The House of Favourite Newspapers

UFISADI TRIONI MOJA…LUGOLA TAA NYEKUNDU JELA YAWAKA

0

UNAWEZA kusema jela inaweza kuanza kumuita aliyekuwa Waziri wa Mambo wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola baada ya Rais Dk John Magufuli kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza mkataba tata wenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni moja uliosababisha waziri huyo kutumbuliwa.  Lugola pamoja na viongozi wengine wa wizara hiyo akiwamo aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye walidaiwa kutia saini makubaliano ya zabuni ya kununua vifaa vya zimamoto na uokoaji vyenye thamani ya Euro milioni 408.5 (sawa na zaidi ya Sh trilioni 1) kutoka kampuni moja ya nje bila kufuata sheria pamoja na kuidhinishwa na Bunge.

Rais Magufuli alichukua maamuzi ya kuwafuta kazi Januari 23 mwaka huu wakati akizindua nyumba za makazi ya askari Magereza, Ukonga jijini Dar. Licha ya Lugola na Andengenye kuwatumbua katika nafasi zao, pia alikubali barua ya kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu na kubainisha wazi kuwa mkataba huo walioingia ulikuwa wa ovyo kabisa.

WANASHERIA WANENA JELA INAWAITA

Kutokana na agizo hilo, baadhi ya wanasheria waliozungumza na UWAZI, wamebainisha kuwa hatua hizo zikibainisha tuhuma zao zinaweza kumuingiza hatiani Lugola pamoja na wenziye kutokana na makosa ya jinai yanayohusishwa na rushwa kubwa.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Jinai, iwapo Lugola alishiriki katika mchakato wa kusaini mkataba huo kwa nia ya kujinufaisha binafsi na kiwango cha fedha kuanzia Sh bilioni moja na kuendelea, anaweza kukumbana na kifungo cha miaka 15 jela na kufilisiwa.

“Kwa sababu wanachoangalia ni kiwango cha rushwa, suala hili la jinai lazima litaenda mbele zaidi hadi kubaini kiwango cha rushwa ambacho anadaiwa amechukua au alitarajiwa kuchukua, kwa hiyo kama ni rushwa kubwa kifungo ni kuanzia miaka 15 na faini pamoja na kufilisiwa.

“Lakini pia kama atakutwa na hatia ya kutumia madaraka vibaya kama hivyo kutoshirikisha Bunge wala Baraza la Mawaziri, tayari adhabu yake ameshaipata ambayo ni kuwajibishwa katika nafasi ya uwaziri. Ila sasa kwa kuwa Takukuru wameagizwa na rais kuchunguzwa, upo uwezekano wa kufika mbali hadi kwenye makosa ya jinai,” alisema.

Hoja hiyo iliungwa mkono pia na aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo Bisimba ambaye alisema mbali na makosa ya jinai, inaweza kwenda mbali zaidi hata kwenye utakatishaji fedha.

MKATABA WA OVYO

Januari 23 mwaka huu, wakati akizungumza katika uzinduzi wa nyumba hizo, Rais Magufuli alisema viongozi wa wizara hiyo walitia saini makubaliano ya zabuni ya kununua vifaa vya zimamoto na uokoaji vyenye thamani ya Euro milioni 408.5 (sawa na zaidi ya Sh trilioni 1) kutoka kampuni moja ya nje bila kufuata sheria.

“Kulikuwa na mkataba wa ovyo unaotengenezwa Wizara ya Mambo ya Ndani wenye thamani ya Euro milioni 408. “Umetayarishwa na kusainiwa na Kamishna Jenerali wa Zimamoto, haujapangwa kwenye bajeti, haujapitishwa na Bunge.

“Wakati wa vikao na kampuni moja ya Romania, wahusika wa Tanzania walipokuwa wanakwenda kwenye majadiliano wanalipwa ‘seating allowance’ (posho ya vikao) ya Dola 800 (Sh 1,832,170) na hata tiketi za ndege walilipiwa.

“Yanayokwenda kununuliwa kule kwenye mkataba ni ya ovyo, ni ya ajabu kabisa, ukitaka kuuvunja, yale ambayo yameshaanza kutekelezwa lazima yaendelee kutekelezwa,” alisema Rais Magufuli. Pia alisema maofisa wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliohusika kupitisha makubaliano hayo wajitafakari.

Maofisa hao wanadaiwa kupitisha makubaliano hayo wakati Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Profesa Andelardus Kilangi alipofiwa na mkewe. Alisema licha ya kwamba Lugola alikuwa ni mwanafunzi wake wakati akifundisha Shule ya Sekondari Sengerema, lakini hafai kuendelea na wadhifa huo.

“Nakueleza Lugola, Kamishna Jenerali (Thobias Andengenye) ninawashangaa kuona mko hapa, sitaki kuwa mnafiki, trilioni moja na zaidi mnasaini wakati sheria zote zinajulikana. “Kwa hiyo mwanafunzi wangu Lugola nasema kwa dhati nakupenda sana, lakini kwenye hili hapana. “Umenisifia sana hapa nakushukuru, lakini kwenye hili hapana, ni lazima niwe mkweli,” alisema Rais Magufuli.

Alisema wapo wanaohusika kwenye wizara hiyo, hasa kitengo cha Zimamoto, hivyo akawataka wasaidizi wa Andengenye wajitathmini. “Andengenye nampenda sana ni mchapakazi, umejenga nyumba mpaka Chato, lakini kwenye hili hapana, nilitegemea asiwepo hapa.

“Unakwenda Ulaya unasaini mradi ambao haujapitishwa hata na Bunge… ‘no’, nitaendelea kuwapenda, lakini kwenye ‘position’ hii ‘no’,” alisema Rais Magufuli.

Waziri wa tatu mambo ya ndani kutumbuliwa na JPM Lugola amekuwa waziri watatu kutumbuliwa na Rais Magufuli katika kipindi cha miaka minne tangu aingie madarakani na amehudumu kwenye wizara hiyo kwa mwaka mmoja na miezi sita na siku 23 tangu Julai Mosi mwaka juzi alipoteuliwa kushika wadhifa huo baada ya mtangulizi wake, Mwigulu Nchemba kutumbuliwa.

Anakuwa waziri wa tatu kuondolewa katika wizara hiyo tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, baada ya Charles Kitwanga na Mwigulu.

Kitwanga aling’olewa Mei 20, 2016 kwa tuhuma za kuingia bungeni akiwa amelewa na Mwigulu aling’olewa Julai Mosi 2018, kwa kushindwa kushughulikia azimio la Bunge kuhusu suala la kufunga mashine za kielektroniki za utambuzi wa alama za vidole (Afis) katika vituo 108 vya polisi, mradi uliofanywa na Kampuni ya Lugumi kwa gharama ya Sh bilioni 37.

 

HABARI; Mwandishi Wetu, Uwazi

Leave A Reply