The House of Favourite Newspapers

Ukiona Dalili Hizi, Tambua Wewe Siyo Chaguo Lake

SAFARI ya mapenzi kati ya watu wawili wanaopendana, huanza kwa mmoja kati yao, hasa mwanaume kumtamkia nia yake yule anayempenda ingawa katika wakati huu tulionao, si ajabu pia kwa mwanamke kumtamkia mwanaume kwamba anampenda.  Mara zote matarajio ya yule anayemfikishia mwenzake ujumbe, huwa ni kukubaliwa kwa ombi lake na hivyo kuanzisha uhusiano wa kimapenzi. Hata hivyo, wasichokijua wengi ni kwamba siyo kila ombi linaweza kukubaliwa.

Hapa nawazungumzia watu wanaotaka kuingia kwenye uhusiano serious. Unaweza kumtongoza mwanamke ukiwa na lengo la kuanzisha naye uhusiano, ambao baadaye utaingia kwenye hatua ya uchumba na hatimaye ndoa! Unaweza kuanza kumuonesha mwanaume unayempenda ishara fulani za mapenzi. Umetokea kumpenda, moyo wako unamhitaji awe wako, mjenge familia!

Bila shaka majibu tayari unakuwa nayo, kwamba lazima atakubali! Hata kama atakuzungusha  lakini mwisho atakukubalia. Lakini je, huwa unafikiria kwamba ikitokea amekukataa itakuwaje? Kwa taarifa yako, siyo kila ombi linaweza kukubaliwa, kuna mwingine kwa sababu zake, hayupo tayari kuingia kwenye uhusiano na wewe.

Utafanya kila unachoweza lakini moyo wake haupo tayari. Utajuaje kama hayupo tayari kuingia kwenye uhusiano na wewe? Nini cha kufanya inapotokea hali kama hii? Twende pamoja utapata majibu ya maswali yako.

DALILI KWAMBA HAKUHITAJI

Kukubaliana na ukweli kwamba hakuhitaji, wewe siyo chaguo lake, huwa ni jambo gumu sana na wengi hujukuta wakitumia muda mrefu ‘kulazimisha’ mapenzi na kuishia kuumia. Ukiona dalili zifuatazo, tambua kwamba wewe siyo chaguo lake na hata ukiendelea kumng’ang’aniza, utakuwa unapoteza muda wako na kuutesa moyo wako bure.

  1. HAISHIWI VISINGIZIO

Ukiona kila unapopanga kukutana naye anatoa visingizio, hiyo ni dalili mbaya. Umeshamwambia kilichomo ndani ya moyo wako, hajakupa majibu yanayoeleweka lakini mkipanga mtoke ‘out’, iwe ni lunch, dinner au matembezi ya kawaida, dakika za mwisho anakwambia kwamba ana udhuru.

Leo atakwambia hajisikii vizuri, kesho atakwambia ana kazi, siku nyingine atakwambia hili au lile! Ukiona hali hii inazidi, kila siku anatoa ‘excuse’ ya kuonana na wewe, unatakiwa kujiongeza, hataki kuwa na wewe lakini anashindwa namna ya kukukataa.

  1. ANASISITIZA KUHUSU URAFIKI WA KAWAIDA

Ukiona mara kwa mara anasisitiza kwamba anataka muwe marafiki wa kawaida, anakuita majina kama rafiki, kaka, dada na kadhalika, hata pale unapojitutumua na kumtumia ujumbe wa kimapenzi, elewa kwamba huyo siyo riziki yako. Anajaribu kukufikishia ujumbe katika njia ambayo haitakuudhi.

  1. HATAKI MGUSANE

Ni kawaida kwa watu wanaopendana kushikana mikono, kugusana sehemu mbalimbali hata za kawaida, au wakati mwingine ‘ku-kiss’. Ukiona hapendi kabisa umshike hata mkono au kumgusa sehemu yoyote, hapendi umsogelee na hata inapotokea ukamgusa kwa bahati mbaya, haoneshi kuguswa kihisia, basi tambua kwamba mawazo yake hayapo kwako.

  1. ANAKUJIBU KWA MKATO

Unapotokea kumpenda mtu, ni kawaida kupenda kuwasiliana naye mara kwa mara. Utataka kujua yupo wapi, anafanya nini, amekula nini au siku yake ilikuwaje. Hata hivyo, ukiona majibu yake ni yale ya ‘shortcut’, kama ‘nipo’, ‘ok’, ‘sawa’, ‘poa’ na kadhalika, au wakati mwingine hakujibu kabisa, ukipiga simu wewe ndiyo unakuwa muongeaji yeye kazi yake ni kukuitikia tu, au wakati mwingine hapokei simu bila sababu, basi jua kwamba hajavutiwa na wewe.

  1. HATAKI MTU YEYOTE AKUJUE

Unapompenda mtu, utapenda watu wako wa karibu wamjue na yeye awajue, hali kadhalika kama amekupenda, hata kama bado hamjaingia kwenye uhusiano rasmi, atapenda kukutambulisha kwa watu wake wa karibu. Ukiona hataki watu wake wa karibu wakujue, unapaswa kuwa na walakini. Hapendi kukaa karibu na wewe, hapendi watu wengine wajue kwamba mna mawasiliano, hiyo ni dalili kwamba hana mpango wa kuwa na wewe. 

Comments are closed.