The House of Favourite Newspapers

Bila Kubadilika, Kiki Na Bifu Hazitasaidia Bongo Movie

0
Tamthiliya iliyohusisha ndoa ya Irene Uwoya na Dogo Janja.

 

MAISHA ni kitu cha ajabu kabisa. Leo mambo yanaweza yakawa mabaya kwa mtu fulani kiasi cha kila mmoja kumuonea huruma au hata kumcheka. Lakini dakika moja tu ya siku ikabadilisha kila kitu na ghafla, mtu dhahiri, aliyechekwa na kila mtu, akajikuta katika kiti cha enzi na kila mmoja akimshangilia kwa sifa za utukufu.

 

Vivyo hivyo kinyume chake. Mtu mmoja mwenye kila kitu, kesho anaweza kuwashangaza watu baada ya kuwa kila alichokuwa nacho sasa kubakia kuwa ni simulizi yenye kusikitisha. Hivi ndivyo ilivyo na hakuna mtu anaweza kusimama na kusema pale alipo hawezi kushuka, au kumsema mwenzake kuwa hawezi kufika sehemu fulani.

Usipitwe na Matukio, Install App Yako ya Kijanja na Namba Moja Tanzania ya Global Publishers

Android ===>Google Play

iOS ===>Apple Store

Hata hivyo, katika vitu ambavyo Mwenyezi Mungu amewapendelea binadamu, ni uwezo wao wa kujitambua na kupambana ili kubadilisha matokeo, yawe ya maisha au changamoto zozote zinazowakabili. Mtu anayeishi katika eneo lenye maji mengi wakati wa masika, lazima atatafuta namna ya kuishi nyakati hizo, kama siyo kurekebisha ardhi hiyo, basi atatafuta sehemu nyingine ili maisha yaendelee vizuri kwa siku zote za mwaka.

Wolper na mpenzi wake

Changamoto ziko nyingi katika kila kona za maisha, wengine huzipata katika biashara zao, wengine kazini mwao, baadhi kwenye utumishi wao kwa Mungu na kadhalika, ili mradi hata mchunga kondoo hulazimika kuhakikisha wote wanaingia zizini kwa wakati.

 

Inapotokea mtu akakubali kushindwa na changamoto na kuyaacha maisha yaende kwa kadiri yanavyokuja pasipo kuwa na nia ya kuboresha, ni wazi kuwa matokeo yake yatakuwa mabaya kila siku.

Hivi ndivyo unavyoweza kusimulia linapokuja suala la ubunifu wa wasanii wa muziki na filamu Bongo, ambao kwa kadiri muda unavyokwenda, wanaonekana kukosa mbinu mbadala za kukabili soko, isipokuwa kwa kutegemea matukio nje ya uwanja. Nazungumzia tukio la hivi karibuni la ujio wa tamthiliya iliyohusisha ndoa ya Irene Uwoya na Dogo Janja. Zaidi ya wasanii nane walikubaliana kushiriki uongo na kuusimamia ili kuwaaminisha watu kuwa hilo lilikuwa ni tukio la kweli, ili mradi tu, kuwapa watu ‘attention’.

 

Kwa nini walifanya hivyo? Ni kwa sababu soko la filamu hivi sasa linaonekana kuyumba baada ya waigizaji wake kukosa vitu vipya vya kuwashawishi watazamaji waweze kuvutiwa navyo. Wanaamini ukiwaambia watu kuhusu ujio wa tamthiliya mpya bila manjonjo kama haya ya fiksi, watu hawawezi kuvutiwa nayo. Na njia pekee ya kuwavutia wateja sokoni ni kuwapa matukio, badala ya kutengeneza kazi bora zaidi ya iliyopita, ili hata kama watatokea watazamaji wachache, basi waweze kuitangaza kwa wengine na
hatimaye kukubalika sokoni.

 

Ndiyo maana imetumika nguvu kubwa ya fedha kuweza kutengeneza uongo huo na kuwaacha watu sasa wasubiri hiyo tamthiliya ambayo ina ndoa ya Janjaro na Uwoya ndani yake. Kuendelea kwa wasanii wetu kuamini katika matukio nje ya sanaa, ndiko kumezalisha kitu kinaitwa bifu na sasa kiki. Vijana wetu hawapiti tena kutangaza kuhusu ujio wa kazi zao mpya kwa namna ya kusifia ubora, bali wanajiaminisha kwa kutengeneza bifu na kiki, hata zile za kujiaibisha ndiko kunaweza kuiweka kazi yao kuwa juu.

 

Pengine watu wanaweza kuvutika kuisikiliza au hata kuitazama kazi kutokana na bifu au kiki, lakini kama wasanii hawatakuwa makini kubuni vitu vinavyoongeza ubora wa kazi zao, matokeo yake ni kuzidi kudidimia kwa tasnia yao. Tengeneza kiki au bifu la kikazi, lakini basi kitu kinachofuata kiwe kimeandaliwa kwa ubora wa hali ya juu ili hata kama baadaye itajulikana kuwa ilikuwa ni danganya toto, lakini kazi ambayo watu watakutana nayo sokoni, wenyewe waseme ilistahili mshtuko.Ninachokiona kwa wasanii wetu ni kuwa hivi sasa wamejenga mazoea ya kuamini katika kiki na bifu pekee, huku kazi zao zikiendelea kuwa zilezile zenye matundu lukuki, hasa huku kwenye Bongo Movie.

Muandaaji: Ojuku Abraham, Mzee wa Bunduki

Usipitwe na Matukio, Install App Yako ya Kijanja na Namba Moja Tanzania ya Global Publishers

Android ===>Google Play

iOS ===>Apple Store

Leave A Reply