The House of Favourite Newspapers

Ugomvi wa Aboud Jumbe na Nyerere ulivyotetemesha nchi-13

0

Tunaendelea kuchambua mgogoro wa Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Pili wa Zanzibar, Aboud Jumbe:

Uteuzi wa mtu atakayemridhi Mwalimu Julius Nyerere uligawa wajumbe wa mikutano ya CCM mjini Dodoma na gumzo lilikuwa ni ama Ali Hassan Mwinyi au Dk. Salim Ahmed Salim.

Hoja yao ilikuwa kwamba, kumruka Mwinyi aliyekuwa Makamu wa Rais na Makamu Mwenyekiti wa CCM na kumteua Dk. Salim Ahmed Salim, kungetafsiriwa vibaya ndani na nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kwamba, Watanzania hawakuwa na mipango thabiti ya kuandaa watawala na kurithishana madaraka.

 Isitoshe, Mwinyi angejiona vibaya kwa kurukwa. Kwa njia hii, Mwinyi akaibuka mshindi kama pendekezo la Kamati Kuu ya CCM (CC)  kwenda Halmashauri Kuu ya Taifa  (Nec) kwa uteuzi wa mwisho.

Mwalimu Nyerere, aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao, hakupinga, pengine kwa kutarajia kwamba Nec ingembeba Dk. Salim.

Ilipofika uteuzi wa mgombea kiti cha Rais wa Zanzibar, baada ya kupendekeza kwa sauti moja, jina la Idrisa Abdul Wakil, ambapo wanamstari wa mbele walimpendekeza Maalim Seif Sharrif Hamad.

Mapendekezo ya CC yaliwasilishwa Nec Agosti 15, 1985 kwa uteuzi wa mwisho.  Kwenye kikao hicho, kambi ya wanamstari wa mbele ilipata mtetezi ambaye ni Shehe Thabit Kombo, rafiki mkubwa wa Nyerere; aliyewasilisha hoja kwamba, kumtoa Mwinyi Zanzibar ili awe Rais wa Muungano, kungevuruga hali ya amani na utulivu aliyosaidia kujenga na kusimika katika uongozi wake wa miezi 18 tu visiwani.

Kauli ya Shehe Thabit Kombo ilimezwa kwa sauti za kupinga za wajumbe wa Nec kutoka Bara, kuonesha kwamba Paul Bomani na mama Getrude Mongela hoja zao zilipenya vyema kwa wajumbe.

Mwalimu Nyerere akaahirisha kikao kwa muda, akawaita pembeni wasiri wake wachache, wakiwamo Mwinyi, Kawawa na Kombo; wote hao, wakateta.

Kikao kiliporejea, SheheThabit Kombo alikuwa amegeuka, alimuunga mkono Mwinyi.

Kwa mara ya kwanza alimuunga mkono Wakil, kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar. Kura zilipopigwa ni kura 14 tu kati ya 1,746 zilizomkataa Mwinyi.

Kwa upande wa Zanzibar, ambapo ni wale wajumbe 163  wa Nec kutoka Zanzibar waliokuwa na haki ya kupiga kura kwa uteuzi wa Rais wa Zanzibar, Wakil alipata ushindi mdogo wa kura 85 dhidi ya 75 za Maalim Seif Sharrif Hamad.

Itaendelea wiki ijayo.

Leave A Reply