The House of Favourite Newspapers

Ugonjwa Wa Kwashiorkor Na Mapafu Kwa Watoto

0

1. KWASHIORKOR Unyafuzi au Kwashakoo (Kwashiorkor) kama wengi walivyozoea kuuita, ni ugonjwa unaowakumba watoto wadogo, kutokana na ukosefu wa lishe bora hasa protini. Mara nyingi ugonjwa huu huwapata watoto wanaotoka kwenye familia za kimaskini, au wanaoishi kwenye maeneo yenye njaa. Dalili za awali za ugonjwa
huu, ni mtoto kudhoofika sana, kuvimba miguu, tumbo kuwa kubwa, nywele kuwa nyembamba na kunyonyoka, kung’oka meno bila mpangilio, rangi ya ngozi kubadilika na kutokwa na mapunye mengi.

 

Mtoto mwenye kwashakoo hukosa raha, mwili hukosa nguvu na hulialia ovyo na kama asipopata matibabu, husababisha kudumaa kwa
mwili na akili na mwisho mtoto hufa.

 

Utafiti unaonesha kuwa kukosa elimu ya lishe kwenye baadhi ya familia, ndiyo chanzo kikubwa cha tatizo hili ambalo linatajwa kusababisha sana vifo vya watoto barani Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara.

 

MATIBABU Kwa kuwa ugonjwa huu husababishwa na ukosefu wa lishe bora, hasa Protini kama tulivyoona, matibabu yake huhusisha kuanza kumpa mgonjwa lishe kamili, ikiwa ni pamoja na kumtundikia dripu za protini kwa mtoto ambaye hali yake ni mbaya na hawezi kula. Pia matibabu ya magonjwa mengine yaliyoambatana na kwashakoo, kama mapunye huenda sambamba na lishe bora kwa mtoto. Mtoto akishaanza kupata nguvu, anatakiwa kuanza kupewa mlo kamili, angalau mara tatu kwa siku.

 

Baadhi ya vyakula vyenye protini kwa wingi, ni pamoja na samaki, jibini, maharage, maziwa, mayai, karanga na vyakula vingine vya nafaka.

 

2. UGONJWA WA MAPAFU
KWA WATOTO (RESPIRATORY SYNCTIAL) Huu ni ugonjwa unaosababishwa na virusi viitwavyo (respiratory syncytial virus- RSV) ambavyo hushambulia mapafu ya mtoto na kumfanya ashindwe kupumua vizuri na atokwe na kamasi nyingi. Ugonjwa huu huweza kuwapata pia watu wazima ambapo huambatana na mafua makali lakini hali huwa mbaya zaidi kwa watoto. Dalili zake ni kama mtoto kutokwa na kamasi nyingi, kutokwa na vidonda kooni, kuumwa sana kichwa, kukohoa na homa kali. Kwa watoto, ugonjwa huu usipotibiwa, husababisha matatizo makubwa kwenye mapafu, moyo na kinga ya mwili ya mtoto.

 

Kwa bahati mbaya zaidi, ugonjwa huu husambaa kwa kasi kutoka kwa mtoto mmoja hadi mwingine kupitia njia ya hewa au kugusa kamasi au mate ya mgonjwa. Hii husababisha kama mtoto mmoja anaugua ugonjwa huu, kuwaambukiza wenzake wengi shuleni au sehemu wanapocheza kwa hiyo ni muhimu mtoto mwenye
ugonjwa huu akatibiwa haraka.

 

Ni vizuri wazazi wakawawahisha watoto wao hospitali, wanapoona dalili zake kwa sababu mara nyingi, wengi huuchanganya ugonjwa huu na mafua ya kawaida. Tofauti na mafua ya kawaida, ugonjwa huu hautibiwi kwa antibiotics za kawaida, ni lazima mtoto apelekwe hospitali, kupimwa na kupatiwa tiba sahihi. Baada ya kupata matibabu, mtoto mgonjwa hatakiwi kuchanganyikana na wenzake mpaka atakapoanza kupona. Unapoona dalili hizi, unashauriwa kuwahi hospitali haraka.

Leave A Reply