The House of Favourite Newspapers

Ufafanuzi Kuhusu Rais Samia Kuitwa Amiri Jeshi au Amirat

0

SIKU chache baada ya kuibuka utata wa matumizi ya maneno ‘amiri’ na ‘amirat’ kutokana na Tanzania kupata Rais mwanamke kwa mara ya kwanza, Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limetoa ufafanuzi kuhusu maneno hayo.

 

Ibara ya 33(1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, inabainisha kwamba kutakuwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano, ambaye atakuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu.

 

 

Hata hivyo, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuapishwa kushika nafasi hiyo kubwa zaidi ya uongozi nchini, kuliibuka utata katika matumizi ya neno ‘amiri’, hoja kuu ikiwa ni kwamba neno hilo linatumika kwa mwanaume na kwa mwanamke anapaswa kuitwa ‘amirat’.

 

 

Baraza hilo kupitia kwa Katibu Mtendaji wake, Consolata Mushi, lilibainisha kuwa neno ‘amiri’ limechukuliwa kutoka lugha ya Kiarabu na halina mgawanyo wa kijinsia.

 

 

“Haina tofauti kati ya mwanamume na mwanamke, wengi wamekuwa na maswali. Unapochukua neno katika lugha uliyoichukua maana yake haiwi mbali katika ile maana ya msingi ya lugha yako.

 

 

“Amiri Jeshi Mkuu maana yake unamzungumzia kiongozi mkuu, yaani ni kiongozi mkuu wa jeshi, ambaye anasimamia majeshi yote nchini. Ana mamlaka ya kusimamia majeshi hayo. Tulilichukua kwa lengo moja, si kuligawanya kijinsia.

 

 

“Haina tofauti kati ya mwanamume na mwanamke, wengi wamekuwa na hili swali. (Mwandishi) si wa kwanza kuuliza hili swali, kwamba aitwe amirat? Hapana!

 

 

“Tulipolichukua neno ‘amiri’, tulimchukua kwa maana mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama. Hatukuchukua kama Kiarabu, amiri ni kwa wote. Awe mwanamume au mwanamke,” alisema Mushi.

 

 

Alisema neno hilo linabeba maana moja kwa lugha ya Kiswahili na jamii inapaswa kuzingatia uongozi uliopo na cheo chake na si kuangalia neno lilikotoholewa na jinsia.

 

 

Kumekuwa na maswali kwenye mitandao ya kijamii kuhusu namna ya Rais Samia atakavyoitwa kijeshi huku baadhi ya vyombo vya habari vikianza kutumia neno ‘amirat’ kwa kiongozi huyo.

Leave A Reply