizuri, aliliambia gazeti hili kuwa alifanywa msukule na mtu aliyedai alikuwa mfanyabiashara mwenzake (jina tunalo).

“Nakumbuka siku moja huyo mfanyabiashara alininunulia chakula, zilipita siku kadhaa, nikaanza kuumwa, sikujua kilichoendelea ila nilijikuta nipo sehemu ambayo hata siijui. Niliambiwa hapo ndipo nitakuwa naishi na wenzangu niliyowakuta,” alisema kijana huyo.

Akiendele kueleza kwa kusitasita, Nyabongo alisema walikuwa wanakula pumba, nyama na vyakula vingine ambavyo havijui walivyokuwa wakipelekewa na mwanamke.
“Tulipokuwa mle ndani, niliwaeleza wenzangu kuwa nimechoka kula hivyo vyakula hivyo bora niende kwetu lakini wenzangu walikuwa hawanijibu.

“Siku moja yule mwanamke aliacha mlango wazi ndipo nikatoka, nilivyoona mazingira tofauti nilirudi ndani kwani sikujua kilichoendelea hadi nilipomuona baba yangu.
Nashangaa kusikia nilikufa,” alisema kijana huyo ambaye kwa sasa anaendelea vizuri japokuwa hajaanza kufanya kazi yoyote.

1 Comment
  1. Nsolo S. Stephen says

    Hapa sijui tusemeje, ni maajabu ya Mungu au maajabu ya Binadamu?

Leave A Reply