The House of Favourite Newspapers

Nilifanya Mapenzi na Maiti 20 Ili Nitajirike -2

0

ILIPOISHIA

“Baba, hizi dharau zitakwisha lini?” nilimuuliza baba.

“Mpaka tutakapokuwa na fedha Zakia,” alinijibu.

“Na hizo fedha tutazipata lini?”

“Sijui, cha msingi tuvumilie, kuna siku Allah atafanikisha jambo,” aliniambia baba, uso wake ukajawa na tabasamu pana, tabasamu la kuniridhisha, ila kwa kupitia macho yake, niliona ni jinsi gani alikuwa na maumivu moyoni mwake.

ENDELEA NAYO…

Siku ziliendelea kwenda mbele. Maisha yalizidi kutupiga na kila siku iliyoingia nilisema afadhali ya jana. Moyo wangu ulikuwa kwenye maumivu makali kwa ajili ya vitu viwili tu, kitu cha kwanza ni kwa jinsi familia yetu ilivyotafunwa na umaskini lakini kitu cha pili kilikuwa ni jinsi wanaume waliotaka kunioa kuniacha na kuwafuata wanawake wengine.

Baada ya kuona kwamba maisha yanakuwa magumu sana ndipo nilipoamua kuwaita wazazi wangu na kuwaambia kwamba nisingeweza kuishi kijijini kwa sababu hakukuwa na kitu kilichobadilika kwa miaka yote, hivyo nilitaka kuondoka kuelekea jijini Dar es Salaam.

Wazazi wangu hawakukubali kabisa, waliniambia kwamba mjini hakukuwa kuzuri, kulikuwa na wanawake wengi waliokwenda huko lakini kutokana na ugumu wa maisha waliishia kujiuza tu. Niliwaambia kwamba nisingeweza kufanya hivyo bali nilitaka kwenda huko na kutafuta fedha kwa njia halali kabisa.

“Haiwezekani…” alisema baba huku akionekana kukasirika.

“Baba! Siendi kufanya biashara ya kujiuza, nakwenda kutafuta fedha,” nilimwambia kwa sauti ya kulalamika.

“Utafikia wapi? Mjini hatuna ndugu yeyote, wewe utaishi kwa nani?” aliniuliza huku akiniangalia machoni.

“Nitafikia kwa rafiki yangu!”

“Nani?”

“Sikujua…”

Japokuwa niliwaambia hivyo lakini hawakutaka kuniruhusu. Moyo wangu ukakosa furaha, nilikasirika sana kwani niliamini nilikuwa binti mkubwa ambaye nilitakiwa kuondoka nyumbani na kwenda kutafuta maisha yangu.

“Baki nyumbani Zakia, mbona hapa unakula na kulala bure, huko mjini hakuna maisha. Mwenzako Zubeda alikwenda huko, kilichomtokea nadhani unakijua, achana na huyo, kuna Hawa, Mwamvita, wote walitokewa na mabaya, kwa nini uende huko?” aliuliza mama huku naye akiniangalia usoni kwa macho yaliyoonesha dhahiri hawakutaka niondoke pale kijijini.

Sikuzungumza kitu chochote kile, kama kuomba, niliwaomba ila walinikatalia hivyo nilichokifanya ni kusuka mipango yangu ya kutoroka. Sikutaka kuonekana mnyonge, wangeweza kushtuka kile kilichokuwa akilini mwangu wakati huo, niliwaonesha tabasamu pana huku nikiwa mchangamfu kana kwamba hakukuwa na kitu kilichoniumiza.

Baada ya siku nne tu, sikutaka kubaki pale kijijini, umaskini ulitutesa na hivyo njia ya kupata fedha na kuwa milionea niliiona ni kutoroka tu, hivyo nikafanya hivyo. Siku ambayo nilitoroka, niliamka saa kumi alfajiri hata kabla ya mtu yeyote kuamka nyumbani, nikachukua nguo zangu chache na kuziweka katika begi langu chakavu, nikaanza kunyata, nilipoufikia mlango, nikaufungua na kuanza kukimbia.

“Ninaondoka nikiwa maskini, nitarudi nikiwa tajiri…” nilisema huku nikikimbia kwa kasi kuelekea porini.

Kulikuwa na giza lakini sikuogopa hata kidogo, nilikuwa nikikimbia kuelekea upande wa kusini kulipokuwa na Lupiro. Kulikuwa na umbali kama kilometa ishirini kutoka kijijini kwetu lakini sikutaka kukata tamaa, niliendelea kukimbia, nilipochoka, nilipumzika na kuendelea na safari.

Baada ya saa kama nne, nikaanza kuingia katika kijiji hicho ambapo kulikuwa na kituo cha daladala ndogo (hiace) zilizokuwa zikielekea Ifakara mjini. Sikuwa na pesa yoyote mfukoni mwangu ila niliamini kwa kutumia jinsi yangu, ingekuwa kazi rahisi sana kumlaghai hata utingo.

“Za saa hizi kaka!” nilimsalimia utingo.

“Poa! Karibu mrembo!” aliniambia.

Kitendo cha kuniita mrembo tu kilinipa uhakika wa kufanikiwa kile nilichokuwa nikikitaka. Nilikuwa mzuri wa sura na hata umbo langu lilivutia, akawa ananiangalia kwa macho niliyoyaelewa nini alihitaji, na nilichokifanya ni kuanza kuunyonganyonga mwili wangu.

“Mbona huongei jamani? Tatizo nini?” aliniuliza huku akinisogelea.

“Nataka kufika Ifakara mpenzi!” nilimwambia kwa sauti ndogo.

“Hakuna tatizo! Mbona poa tu…”

“Ila kuna tatizo!”

“Tatizo gani?”

“Sina nauli!’ nilimwambia.

Kwanza akatoa tabasamu pana, nilihisi alifurahia sana kusikia hivyo kwani ndiyo ilikuwa njia nyepesi kwake kukamilisha lengo lake. Akaniambia kwamba hakuna tatizo lolote lile, angenisaidia mpaka kufika huko Ifakara kwani ndiko anakoishi.

“Nitakupeleka bure kabisa….una ndugu huko?” aliniuliza.

“Sina.” Nikamjibu, akaongeza tabasamu zaidi.

Alichokifanya ni kunipokea begi langu na kunipeleka ndani ya daladala lile. Nilikaa huku nikiwa najifikiria ni kitu gani kingetokea mara baada ya kufika Ifakara. Nilipomwangalia utingo ambaye nilimsikia dereva akimuita kwa jina la Mudi, muda wote alionekana kuwa mwenye furaha tele.

Je, kiliendelea nini? Usikose kufuatia Jumanne ijayo.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

Leave A Reply