The House of Favourite Newspapers

Ukiumiza katika mapenzi

0

NI Jumanne tena. Jumanne yenye hekaheka ya kampeni ya uchaguzi mkuu wa mwezi ujao. Lakini kwa wasomaji wangu naamini mnajua kutenganisha muda wa kunisoma na muda wa kushiriki kampeni ili kusikia sera za vyao.

Mada yangu ya leo inaweza kuwa kali kwa maana ya ujumbe unavyosomeka kwenye kichwa cha habari; Ukiumiza Katika Mapenzi, Hufi Mpaka na Wewe Uumizwe!

Nimeamua kuandika mada hii kutokana na vilio vingi vya watu walioumizwa na mapenzi. Kusema kweli wengi wanaumizwa sana, hasa siku hizi. Hali ya uaminifu katika mapenzi haiko kama enzi za wazee wetu. Si kama enzi za mzee Anjelus (baba yangu).

NINI MAANA YA KUUMIZWA?

Kuumizwa katika mapenzi si kupigana au kujeruhiana, bali ni kile kitendo cha kuuvuruga uhusiano. Na kitendo hiki kwa kawaida hufanywa na upande mmoja bila ridhaa ya upande wa pili.

Mfano, una mtu wako. Awe mchumba, mke au mpenzi. Mnapendana sana. Na kila siku, kila mmoja anamhakikishia mwenzake kuhusu kudumisha uhusiano wenu.

Sasa ghafla inatokea mmoja anakata uhusiano huku penzi bado motomoto. Hapo si ina maana aliyekatiwa uhusiano lazima ataumia sana?

Au, wawili wanapendana, wanapanga mipango mingi ya mbele kuhusu mapenzi yao kiasi kwamba kila mmoja anaamua kuacha vyote ili kuimarisha penzi. Lakini siku inafika ghafla mmoja anaua uhusiano. Anakuwa hapokei simu, hatumi meseji tofauti na zamani mpaka mwenzake anajua hapa nimeshapigwa chini.

USALITI PIA

Lakini kuna suala la usaliti. Unaweza kukuta wawili wanapendana sana. Kila mmoja anajitoa kwa mwenzake. Inatokea siku moja mmoja anabaini mwenza wake anachepuka. Tena huenda anachepuka na mtu wa karibu au na rafiki wa mpenzi wake, inajulikana. Ina maana yule aliyejua ataumia sana na uhusiano utakufa.

KAULI ZA KUUMIZWA

Ndiyo maana utakuta mtu aliyesalitiwa akabaini na uhusiano ukafa anasema; ‘yaani nilimpa moyo wangu wote lakini leo kanitenda hivi, wala sikutegemea. Anatembea na rafiki yangu!!’

WAPO WANAOCHUKIA JINSIA

Mama Neema, mkazi wa Kimara, Dar yeye anasema kuwa, mwaka 2013 alikutana na mwanaume, wakapendana sana mpaka wakafikia kuweka mikakati ya kufunga ndoa.

“Lakini siku moja nikaja kugundua kuwa, kumbe Arusha ana mke na watoto wawili. Tena ni mke wa ndoa na wala ndoa yenyewe haijavunjika.

“Kwa kweli niliumia sana maana nilijiachia naye mpaka kwa wazazi wangu, ndugu na marafiki. Wote walimjua kama mchumba wangu.

“Kuanzia hapo, uhusiano ukafa na nikawa nawachukia sana wanaume. Kila mwanaume anayenitokea kunitongoza namuwazia yule jamaa wa mwanzo.”

HISTORIA INAVYOSEMA

Nimekuwa mfuatiliaji mzuri wa mikasa inayoanikwa kupitia filamu mbalimbali duniani, mara zote mtu anayemliza mwenzake kwenye mapenzi, hamalizi maisha yake ya duniani bila na yeye kulia. Lazima!

Kama utataka kuungana na mimi pitia kichwani mwako watu unaowafahamu au labda hata wewe mwenyewe, inawezekana uliwahi kulizwa lakini ukaja kubaini aliyekuliza naye amelizwa kwingine. Ipo kabisa hiyo.

Lengo la mada yangu ni kuwataka wapendanao kuishi kwa kupendana sana huku wakijua kuwa, kumuumiza mwenzako kuna malipo na malipo yake ni hapahapa duniani kabla hujafa! Tuonane wiki ijayo.

Leave A Reply